ALHAMISI BAADA YA JUMATANO YA MAJIVU
MASOMO

SOMO 1: Kum.30:15-20
Musa aliwaambia watu akisema: Aangalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki. Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia; nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia; hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki. Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti Baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani huyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.1:1-4, 6
1. Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.

(K) Heri mtu aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.

2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)

3. Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)

SHANGILIO: Zab.130:5
Nimemngoja Bwana, roho yangu imemngoja, na neno lake nimelitumaini. Nafsi yangu inamngoja Bwana, kuliko walinzi waingojavyo asubuhi, naam, walinzi waingojao asubuhi.

INJILI: Lk.9:22-25
Siku ile: Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. Akawaambia wote, Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, na kujipoteza mwenyewe?

MAOMBI
Ndugu zangu, Mwana wa Mtu anatabiri ufufuko utakaotanguliwa na mateso mengi na kifo. Tuombe ili nasi tupate kutimiza matakwa yake.

Kiitikio: Kwa huruma yako, utusikie.
1. Viongozi wote wa Kanisa wazidi kuwa mfano mwema na kutukumbusha kuwa kila mwanafunzi wa Yesu yampasa kujikana mwenyewe, kuubeba msalaba wake kila siku na kumfuata.

2. Watawala wa nchi, wanasiasa na wote wenye mamlaka katika jamii zetu waenende katika njia za Bwana na kuwatumikia watu wao kwa mapendo.

3. Sisi sote tuliowekewa mbele yetu uzima na mema, mauti na mabaya, tujaliwe busara ya kuchagua daima yale yakupendezayo wewe na jirani zetu.

4. Marehemu wetu washirikishwe ufufuko wa Kristo na kupewa uzima wa milele huko mbinguni.

Hayo yote tunayaomba kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.