Generic placeholder image

SIKUKUU YA FAMILIYA TAKATIFU
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

TENZI angalia pia AU

AU
6
Ua lake Yuda, ua azizi,
Limechipuka kwenye mizizi,
Mizizi ambayo ni teketeke, Waridi la kwenye Shina la Yese,
Kama walivyoimba manabii:
Limechipuka kwenye mizizi,
Majira ya baridi hilo ua
Tafanya usiku upambazuke.

Waridi rembo na lenye neema,
Ambalo Isaya analiimba,
Ni wewe Mama Bikira Maria
Na Kristo ni ua unalochipua;
Kwa amri kamambe yake Mungu;
Maria ulimzaa Mwokozi
Ulimzaa Mpenzi wa sisi
Ambaye akafa atukomboe.

Maria wewe u mama mpenzi,
Sisi tunakuomba mama kwa dhati,
Twasihi kwa mioyo yetu yote:
Jalia huyo mwanao mchanga
Madhambi yetu atuondolee,
Kwa upendo wake atuongoze
Tuweze kwishi naye huko juu
Pia tumtumikie milele.
Karne ya 15

AU
7
Kutoka lichomozeako jua
Hadi lizamiako magharibi,
Kwa Kristo Mfalme heshima twatoa,
Alozaliwa leo na Bikira.

Mwumba Mtukufu ulijishusha
Uwe mtwana kwa ajili yetu,
Mwili hadhi ukaurudishia
Sisi viumbe tupate kuishi.

Tumbo la uzazi safi likaa
Lililojaa neema za mbingu;
Wala Bikira hakuweza sema
Mgeni wake katokea wapi.

Kutoka juu Mungu alikuja
Kuuhifadhi utukufu wake
Kifuani mwa asiye na dhambi,
Bikira aliyejaa utii.

Bikira imani alionesha
Kwa neno lililotoka kwa Mungu,
Na hapo ndipo akapata mimba
Bila kuwa na hatia yo yote.

Kishapo Mtoto akamzaa,
Alivyojulishwa na Gabrieli;
Huyo ndo Mtoto alotangazwa
Na mtangulizi kabla yake.

Alilala fofofo majanini
Ndani ya chombo cha kulishia ng'ombe;
Alinyonya maziwa ya mamake,
Yeye ambaye huwalisha wote.

Utukufu kwa Mungu! yasikika,
Hao malaika juu waimba;
Mchungaji, Bwana wa watu wote
Aabudiwa kwanza na wachunga.
Karne ya 5

AU
8
Kristo kwa ajili ya watu
Damu yako ndo ilitiririka,
Wewe u nuru iliyoangaza
Kabla haijawa asubuhi,
Wewe Bwana hakika ndiwe Mungu
Nawe milele ni Mwana wa Mungu,
Tena Wewe pamoja naye Baba
Nyie ni Mungu mmoja milele;

Ewe uliye mng'ao azizi
Utokanao na Nuru ya Baba,
U nyota iletayo tumaini
Ambayo daima yametameta,
Zisikilize basi twakuomba
Sala zenye kukumiminikia,
Kutoka huku chini duniani
Watumishi wako wanazosali.

Ee Bwana ukumbuke ya kuwa
Ni kwa sababu ya upendo wako
Wewe ulikiacha kule juu
Kile kiti chako cha enzi kuu
Chini ukaja upate kutwaa
Hali dhaifu ya kibinadamu,
Na ndipo mimba ukachukuliwa,
Na Mama aliye safi Bikira.

Kwa hiyo usikubali ardhi
Iwe peke yake yashangilia,
Bali hata bahari na uwingu
Pamoja vichange zao sauti,
Kusudi na uimbwe wimbo mpya
Wa kuishangilia asubuhi
Ile ya siku alipozaliwa
Yeye aliye Bwana wa uzima.

Ewe aliyekuzaa bikira
Ni wewe wa kuzipokea sifa,
Haya, hivi sasa tunakusifu,
Na milele uwe unasifiwa;
Baba naye pia apewe sifa
Kama hizo utolewazo Mwana,
Hizo pia na zimwendee Roho,
Ninyi msifiwe milele yote.

AU
9
Njooni, wamini wote,
Kwa furaha na kwa shangwe,
Njooni Betlehemu
Njooni mpate mwona
Mfalme alozaliwa,
Mfalme wa Malaika.

W. Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.

Ni Mungu sawa na Mungu,
Ni Nuru kutoka Nuru,
Lile tumbo la uzazi
La bikira hachukii;
Yeye ni Mungu halisi
Ana baba, hakuumbwa.

W. Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.

Imbeni, nyi malaika,
Imbeni kwa shangwe kuu,
Imbeni, wakazi wote
Wa huko mbinguni juu;.
'Utukufu kwako Mungu
Uliye mbinguni juu.'

W. Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.

Bwana tunakusalimu,
Uliyezaliwa leo
Asubuhi ya furaha,
Utukuzwe Bwana Yesu,
Neno wake Baba Mungu
Sasa u katika mwili.

W. Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Karne ya 18

AU
10
Tumempata sisi
Tumepewa mtoto,
Analeta uhuru
Kristo Mwokozi,
Yeye ni Mshauri
Ni Baba wa milele,
Mungu aliye mtu,
Mfalme wa Amani.

Mamake ni Maria
Bikira na mpole,
Hiyo kazi ya Roho,
Roho yule wa Bwana;
Huyo alitamkwa
Kale tangu milele:
Huyu ndiye ni Neno
Wake Baba Mwenyezi.

Ndaniye tachanua
Upendo na ukweli,
Navyo tatenda kazi
Kwa nguvu zake Neno.
Matawi yaso kitu
Maua yatapata;
Furaha ilolala
Yaanza kuamka.

Na apatiwe sifa
Baba alo milele,
Pia na Neno wake
Mwanae wa pekee,
Pamoja nao pia
Roho Mtakatifu
Ni Utatu kamili
Na ni Mungu mmoja.

AU
11
Alozawa na upendo wa Baba
Kabla ya ulimwengu kuumbwa,
Yeye ndiye Alfa na Omega,
Yeye ni chanzo, yeye ni kikomo
Cha vilivyo na vilivyokuwapo
Na vitavyoonekana badaye:
Kwa milele na milele.

Ilibarikiwa milele siku
Bikira - aliyejaa neema,
Mwenye mimba kwa uwezo wa Roho-
Alipomzaa Mwokozi wetu,
Naye Mkombozi wa ulimwengu
Alipoonesha kwanza usowe:
Kwa milele na milele.

Atukuzwe Mungu Baba Mwenyezi,
Atukuzwe Mungu Mwana Mwokozi,
Atukuzwe Roho Mtakatifu,
Umungu mmoja, Nafsi tatu.
Viumbe vyote na vimtukuze
Mwenyezi Mungu kwa nyakati zote:
Kwa milele na milele.
Aurelio C. Prudensio
348-yapata 413

AU
12
Kristo huyu hapa,
Mwenyewe Emanueli,
Yeye ndiye mtukufu
Na ni mpole ajabu:
Hekima nayo neema,
Hekima nao ukweli
Vipo ila mefichama
Katika huyu Mtoto.

Vile Mungu alitaka
Yesu ndipo kaumbika,
Kristo ndiye Mwanga
Aliyetoka kwa Mwanga,
Amekuja waokoa
Waana wake Adamu
Ambao wanangojea
Katika giza - usiku.

Sifa kwa Baba na Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Utukufu wao hao
Wa mbinguni wanaimba,
Na walio duniani
Kwa sauti ilo kuu
Sawia wanausifu
Utatu wauabudu.
Stanbrook Abbey Hymnal

ANT. I: Yakobo alikuwa baba ya Yosefu, mume wa Maria; Maria alikuwa mama ya Yesu aitwaye Kristo.

Zab.113 Sifa kwa Mungu mtukufu
Enyi watumishi wa Mungu,*
lisifuni jina lake!

Jina lake litukuzwe,*
sasa na hata milele.

Kutoka mashariki hata magharibi,*
litukuzwe jina la Mungu!

Mungu atawala mataifa yote,*
utukufu wake wazipita mbingu.

Hakuna aliye sawa na Mungu, Mungu wetu,*
ambaye anakaa juu kabisa;

lakini huinama chini*
kuzitazama mbingu na nchi.

Humwinua fukara kutoka mavumbini;*
humnyanyua maskini kutoka unyonge wake,

na kumweka pamoja na wakuu;*
naam, pamoja na wakuu wa watu wake.

Humrudishia hadhi mwanamke aliye tasa;*
na kumfurahisha kwa kumjalia watoto.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Yakobo alikuwa baba ya Yosefu, mume wa Maria; Maria alikuwa mama ya Yesu aitwaye Kristo.

ANT. II: Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria kuwa mkeo. Amepata mimba hiyo kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Zab.147:12-20 Ni vizuri kumsifu Mungu
Ee Yerusalemu, umsifu Mungu!*
Umsifu Mungu wako, ee Sion!

Maana ameiimarisha milango yako,*
amewabariki watu waliomo kwako.

Ameweka amani mipakani mwako;*
anakushibisha kwa ngano safi kabisa.

Yeye hupeleka amri yake duniani,*
na neno lake hutekelezwa upesi.

Hutandaza theluji kama pamba,*
hutawanya umande kama majivu.

Huleta mvua ya mawe/
vipande vikubwa vikubwa kama mkate*
na kwa ubaridi wake maji huganda.

Kisha hutoa amri, na maji hayo huyeyuka;*
huvumisha upepo wake, nayo hutiririka.

Humjulisha Yakobo ujumbe wake,*
na Israeli amri na maagizo yake.

Lakini watu wengine hakuwafanyia hayo;*
watu wengine hawayajui maagizo yake.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria kuwa mkeo. Amepata mimba hiyo kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

ANT. III: Wachungaji wakaenda kwa haraka, wakawakuta Maria na Yosefu, na yule mtoto mchanga amelala horini.

WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!

Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.

Kabla ya kuumbwa ulimwengu,/
Mungu alituteua tuwe wake*
katika kuungana na Kristo

ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.

Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani

kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.

Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu

kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!

Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!

Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,

akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.

Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,

ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Wachungaji wakaenda kwa haraka, wakawakuta Maria na Yosefu, na yule mtoto mchanga amelala horini.

SOMO: 2Kor.8:9
Ninyi mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo: yeye, ingawa alikuwa na kila kitu, alijifanya maskini kwa ajili yenu, ili kutokana na umaskini wake awatajirishe.

KIITIKIZANO
K. Neno akatwaa mwili, akakaa kwetu. (W. Warudie)
K. Kutoka utimilifu wake sisi sote tumepokea neema.
W. Akakaa kwetu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Neno akatwaa...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Mtoto Yesu alibaki nyuma, huko Yerusalemu, na wazazi wake hawakuwa na habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara, wakawa wakimtafuta kati ya jamaa zao na marafiki.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mtoto Yesu alibaki nyuma, huko Yerusalemu, na wazazi wake hawakuwa na habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara, wakawa wakimtafuta kati ya jamaa zao na marafiki.

MAOMBI
Tumwabudu Mwana wa Mungu Aliye Hai, aliyepata kuwa mwana katika familia ya kibinadamu.
W. Bwana Yesu, zibariki familia zetu.

Kwa utii wako kwa Mama Maria na Mtakatifu Yosefu,
- utufundishe jinsi ya kuwaheshimu viongozi, na jinsi ya kushika taratibu. (W.)

Kwa mapendo yaliyotawala nyumba yako,
- uzijalie familia zetu neema ya kupenda uelewano na amani. (W.)

Kusudi lako la kwanza lilikuwa kumheshimu Baba yako.
- Mungu na awe kiini cha maisha ya familia zetu. (W.)

Wazazi wako walikukuta ukifundisha katika nyumba ya Baba yako.
- Utusaidie tufanane nawe katika kutimiza kwanza matakwa ya Baba. (W.)

Kwa kuungana tena na Mama Maria na Yosefu katika furaha ya mbinguni,
- uwakaribishe ndugu zetu marehemu katika familia ya watakatifu. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu, Baba yetu, umetupatia Familia Takatifu ya Nazareti iwe mfano bora wa familia ya Kikristo. Kwa kufuata mfano wa upendo kati ya Yesu, Maria na Yosefu, na mfano wa maisha yao ya kifamilia, tujaliwe kufika nyumbani kwako kwenye amani na furaha. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.