ALHAMISI JUMA 4 LA KWARESIMA
MASOMO
SOMO 1: Kut.32:7-14
Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu
nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha, wakaiabudu na
kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Tena
Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu; basi sasa niache,
ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize; nami ninakufanya wewe uwe taifa kuu. Musa akamsihi sana
Bwana, Mungu wake, na kusema, Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka
nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa
kwa kuwatenda uovu, ilia pate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika
hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli,
watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota
za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu, nao watairithi milele. Na Bwana
akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.106:19-23
1. Walifanya ndama huko Horebu,
Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
Wakaubadili utukufu wao
Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani.
(K) Ee Bwana unikumbuke mimi,
kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.
2. Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,
Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.
Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,
Aliyetenda makuu katika Misri. (K)
3. Akasema ya kuwa atawaangamiza,
Kama Musa, mteule wake, asingalisimama,
Mbele zake kama mahali palipobomoka,
Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. (K)
SHANGILIO: Mt.4:17
Tubuni, asema Bwana,
kwa maana ufalme wa mbinguni
umekaribia.
INJILI: Yn.5:31-47
Yesu aliwambia Wayahudi: Mimi nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Yuko mwingine
anayeshuhudia; nami najua ya kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli. Ninyi mlituma watu kwa
Yohane, naye akaishuhudia kweli. Lakini mimi siupokei ushuhuda kwa wanadamu; walakini ninasema
haya ili ninyi mpate kuokoka. Yeye alikuwa taa iwakayo na kung’aa, nanyi mlipenda kuishangilia
nuru yake kwa muda. Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohane; kwa kuwa zile
kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba
amenituma. Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wowote, wala sura
yake hamkuiona. Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa
na yeye. Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake;
na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu
kwa wanadamu. Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu. Mimi nimekuja kwa
jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo.
Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye
wa pekee hamuutafuti? Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa,
mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika
habari zangu. Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini wapi maneno yangu?
MAOMBI
Ndugu wapendwa, kumwamini na kumpenda Mungu ni kuwaamini na kuwapenda wajumbe wake anaowatuma kwetu. Tunahitaji
neema ya Mungu, ili tuongezewe hekima yake. Basi, tuombe: Ee Mungu twakuomba:-
Kiitikio: Mungu wa huruma, utusikie.
1. Mfungo huu wa Kwaresima uwaneemeshe makasisi wetu, ili waongezewe ari ya kumshuhudia Mwanao kwa mahubiri mazuri
yasio na woga wowote ndani yake.
2. Uzibariki juhudi za viongozi wetu wa serikali na vyama vya siasa za kutafuta ukweli, haki na amani duniani.
3. Utujalie sisi sote kuepa dhambi na kuwa mstari wa mbele katika kuwashauri na kuwaombea wakosefu wapate kurudi
kwako.
4. Uwasamehe wale wote wanaoleta makwazo katika mfungo huu wa Kwaresima na uwajengee mazingira ya kujirudi, ili
tufurahie ufufuko wa Mwanao pamoja nao.
Ee Baba Mungu, ukubali kuyapokea maombi yetu kama ulivyopokea sala ya Musa mtumishi wako alipowaombea wakosefu.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.