MASOMO
SOMO: Mdo.5:27-33
Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru
ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho
yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa
kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika
katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli
toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu
amewapa wote wamtiio. Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:1,8,15-19(K)6
1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
Heri mtu yule anayemtumaini.
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia.
2. Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,
Na masikio yake hukielekea kilio chao.
Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote. (K)
3. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
Mateso ya mwenye haki ni mengi,
Lakini Bwana humponya nayo yote. (K)
SHANGILIO: Yn.20:29
Aleluya, aleluya,
Umesadiki, Toma,
kwa kuwa umeniona,
wa heri wale wasioona,
wakasadiki.
Aleluya.
INJILI: Yn.3:31-36
Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia,
naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote. Yale aliyoyaona na
kuyasikia ndiyo anayoyashuhudia, wala hakuna anayeukubali ushuhuda wake. Yeye aliyeukubali
ushuhuda wake ametia muhuri ya kwamba Mungu ni kweli. Kwa kuwa yeye aliyetumwa na Mungu
huyanena maneno ya Mungu; kwa sababu hamtoi Roho kwa kipimo. Baba ampenda Mwana, naye amempa
vyote mkononi mwake. Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima,
bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.
MAOMBI
Ndugu, imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Lakini kwa nguvu zetu wenyewe hatuwezi. Tunahitaji
sana msaada wake. Basi tumwombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwalinde Baba Mtakatifu na viongozi wote wa Kanisa ili waendelee kumshuhudia Mwanao kwa mataifa yote.
2. Uwasaidie viongozi wetu wa serikali katika juhudi zao za kuziboresha na kuzilinda sheria za nchi
kwa manufaa ya raia wote.
3. Kanisa linalosafiri hapa duniani lisichoke kukutii wewe unayeongea nasi hata kwa njia ya wenzetu.
4. Marehemu waliomshuhudia Mwanao kwa ubatizo na maisha yao hapa duniani, wafufuliwe na kuishi milele
huko mbinguni.
Ee Baba Mungu, tunakiri kwamba Mwanao aliyetoka juu yu juu ya yote. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu
tuliyempokea, utuzidishie moyo wa kulikuza fumbo hili la Paska kwa mawazo, maneno na matendo
yanayotushuhudia, kwamba tunamwamini huyo uliyemtuma, ili tupate uzima wa milele. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.