SIKUKUU YA EPIFANIA
Masomo Misa ya siku
ANTIFONA YA KUINGIA: Mal.3:1; 1Nya.29:12
Tazama anakuja Bwana Mtawala, mwenye ufalme mkononi mwake, na uweza na nguvu.
Utukufu husemwa
KOLEKTA:
Ee Mungu, siku ya leo ulimfunua Mwanao pekee kwa mataifa wakiongozwa na nyota. Utujalie kwa
wema ili sisi, tuliokwisha kukutambua kwa imani, tuongozwe hadi kukutazama katika uzuri wa
ukuu wako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika
umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Isa.60:1-6
Ondoka, ee Yerusalemu, uangaze; Kwa kuwa nuru yako imekuja Na utukufu wa Bwana umekuzukia.
Maana, tazama, giza litaifunika dunia, Na giza kuu litazifunika kabila za watu; Bali Bwana
atakuzukia wewe, Na utukufu wake utaonekana juu yako. Na mataifa wataijilia nuru yako, Na
wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako. Inua macho yako, utazame pande zote; Wote wanakusanyana;
wanakujia wewe; Wana wako watakuja kutoka mbali, Na binti zako watabebwa nyongani. Ndipo utakapoona
na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia,
Utajiri wa mataifa utakuwasilia. Wingi wa ngamia utakufunika, Ngamia vijana wa Midiani na Efa; Wote
watakuja kutoka Sheba; Wataleta dhahabu na uvumba; Na kuzitangaza sifa za Bwana.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.72: 1-2,7-8,10-13 (K)11
1. Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako.
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu.
(K) Mataifa yote ya ulimwengu,
Watakusujudia, ee Bwana.
2. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka mto hata miisho ya dunia. (K)
3. Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi,
Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.
Naam, wafalme wote na wamsujudie;
Na mataifa yote wamtumikie. (K)
4. Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini.
Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)
SOMO 2: Efe.3:2-3,5-6
Ndugu zangu: Ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya
kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi
vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho: ya
kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja
nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.
SHANGILIO: Mt.2:2
Aleluya, aleluya!
Tuliona nyota yake mashariki,
Nasi tumekuja kumsujudia.
Aleluya!
INJILI: Mt.2:1-12
Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki
walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota
yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu
pia pamoja naye. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao: Kristo
azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na Nabii,
Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda, kwa kuwa kwako atatoka
mtawala atakayewachunga watu wangu Israeli. Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao
hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota. Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize
sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie. Nao
waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia,
hata ikaenda ikasimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha
kubwa mno. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao
walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane. Nao wakiisha kuonywa
na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Ndugu, tupeleke sasa maombi yetu mbele ya Mungu ambaye amejifunua kwa mataifa
kwa njia ya Mwana wake, Kristo Bwana. Tumuombe Mungu Baba. Ee Mungu, mtawala mkuu, twakuomba,
1. Kanisa letu liwe mwanga unaoangaza dunia yote kwa kushuhudia kwamba Wewe ndiwe Mungu na Mkuu wa vyote.
2. Viongozi wa dunia wakukiri Wewe kuwa ndiwe mwenye mamlaka na enzi yote hapa duniani na huko mbinguni
na watumie madaraka yao kwa manufaa ya watu.
3. Watu wote wapate kukutambua Wewe uliyejifunua kwetu sisi kwa njia ya Mwanao Yesu Kristo.
4. Ututie moyo wa kumtafuta na kumsujudia Kristo Mwanao kwa njia ya kuwahudumia wenzetu wenye shida kama
vile wagonjwa, yatima, wajane na wasiojiweza.
5. Uwasaidie Wamisionari waliotumwa kuhubiri Habari Njema, wasichoke kumshuhudia Kristo Mwanao, Mfalme
na Mkombozi wa dunia.
Ee Mungu wa milele, tunakuomba upokee na usikilize maombi yetu kwa jina la
Kristo, Bwana wetu. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba uvitazame kwa wema vipaji vya Kanisa lako. Kwa njia ya hivyo, havitolewi
tena dhahabu, ubani na manemane, ila yule ambaye katika tunu hizo anatangazwa, anatolewa sadaka
na kupokewa, yaani Yesu Kristo. Anayeishi na kutawala milele na milele.
EPIFANIA YA BWANA: Kristo mwanga wa mataifa.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote,
ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Maana, leo, Wewe mwenyewe umefunua
fumbo la wokovu wetu katika Kristo kuwa mwanga wa mataifa. Alipotokea katika hali yetu yenye
kufa, Wewe ulitutengeneza katika hali mpya ya utukufu wake wa milele.
Kwa sababu hiyo, sisi
pamoja na Malaika na Malaika Wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, na majeshi yote ya Malaika
wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho:
W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Mt.2:2
Tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja na zawadi kumsujudia Bwana.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunakusihi, ututangulie daima na popote kwa nuru yako ya mbinguni, ili fumbo hili
ulilotaka kutushirikisha tulitazame kwa macho safi na kulipokea kwa upendo unaostahili. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu.