Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 34
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Njooni mbele ya Bwana, mkiimba kwa furaha.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Peke yangu - wa pili wewe Mungu,
Nasafiri katika njia yangu;
Nihofu nini uwapo karibu,
Mtawala mchana na usiku?
Chini yako ni salama zaidi,
Kuliko kama 'ngelindwa na jeshi.

Saa ya kufa kwangu umepanga,
Mauti yaijua hiyo saa.
Hata 'ngezungukwa na jeshi kali
Halingeshinda nguvu za mauti;
Hazifai kitu kuta za mawe
Unapomtuma wako mjumbe.

Nitaishi kadiri ya amri,
Na kufuata yako maongozi,
Katika amani na utulivu,
Kwani duniani hapana nguvu
Iwezayo kuipokonya roho -.
Yake aliye mkononi mwako.

Ovu lo lote hawezi ogopa,
Mtoto wa Mungu, mteuliwa;
Mambo yetu yote twakuachia,
Lini tuende twangoja sikia.
Watufariji, Mfalme Mkuu,
Wewe Bwana u tumaini letu.

ANT. I: Ee Bwana, uziamshe nguvu zako, na uje kutusaidia.

Zab.80 Kwa ajili ya urekebisho wa Israeli
Njoo, Bwana Yesu (Ufu.22:20)

Utusikilize, ewe Mchungaji wa Israeli,*
unayewaongoza watu wako, Yosefu, kama kondoo.

Ewe ukaaye juu ya viumbe vyenye mabawa,/
ujioneshe kwa Efraimu, Benyamini na Manase.*
Uoneshe nguvu yako, uje ukatuokoe!

Uturekebishe, Ee Mungu;*
utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka.

Ee Mungu, Mungu mwenye nguvu,*
hata lini utazikasirikia sala za watu wako?

Umefanya huzuni iwe chakula chetu;*
umetunywesha machozi kwa wingi.

Umetufanya kisa cha ubishi kwa jirani zetu;*
adui zetu wanatudhihaki.

Ee Mungu mwenye nguvu, uturekebishe,*
utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka.

Ulileta mzabibu mmoja kutoka Misri;/
ukawafukuza watu wa mataifa mengine,*
na kuupanda katika nchi yao.

Uliupalilia upate kukua,*
nao ukatoa mizizi, ukaenea kote nchini.

Uliifunika milima kwa kivuli chake,*
na matawi yake yakawa kama mierezi mikubwa.

Matawi yake yalienea mpaka baharini;*
machipukizi yake mpaka kando ya mto Eufrate.

Mbona ulibomoa kuta zilizouzunguka?*
Sasa kila apitaye anachuma zabibu zake;

nguruwe-mwitu wanauharibu,*
na wanyama wa porini wanautafuna!

Ee Mungu mwenye nguvu, utugeukie tena!*
Uangalie toka mbinguni, uutunze mzabibu huo.

Uulinde huo mche ulioupanda kwa mkono wako;*
hicho kichipukizi ulichokisitawisha.

Watu walioukata na kuuteketeza,*
uwatazame kwa ukali, waangamie.

Mkono wako umkinge huyo uliyemfadhili;*
huyo uliyemteua kwa ajili yako.

Hatutakuacha na kukuasi tena;*
utujalie uzima, nasi tutakusifu.

Ee Mungu, Mungu mwenye nguvu, uturekebishe;*
utuangalie kwa wema, nasi tutasalimika.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, uziamshe nguvu zako, na uje kutusaidia.

ANT. II: Bwana ametenda maajabu, yatangazeni kwa ulimwengu mzima.

WIMBO: Isa.12:1-6 Furaha ya watu waliokombolewa
Aliye na kiu na aje kwangu anywe (Yoh.7:37)

Ee BWANA, nitakushukuru wewe;*
Kwa kuwa ijapokuwa ulinikasirikia,

Hasira yako imegeukia mbali,*
Nawe unanifariji moyo.

Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;*
Nitatumaini wala sitaogopa;

Maana BWANA ni nguvu zangu na wimbo wangu;*
Naye amekuwa wokovu wangu.

Basi, kwa furaha mtateka maji*
Katika visima vya wokovu.

Na katika siku hiyo mtasema,*
Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake;

Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,*
Litajeni jina lake kuwa limetukuka.

Mwimbieni BWANA; kwa kuwa ametenda makuu;*
Na yajulikane haya katika dunia yote.

Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sion;*
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana ametenda maajabu, yatangazeni kwa ulimwengu mzima.

ANT. III: Mshangilieni Mungu, aliye nguvu yetu.

Zab.81 Wimbo wa sikukuu
Basi, ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini (Ebr.3:12)

Mshangilieni Mungu, mlinzi wetu,*
mwimbieni sifa Mungu wa Yakobo;

Vumisheni wimbo wa shangwe, pigeni ngoma,*
chezeni kinubi na zeze zenye sauti nzuri.

Pigeni baragumu la mwezi mpya,*
na la mwezi mpevu, sikukuu yetu.

Hiyo ndiyo kanuni katika Israeli;*
hilo ndilo agizo la Mungu wa Yakobo.

Alimpa Yosefu agizo hilo,*
alipoishambulia nchi ya Misri.

Nasikia sauti nisiyoitambua ikisema:/
"Mimi nimekutua mizigo yako mabegani,*
nimekuondolea matofali uliyochukua mikononi.

Ukiwa shidani uliniita, nami nikakuokoa./
Nikiwa nimejificha katika ngurumo nilikujibu.*
Nilikujaribu kwenye maji ya Meriba.

Enyi watu wangu, sikilizeni onyo langu.*
Laiti ungenisikiliza, ee Israeli!

Asiwepo kwako mungu wa kigeni;*
usiabudu kamwe mungu mwingine.

Mimi ndimi Mungu, Mungu wako,/
niliyekuhamisha kutoka nchi ya Misri.*
Fungua kinywa chako, nami nitakulisha.

Lakini watu wangu hawakunisikiliza;*
Israeli hakupenda kunitii mimi.

Basi, nikawaacha wabaki na ukaidi wao;*
wafuate mashauri yao wenyewe.

Laiti watu wangu wangenisikiliza!*
Laiti Israeli angefuata mwongozo wangu!

Mara ningewaangamiza adui zao;*
ningewashinda wadhalimu wao.

Wanichukiao wangenipigia magoti kwa hofu,*
na adhabu yao ingekuwa ya milele.

Lakini wewe ningekulisha kwa ngano bora,*
na kukushibisha kwa asali ya mwambani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mshangilieni Mungu, aliye nguvu yetu.

SOMO: Rom.14:17-19
Utawala wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu. Anayemtumikia Kristo namna hiyo humpendeza Mungu, na hukubaliwa na watu. Kwa hiyo tuyazingatie daima mambo yenye kuleta amani, na yanayotusaidia kujengana.

KIITIKIZANO
K. Mapema asubuhi nitakutafakari, wewe Ee Bwana. (W. Warudie)
K. Umekuwa msaada wangu.
W. Wewe, Ee Bwana.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mapema...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Bwana, uwajulishe watu wako wokovu, na utusamehe dhambi zetu.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana, uwajulishe watu wako wokovu, na utusamehe dhambi zetu.

MAOMBI
Sifa iwe kwa Mungu, Baba yetu, asikiaye sala za watoto wake.
W. Bwana, utusikie.

Baba, tunakushukuru kwa kutuletea Mwana wako:
- tujalie tuweze kumwona kati yetu siku nzima ya leo. (W.)

Ifanye hekima iwe mwongozo wetu,
- utusaidie tutembee katika upya wa maisha. (W.)

Bwana, utupatie nguvu zako sisi wadhaifu:
- tunapokutana na matatizo, utujalie ujasiri wa kukabiliana nayo. (W.)

Uyaongoze mawazo, maneno na matendo yetu leo,
- ili tuweze kujua na kutekeleza matakwa yako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, Nuru ya kweli na Mwumba wa mwanga, utujalie, tukitafakari kiaminifu mambo yote yaliyo matakatifu, tuishi daima katika mwanga wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.