Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 4 LA KWARESIMA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Kristo Bwana alishawishiwa, na akateswa kwa ajili yetu. Njooni, tumwabudu.

Au
Aheri kama mngesikia sauti yake leo: msiwe na mioyo migumu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuiongie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI tazama pia AU
1 (15)
Mungu kwa huruma yako
Ututegee sikio
Kwa fadhili na wemao
Sisi ndo watoto wako,
Twakuomba zisikie
Sala na nadhiri zote
Watoazo watu wako.

'Toka kiti kitukufu
Tazama chini kwa wema,
Tujaze rohoni mwetu
Mng'aro wako mwenyewe,
Ondoa nyoyoni mwetu
Vivuli vyote vya giza,
Angaza hatua zetu.

Utuondolee dhambi
Kwa pendo lako kamambe,
Wachafu uwatakase,
Roho fungwa zifungue,
Wachilie wenye dhambi,
Na wote waloanguka
Kwa mkono wainue.

Utukuzwe Mungu Baba
Mungu Baba wa milele,
Na atukuzwe daima
Mwana wako wa pekee,
Ambaye pamoja naye
Roho wao atawala
Sawa nawe siku zote.
Ante-Tridentine Breviary


2 (16)
Ewe Mungu Muumbaji
Uliyetuumba sisi,
Kwako wewe tumetoka
Kwako sisi tunakuja
Kwa huruma watazama
Mioyo ya sisi watu,
Wewe waelewa kuwa
Utashi wetu dhaifu.

Utuhurumie Sisi
Dhambi zote tufanyazo,
Na hivyo uitakase
Kila roho ilo chafu.
Tulichokitia kiza
Wewe ukipe mwangaza,
Na tulichokiharibu
Ukipe ukamilifu.

Sheria na manabii
Walifundisha mfungo,
Ambao Wewe, E Kristo
Umeutakatifuza.
Ibariki yetu toba,
Na nguvu utupatie
Tushiriki msalaba
Ule uliofilia.

Ee Baba wa huruma,
Kristo wako Mwana,
Na Roho Mtakatifu,
Sikieni sala yetu;
Ninyi mwafanya Utatu
Tusoweza ufahamu
Katika huo Utatu
Viumbe vitatulia.
Stanbrook Abbey Hymnal


3 (17)
Bwana Yesu, nifikirie mimi
Na uniondolee dhambi zangu;
Nondolee vionjo vya kishenzi,
Unifanye safi moyoni mwangu.

Bwana Yesu, nifikirie mimi,
Nalemewa na tabu na shughuli;
Nifanye niwe wako mtumishi,
Na nionje raha ulotwahidi.

Bwana Yesu, nifikirie mimi
Ni kati ya mapambano makali;
Katika shida zote na uchungu
Uwe afya na uzima wangu.

Bwana Yesu, nifikirie mimi,
Wala usiniache nipotoke;
Katika giza, katika fadhaa
Unioneshe ya mbinguni njia.
Askofu Sinesio 375-430

4 (18)
Yesu jua la dunia
Ambayo mekombolewa,
Angazisha mwanga wako
Ndani kabisa mwa roho,
Kama siku za Chipuko
Jua linavyochomoza
Asubuhi kutangaza
Kwangamia kwa usiku.

Saa hii ya neema
Unayotushirikisha,
Utupe sisi mafunzo
Tumiminike machozi
Yakaondoe madoa
Kila moyo uwe safi
Unaotamani pata.
Kichomi chake upendo.

Ile siku imefika
Siku ilokubalika
Neema yajifunua
Upya ndo kama maua;
Tukifundishwa na wewe
Njia iliyo hakika,
Sisi tunashangilia
Zamu yetu kuchanua.

Na iiname kwabudu
Dunia yote kabisa
Mbele ya Mungu Mkuu
Penye kiti cha huruma,
Kama tufanyavyo sasa,
Ne'ma kisha tubadili,
Twasalimu mbele yako,
Tunakupa sifa mpya.
Karne ya 6


5 (19)
Sasa sote kwa umoja,
Tukijumuika pamwe
Na zama zilizopita,
Tukeshe pamoja naye
Wa mbinguni wetu Bwana
Katika majaribuye,
Katika wake mfungo
Leo tumwunge mkono.

Agano lile la kale
Kale lilofunuliwa
Kwa watu waaminifu
Watu wa zamani hizo,
Kristo kwa wake mfano
Aliidhinisha hilo;
Naye ndo Bwana wa pendo,
Katika pendo azizi.

Kumbuka, Bwana, kumbuka,
Hata kama tu dhaifu,
Tuliumbwa na mwenyewe
Kwa mkono wako mwema;
Basi utusaidie
Udhaifu wetu sie
Usifanye lako jina
Lisalitiwe vibaya.

Utusikie twaomba,
E Utatu mtukufu,
Umoja ulo mmoja,
Na usiogawanyika;
Jalia kipindi hiki,
Kipindi kitakatifu,
Kilete mengi matunda,
Kizae matunda bora.
Mt.Gregori Mkuu 540-604

ANT. I: Ee Bwana, uniwezeshe kulitambua pendo lako asubuhi.

Zab.143:1-11 Sala ya kuomba msaada
Mtu hawezi kuwa na uhusiano mwema na Mungu kwa kutii Sheria, bali tu kwa kumwamini Yesu Kristo (Gal.2:16)

Ee Mungu, usikie sala yangu!/
Kwa ajili ya uadilifu wako sikiliza ombi langu!*
Unijibu kwa ajili ya uaminifu wako.

Usinitie mimi mtumishi wako hukumuni,*
maana hakuna mtu aliye mwadilifu mbele yako.

Adui amenifuatia na kunisagasaga kabisa;*
ameniingiza gizani kama mtu aliyekufa zamani.

Nimevunjika moyo kabisa;*
nimekufa ganzi kwa ajili ya woga.

Nakumbuka siku zilizopita;/
natafakari juu ya yote uliyotenda,*
nawaza na kuwazua juu ya matendo yako.

Nanyosha mikono yangu kuomba;*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Ee Mungu, unisikilize hima;*
nimekata tamaa kabisa!

Usijifiche mbali nami,*
nisije nikafanana na wale washukao shimoni.

Asubuhi unijulishe upendo wako mkuu,*
maana nakutumainia wewe.

Nakutolea moyo wangu;*
unioneshe njia ya kwenda.

Uniopoe na adui zangu, Ee Mungu,*
maana nakimbilia kwako.

Unifundishe kutimiza matakwa yako,/
maana wewe ni Mungu wangu!*
Kwa wema wako uniongoze katika njia iliyo sawa.

Uniweke salama, Ee Mungu,/
kwa ajili ya jina lako;*
kwa uadilifu wako, uniokoe taabuni.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, uniwezeshe kulitambua pendo lako asubuhi.

ANT. II: Bwana ataleta amani Yerusalemu, amani ifurikayo kama kijito.

WIMBO: Isa.66:10-14a Kitulizo na furaha katika mji mtakatifu
Yerusalemu ya juu mbinguni ni mji ulio huru, nao ni mama yetu (Gal.4:26)

Furahini pamoja na Yerusalemu,/
Shangilieni kwa ajili yake,*
Ninyi nyote mmpendaye;

furahini pamoja naye kwa furaha,*
ninyi nyote mliao kwa ajili yake;

Mpate kunyonya, na kushibishwa*
kwa maziwa ya faraja zake,

mpate kukama, na kufurahiwa*
kwa wingi wa utukufu wake.

Maana BWANA asema hivi,/
Tazama, nitamwelekezea amani kama mto,*
na utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho,

nanyi mtapata kunyonya;*
mtabebwa; na juu ya magoti mtabembelezwa.

Mfano wa mtu ambaye mama yake amfariji,/
ndivyo nitakavyowafariji ninyi;*
nanyi mtafarijiwa katika Yerusalemu;

Nanyi mtaona, na mioyo yenu itafurahi,/
na mifupa yenu itasitawi*
Kama majani mabichi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana ataleta amani Yerusalemu, amani ifurikayo kama kijito.

ANT. III: Sifa na shangwe kwa Mungu wetu.

Zab.147:1-11 Ni vizuri kumsifu Mungu
Tunakuabudu, Ee Mungu; Ee Bwana, tunakusujudia

Ni vema kumwimbia Mungu wetu sifa;*
ni vizuri na sawa kabisa kumsifu.

Mungu anaurekebisha mji wa Yerusalemu.*
Anawarudisha salama wakimbizi wake.

Anawaponya waliovunjika moyo;*
anawatibu majeraha yao.

Ameiweka idadi ya nyota,*
na kuzipa kila moja jina.

Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi;*
maarifa yake hayana kipimo.

Mungu huwakweza wanyenyekevu,*
lakini huwatupa waovu mavumbini.

Mwimbieni Mungu nyimbo za shukrani,*
mpigieni kinubi Mungu wetu!

Yeye hulifunika anga kwa mawingu,/
huitengenezea dunia mvua,*
na kuchipusha nyasi vilimani.

Huwapa wanyama chakula chao,*
na kulisha makinda ya kunguru wanaolia.

Yeye hapendezwi na nguvu za farasi,*
wala hafarijiki kwa ushujaa wa askari;

lakini hupendezwa na watu wamchao,*
watu wanaotegemea upendo wake mkuu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Sifa na shangwe kwa Mungu wetu.

SOMO: 1Fal.8:51-53a
Sisi ni watu wako, Bwana, na urithi wako. Macho yako na yafumbuke, na kuielekea dua ya mtumishi wako, na dua za watu wako Israeli, ukatusikilize kila wakati tutakapokulilia. Kwa maana ulitutenga na watu wote wa dunia, tuwe urithi wako.

KIITIKIZANO
K. Yeye ndiye atakayeniopoa kutoka katika mtego wa wawindaji. (W. Warudie)
K. Na kutoka katika hila zao.
W. Ataniopoa yeye.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Yeye ndiye...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Bwana asema, sitegemei ushuhuda wa binadamu, lakini nimesema hayo ili ninyi mpate kuokoka.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana asema, sitegemei ushuhuda wa binadamu, lakini nimesema hayo ili ninyi mpate kuokoka.

MAOMBI
Tumtukuze Mungu kwa ajili ya upendo wake mkuu, ambao umefunuliwa kwetu katika Yesu Kristo.
W. Bwana, kumbuka kuwa sisi ni watoto wako.

Utuingize zaidi na zaidi katika maisha ya Kanisa lako;
- na kwa njia yetu, uliwezeshe Kanisa kuwa alama wazi zaidi ya wokovu wa dunia. (W.)

Wewe unayewapenda wanadamu, utusaidie kutimiza wajibu wetu katika kukuza jumuiya zetu,
- na utusaidie tuweze kuimarisha utawala wako kwa kila njia. (W.)

Utuwezeshe kumwendea Kristo tunapoelemewa na matatizo,
- kwa kuwa yeye ni chemchemi ya maji ya uzima, ambaye anawaburudisha wote waonao kiu. (W.)

Utusamehe kwa madhara yote tuliyofanya,
- utuongoze katika njia ya haki na ukweli. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana mwenye huruma, umetutakasa kwa toba, na umetufunza kutenda mema; utujalie tudumu kwa moyo mmoja katika kushika amri zako, na utufikishe bila dhambi kwenye furaha za Pasaka. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.