Generic placeholder image

ALHAMISI JUMA LA 4 LA KWARESIMA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina.

UTENZI
Baba wa milele, Mungu wa pendo,
Ambaye kwa vumbi ulituumba,
Tugeuze kwa neema ya Roho,
Tutie thamani tulio duni.

Utuandae kwa siku ya siku
Atakapokuja Kristo kwa enzi
Kutugeuza tena toka vumbi
Na miili yetu kuing'arisha.

Ee Mungu hujaonwa, hujaguswa,
Viumbe vyote vyakudhihirisha;
Mbegu ya utukufu ndani mwetu
Itachanua tutapokuona.

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Huu ndio wakati wetu wa kutubu, wakati wa kulipa kwa ajili ya dhambi zetu, na wa kutafuta wokovu.

Adhuhuri
Ant.: 'Hakika,' asema Bwana, 'sifurahii kifo cha mtu mwovu, bali auache mwenendo wake mbaya, apate kuishi.'

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Tukiwa tumevaa haki ambayo ni nguvu ya Mungu, na tuoneshe ustahimilivu mkuu.

Zab.119:153-160 XX Kuomba msaada
Uangalie mateso yangu, uniokoe,*
kwa maana sikusahau sheria yako.

Unitetee na kunikomboa;*
unisalimishe kama ulivyoahidi.

Waovu hawataokolewa,*
maana hawazijali kanuni zako.

Huruma yako ni kubwa, Ee Mungu;*
Unijalie uhai kama ulivyoahidi.

Adui na wadhalimu wangu ni wengi,*
lakini mimi sikiuki maagizo yako.

Niwaonapo wahaini hao nachukizwa mno,*
kwa sababu hawazishiki amri zako.

Tazama, Ee Mungu, jinsi nizipendavyo amri zako!*
Unisalimishe kadiri ya upendo wako mkuu.

Kitovu cha sheria yako ni ukweli,*
hukumu zako za haki, zote ni za milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.128 Tuzo kwa jamaa imchayo Mungu
'Bwana akubariki kutoka Sion,' yaani kutoka Kanisa lake (Arnobius)

Heri wote wamchao Mungu,*
wanaoishi kufuatana na amri zake.

Kazi zako zitakupatia mahitaji yako,*
utaona furaha na kufanikiwa.

Mke wako atakuwa kama mzabibu*
wenye matunda mengi nyumbani mwako;

watoto wako watakuwa kama machipukizi*
ya mizeituni kuizunguka meza yako.

Naam, ndivyo atakavyobarikiwa*
mtu amchaye Mungu.

Mungu akubariki toka Sion!/
Uione fanaka ya Yerusalemu,*
siku zote za maisha yako.

Uishi na hata uwaone wajukuu wako!*
Amani iwe na Israeli!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.129 Sala dhidi ya adui za Israeli
Kanisa lasimulia mateso linayovumilia (Mt. Augustino)

Israeli anasema:/
"Mara nyingi adui wamenitesa,*
tangu ujana wangu!

Naam, wamenitesa tangu ujana wangu,*
lakini hawakuweza kunishinda.

Walinikatakata mgongoni mwangu,*
waliufanya kama shamba lililolimwa.

Lakini Mungu ni mwadilifu;*
amezikata kamba za hao waovu.“

Waaibishwe na kushindwa kabisa*.
wote wale wauchukiao mji wa Sion.

Wote wafanane na nyasi juu ya paa la nyumba,*
ambazo hunyauka kabla hazijakua;

hakuna anayejishughulisha kuzikusanya,*
wala kuzichukua kama matita.

Hakuna apitaye karibu atakayewaambia:/
"Mungu awabariki!*
Twawabariki kwa jina la Mungu.“

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Huu ndio wakati wetu wa kutubu, wakati wa kulipa kwa ajili ya dhambi zetu, na wa kutafuta wokovu.

Adhuhuri
Ant.: 'Hakika,' asema Bwana, 'sifurahii kifo cha mtu mwovu, bali auache mwenendo wake mbaya, apate kuishi.'

Baada ya Adhuhuri
Ant.: Tukiwa tumevaa haki ambayo ni nguvu ya Mungu, na tuoneshe ustahimilivu mkuu.

MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Isa.55:6-7
Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.

K. Uniumbie moyo safi, Ee Mungu.
W. Unitie roho imara ndani yangu.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Adhuhuri: Kum.30:2-3a
Nawe utakapomrudia BWANA, Mungu wako, na kuitii sauti yake, mfano wa yote nikuagizayo leo, wewe na wanao, kwa moyo wote, na kwa roho yako yote; ndipo BWANA, Mungu wako, atakapougeuza utumwa wako, naye atakuhurumia.

K. Usizitazame dhambi zangu.
W. Na uifutilie mbali hatia yangu.

Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Ebr.10:35-36
Basi, msipoteze uhodari wenu, maana utawapatieni tuzo kubwa. Mnahitaji kuwa na uvumilivu, ili mweze kufanya anayotaka Mungu na kupokea kile alichoahidi.

K. Sadaka yangu ni moyo wa majuto.
W. Moyo mnyenyekevu na wenye toba, Ee Mungu, hutausukumia mbali.

SALA:
Tuombe: Bwana mwenye huruma, umetutakasa kwa toba, na umetufunza kutenda mema; utujalie tudumu kwa moyo mmoja katika kushika amri zako, na utufikishe bila dhambi kwenye furaha za Pasaka. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.