ALHAMISI JUMA 3 LA KWARESIMA
MASOMO

SOMO 1: Yer.7:23-28
Naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru, mpate kufanikiwa. Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kwa mashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele. Tokea siku ile baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku na kuwatuma. Lakini hawakunisikiliza, wala kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu; walitenda mabaya kuliko baba zao. Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini hawatakusikiliza; nawe utawaita; lakini hawatakuitikia. Nawe utawaambia, Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali vinywa vyao.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.95:1-2,6-9
1. Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi.

(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu.

2. Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba. (K)

3. Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)

4. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ya Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)

SHANGILIO: Zab.51:10,12
Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Unirudishie furaha ya wokovu wako.

INJILI: Lk.11:14-23
Yesu alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu. Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake. Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.

MAOMBI
Ee Bwana, umependa uwe Mungu wetu na sisi tuwe watu wako. Lakini sisi tunaelekea kuukataa mwaliko huo kwa kutenda dhambi. Kwa kuwa twaukiri na kuujutia udhaifu wetu, twakuomba ukubali kuipokea sala yetu tunayokuletea tukisema:

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uamshe ndani ya watu wako moyo wa kuisikia sauti yako inayotujia kwa njia ya manabii wako na kwa Maandiko yako Matakatifu.

2. Uwaonye wanaotafuta ishara na kumdhihaki Kristo wako, ili waukiri ukuu wake juu ya pepo wabaya.

3. Utujalie sote kumtumainia Mwanao Yesu Kristo ili, kwa nguvu yake kuu, tupate kuponywa maradhi ya kimwili na kiroho.

4. Utuimarishie imani yetu kwa Mwanao, ili tusiyumbishwe na mafundisho tofauti na potofu ya kigeni.

Utujalie hayo kwa njia ya Kristo Bwana na Mwokozi wetu daima na milele. Amina.