SIKUKUU YA FAMILIYA TAKATIFU
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Njooni, tumwimbie Bwana; tumfanyie shangwe Mungu anayetuokoa, Aleluya.
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
TENZI angalia pia AU
AU
6
Ua lake Yuda, ua azizi,
Limechipuka kwenye mizizi,
Mizizi ambayo ni teketeke,
Waridi la kwenye Shina la Yese,
Kama walivyoimba manabii:
Limechipuka kwenye mizizi,
Majira ya baridi hilo ua
Tafanya usiku upambazuke.
Waridi rembo na lenye neema,
Ambalo Isaya analiimba,
Ni wewe Mama Bikira Maria
Na Kristo ni ua unalochipua;
Kwa amri kamambe yake Mungu;
Maria ulimzaa Mwokozi
Ulimzaa Mpenzi wa sisi
Ambaye akafa atukomboe.
Maria wewe u mama mpenzi,
Sisi tunakuomba mama kwa dhati,
Twasihi kwa mioyo yetu yote:
Jalia huyo mwanao mchanga
Madhambi yetu atuondolee,
Kwa upendo wake atuongoze
Tuweze kwishi naye huko juu
Pia tumtumikie milele.
Karne ya 15
AU
7
Kutoka lichomozeako jua
Hadi lizamiako magharibi,
Kwa Kristo Mfalme heshima twatoa,
Alozaliwa leo na Bikira.
Mwumba Mtukufu ulijishusha
Uwe mtwana kwa ajili yetu,
Mwili hadhi ukaurudishia
Sisi viumbe tupate kuishi.
Tumbo la uzazi safi likaa
Lililojaa neema za mbingu;
Wala Bikira hakuweza sema
Mgeni wake katokea wapi.
Kutoka juu Mungu alikuja
Kuuhifadhi utukufu wake
Kifuani mwa asiye na dhambi,
Bikira aliyejaa utii.
Bikira imani alionesha
Kwa neno lililotoka kwa Mungu,
Na hapo ndipo akapata mimba
Bila kuwa na hatia yo yote.
Kishapo Mtoto akamzaa,
Alivyojulishwa na Gabrieli;
Huyo ndo Mtoto alotangazwa
Na mtangulizi kabla yake.
Alilala fofofo majanini
Ndani ya chombo cha kulishia ng'ombe;
Alinyonya maziwa ya mamake,
Yeye ambaye huwalisha wote.
Utukufu kwa Mungu! yasikika,
Hao malaika juu waimba;
Mchungaji, Bwana wa watu wote
Aabudiwa kwanza na wachunga.
Karne ya 5
AU
8
Kristo kwa ajili ya watu
Damu yako ndo ilitiririka,
Wewe u nuru iliyoangaza
Kabla haijawa asubuhi,
Wewe Bwana hakika ndiwe Mungu
Nawe milele ni Mwana wa Mungu,
Tena Wewe pamoja naye Baba
Nyie ni Mungu mmoja milele;
Ewe uliye mng'ao azizi
Utokanao na Nuru ya Baba,
U nyota iletayo tumaini
Ambayo daima yametameta,
Zisikilize basi twakuomba
Sala zenye kukumiminikia,
Kutoka huku chini duniani
Watumishi wako wanazosali.
Ee Bwana ukumbuke ya kuwa
Ni kwa sababu ya upendo wako
Wewe ulikiacha kule juu
Kile kiti chako cha enzi kuu
Chini ukaja upate kutwaa
Hali dhaifu ya kibinadamu,
Na ndipo mimba ukachukuliwa,
Na Mama aliye safi Bikira.
Kwa hiyo usikubali ardhi
Iwe peke yake yashangilia,
Bali hata bahari na uwingu
Pamoja vichange zao sauti,
Kusudi na uimbwe wimbo mpya
Wa kuishangilia asubuhi
Ile ya siku alipozaliwa
Yeye aliye Bwana wa uzima.
Ewe aliyekuzaa bikira
Ni wewe wa kuzipokea sifa,
Haya, hivi sasa tunakusifu,
Na milele uwe unasifiwa;
Baba naye pia apewe sifa
Kama hizo utolewazo Mwana,
Hizo pia na zimwendee Roho,
Ninyi msifiwe milele yote.
AU
9
Njooni, wamini wote,
Kwa furaha na kwa shangwe,
Njooni Betlehemu
Njooni mpate mwona
Mfalme alozaliwa,
Mfalme wa Malaika.
W.
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Ni Mungu sawa na Mungu,
Ni Nuru kutoka Nuru,
Lile tumbo la uzazi
La bikira hachukii;
Yeye ni Mungu halisi
Ana baba, hakuumbwa.
W.
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Imbeni, nyi malaika,
Imbeni kwa shangwe kuu,
Imbeni, wakazi wote
Wa huko mbinguni juu;.
'Utukufu kwako Mungu
Uliye mbinguni juu.'
W.
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Bwana tunakusalimu,
Uliyezaliwa leo
Asubuhi ya furaha,
Utukuzwe Bwana Yesu,
Neno wake Baba Mungu
Sasa u katika mwili.
W.
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Karne ya 18
AU
10
Tumempata sisi
Tumepewa mtoto,
Analeta uhuru
Kristo Mwokozi,
Yeye ni Mshauri
Ni Baba wa milele,
Mungu aliye mtu,
Mfalme wa Amani.
Mamake ni Maria
Bikira na mpole,
Hiyo kazi ya Roho,
Roho yule wa Bwana;
Huyo alitamkwa
Kale tangu milele:
Huyu ndiye ni Neno
Wake Baba Mwenyezi.
Ndaniye tachanua
Upendo na ukweli,
Navyo tatenda kazi
Kwa nguvu zake Neno.
Matawi yaso kitu
Maua yatapata;
Furaha ilolala
Yaanza kuamka.
Na apatiwe sifa
Baba alo milele,
Pia na Neno wake
Mwanae wa pekee,
Pamoja nao pia
Roho Mtakatifu
Ni Utatu kamili
Na ni Mungu mmoja.
AU
11
Alozawa na upendo wa Baba
Kabla ya ulimwengu kuumbwa,
Yeye ndiye Alfa na Omega,
Yeye ni chanzo, yeye ni kikomo
Cha vilivyo na vilivyokuwapo
Na vitavyoonekana badaye:
Kwa milele na milele.
Ilibarikiwa milele siku
Bikira - aliyejaa neema,
Mwenye mimba kwa uwezo wa Roho-
Alipomzaa Mwokozi wetu,
Naye Mkombozi wa ulimwengu
Alipoonesha kwanza usowe:
Kwa milele na milele.
Atukuzwe Mungu Baba Mwenyezi,
Atukuzwe Mungu Mwana Mwokozi,
Atukuzwe Roho Mtakatifu,
Umungu mmoja, Nafsi tatu.
Viumbe vyote na vimtukuze
Mwenyezi Mungu kwa nyakati zote:
Kwa milele na milele.
Aurelio C. Prudensio
348-yapata 413
AU
12
Kristo huyu hapa,
Mwenyewe Emanueli,
Yeye ndiye mtukufu
Na ni mpole ajabu:
Hekima nayo neema,
Hekima nao ukweli
Vipo ila mefichama
Katika huyu Mtoto.
Vile Mungu alitaka
Yesu ndipo kaumbika,
Kristo ndiye Mwanga
Aliyetoka kwa Mwanga,
Amekuja waokoa
Waana wake Adamu
Ambao wanangojea
Katika giza - usiku.
Sifa kwa Baba na Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Utukufu wao hao
Wa mbinguni wanaimba,
Na walio duniani
Kwa sauti ilo kuu
Sawia wanausifu
Utatu wauabudu.
Stanbrook Abbey Hymnal
ANT. I: Wazazi wa Yesu walikuwa wakienda Yerusalemu kila mwaka,
kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka.
Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.
Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.
Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.
Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.
Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.
Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.
Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.
Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;
maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.
Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Wazazi wa Yesu walikuwa wakienda Yerusalemu kila mwaka,
kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka.
ANT. II: Mtoto alizidi kukua, akapata nguvu na kujaa hekima; na
neema ya Mungu ikawa pamoja naye.
WIMBO: Dan:3.37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)
Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.
Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.
Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.
Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.
Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.
Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.
Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.
Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.
Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.
Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.
Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.
Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.
Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.
Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.
Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Ant. II: Mtoto alizidi kukua, akapata nguvu na kujaa hekima; na
neema ya Mungu ikawa pamoja naye.
ANT. III: Baba na mama yake walistaajabia yaliyokuwa yanasemwa juu yake.
Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo,
mfalme wao (Hesychius)
Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!
Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.
Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.
Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.
Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.
Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,
ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;
wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.
kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Baba na mama yake walistaajabia yaliyokuwa yanasemwa juu yake.
SOMO: Kum.5:16
Waheshimu baba yako na mama yako; kama BWANA Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi,
nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako.
KIITIKIZANO
K. Kristo, Mwana wa Mungu Aliye Hai, utuhurumie. (W. Warudie)
K. Uliyewatii Maria na Yosefu.
W. Utuhurumie
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Kristo, Mwana...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Bwana, tunaomba mfano wa familia yako takatifu uangaze akili zetu; ielekeze miguu yetu kwenye
njia ya amani.
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Bwana, tunaomba mfano wa familia yako takatifu uangaze akili zetu;
ielekeze miguu yetu kwenye njia ya amani.
MAOMBI
Tumwabudu Mwana wa Mungu Aliye Hai, aliyepata kuwa mwana katika familia ya kibinadamu.
W. Bwana Yesu, zibariki familia zetu.
Yesu, Neno wa milele wa Baba, uliishi chini ya mamlaka ya Mama Maria na Mtakatifu Yosefu,
- utufundishe tuishi kwa unyenyekevu. (W.)
Mama Maria alikumbuka moyoni mwake yote uliyosema na kutenda:
- utuwezeshe kupenda fikara kama yeye. (W.)
Kristo, nguvu zako ndizo zilizoumba ulimwengu; hata hivyo, ulifika kujifunza kazi ya useremala.
- Utuwezeshe kuziona kazi zetu kuwa ni sehemu ya kazi yako. (W.)
Uliongezeka hekima, ukazidi kupendwa na Mungu na watu.
- Utuwezeshe kuishi kikamilifu ndani yako, na kuujenga mwili wako kwa imani na upendo. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:
Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu, Baba yetu, umetupatia Familia Takatifu ya Nazareti iwe mfano bora wa familia ya Kikristo.
Kwa kufuata mfano wa upendo wa maisha yao ya kifamilia, tujaliwe kufika nyumbani kwako kwenye
amani na furaha. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala
nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.