SIKUKUU YA FAMILIYA TAKATIFU
MASIFU YA JIONI II
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
TENZI angalia pia AU
AU
6
Ua lake Yuda, ua azizi,
Limechipuka kwenye mizizi,
Mizizi ambayo ni teketeke,
Waridi la kwenye Shina la Yese,
Kama walivyoimba manabii:
Limechipuka kwenye mizizi,
Majira ya baridi hilo ua
Tafanya usiku upambazuke.
Waridi rembo na lenye neema,
Ambalo Isaya analiimba,
Ni wewe Mama Bikira Maria
Na Kristo ni ua unalochipua;
Kwa amri kamambe yake Mungu;
Maria ulimzaa Mwokozi
Ulimzaa Mpenzi wa sisi
Ambaye akafa atukomboe.
Maria wewe u mama mpenzi,
Sisi tunakuomba mama kwa dhati,
Twasihi kwa mioyo yetu yote:
Jalia huyo mwanao mchanga
Madhambi yetu atuondolee,
Kwa upendo wake atuongoze
Tuweze kwishi naye huko juu
Pia tumtumikie milele.
Karne ya 15
AU
7
Kutoka lichomozeako jua
Hadi lizamiako magharibi,
Kwa Kristo Mfalme heshima twatoa,
Alozaliwa leo na Bikira.
Mwumba Mtukufu ulijishusha
Uwe mtwana kwa ajili yetu,
Mwili hadhi ukaurudishia
Sisi viumbe tupate kuishi.
Tumbo la uzazi safi likaa
Lililojaa neema za mbingu;
Wala Bikira hakuweza sema
Mgeni wake katokea wapi.
Kutoka juu Mungu alikuja
Kuuhifadhi utukufu wake
Kifuani mwa asiye na dhambi,
Bikira aliyejaa utii.
Bikira imani alionesha
Kwa neno lililotoka kwa Mungu,
Na hapo ndipo akapata mimba
Bila kuwa na hatia yo yote.
Kishapo Mtoto akamzaa,
Alivyojulishwa na Gabrieli;
Huyo ndo Mtoto alotangazwa
Na mtangulizi kabla yake.
Alilala fofofo majanini
Ndani ya chombo cha kulishia ng'ombe;
Alinyonya maziwa ya mamake,
Yeye ambaye huwalisha wote.
Utukufu kwa Mungu! yasikika,
Hao malaika juu waimba;
Mchungaji, Bwana wa watu wote
Aabudiwa kwanza na wachunga.
Karne ya 5
AU
8
Kristo kwa ajili ya watu
Damu yako ndo ilitiririka,
Wewe u nuru iliyoangaza
Kabla haijawa asubuhi,
Wewe Bwana hakika ndiwe Mungu
Nawe milele ni Mwana wa Mungu,
Tena Wewe pamoja naye Baba
Nyie ni Mungu mmoja milele;
Ewe uliye mng'ao azizi
Utokanao na Nuru ya Baba,
U nyota iletayo tumaini
Ambayo daima yametameta,
Zisikilize basi twakuomba
Sala zenye kukumiminikia,
Kutoka huku chini duniani
Watumishi wako wanazosali.
Ee Bwana ukumbuke ya kuwa
Ni kwa sababu ya upendo wako
Wewe ulikiacha kule juu
Kile kiti chako cha enzi kuu
Chini ukaja upate kutwaa
Hali dhaifu ya kibinadamu,
Na ndipo mimba ukachukuliwa,
Na Mama aliye safi Bikira.
Kwa hiyo usikubali ardhi
Iwe peke yake yashangilia,
Bali hata bahari na uwingu
Pamoja vichange zao sauti,
Kusudi na uimbwe wimbo mpya
Wa kuishangilia asubuhi
Ile ya siku alipozaliwa
Yeye aliye Bwana wa uzima.
Ewe aliyekuzaa bikira
Ni wewe wa kuzipokea sifa,
Haya, hivi sasa tunakusifu,
Na milele uwe unasifiwa;
Baba naye pia apewe sifa
Kama hizo utolewazo Mwana,
Hizo pia na zimwendee Roho,
Ninyi msifiwe milele yote.
AU
9
Njooni, wamini wote,
Kwa furaha na kwa shangwe,
Njooni Betlehemu
Njooni mpate mwona
Mfalme alozaliwa,
Mfalme wa Malaika.
W.
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Ni Mungu sawa na Mungu,
Ni Nuru kutoka Nuru,
Lile tumbo la uzazi
La bikira hachukii;
Yeye ni Mungu halisi
Ana baba, hakuumbwa.
W.
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Imbeni, nyi malaika,
Imbeni kwa shangwe kuu,
Imbeni, wakazi wote
Wa huko mbinguni juu;.
'Utukufu kwako Mungu
Uliye mbinguni juu.'
W.
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Bwana tunakusalimu,
Uliyezaliwa leo
Asubuhi ya furaha,
Utukuzwe Bwana Yesu,
Neno wake Baba Mungu
Sasa u katika mwili.
W.
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Njooni, na tumwabudu,
Kristo Bwana wetu.
Karne ya 18
AU
10
Tumempata sisi
Tumepewa mtoto,
Analeta uhuru
Kristo Mwokozi,
Yeye ni Mshauri
Ni Baba wa milele,
Mungu aliye mtu,
Mfalme wa Amani.
Mamake ni Maria
Bikira na mpole,
Hiyo kazi ya Roho,
Roho yule wa Bwana;
Huyo alitamkwa
Kale tangu milele:
Huyu ndiye ni Neno
Wake Baba Mwenyezi.
Ndaniye tachanua
Upendo na ukweli,
Navyo tatenda kazi
Kwa nguvu zake Neno.
Matawi yaso kitu
Maua yatapata;
Furaha ilolala
Yaanza kuamka.
Na apatiwe sifa
Baba alo milele,
Pia na Neno wake
Mwanae wa pekee,
Pamoja nao pia
Roho Mtakatifu
Ni Utatu kamili
Na ni Mungu mmoja.
AU
11
Alozawa na upendo wa Baba
Kabla ya ulimwengu kuumbwa,
Yeye ndiye Alfa na Omega,
Yeye ni chanzo, yeye ni kikomo
Cha vilivyo na vilivyokuwapo
Na vitavyoonekana badaye:
Kwa milele na milele.
Ilibarikiwa milele siku
Bikira - aliyejaa neema,
Mwenye mimba kwa uwezo wa Roho-
Alipomzaa Mwokozi wetu,
Naye Mkombozi wa ulimwengu
Alipoonesha kwanza usowe:
Kwa milele na milele.
Atukuzwe Mungu Baba Mwenyezi,
Atukuzwe Mungu Mwana Mwokozi,
Atukuzwe Roho Mtakatifu,
Umungu mmoja, Nafsi tatu.
Viumbe vyote na vimtukuze
Mwenyezi Mungu kwa nyakati zote:
Kwa milele na milele.
Aurelio C. Prudensio
348-yapata 413
AU
12
Kristo huyu hapa,
Mwenyewe Emanueli,
Yeye ndiye mtukufu
Na ni mpole ajabu:
Hekima nayo neema,
Hekima nao ukweli
Vipo ila mefichama
Katika huyu Mtoto.
Vile Mungu alitaka
Yesu ndipo kaumbika,
Kristo ndiye Mwanga
Aliyetoka kwa Mwanga,
Amekuja waokoa
Waana wake Adamu
Ambao wanangojea
Katika giza - usiku.
Sifa kwa Baba na Mwana
Na Roho Mtakatifu,
Utukufu wao hao
Wa mbinguni wanaimba,
Na walio duniani
Kwa sauti ilo kuu
Sawia wanausifu
Utatu wauabudu.
Stanbrook Abbey Hymnal
ANT. I: Baada ya siku tatu wakamwona Yesu hekaluni, ameketi kati ya
walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.
Zab.122 Sifa za Yerusalemu
Nilifurahi waliponiambia:*
"Twende nyumbani kwa Mungu.“
Sasa sisi tumekwisha wasili,*
tumesimama milangoni mwa Yerusalemu!
Yerusalemu, mji uliorekebishwa,*
kwa mpango mzuri na umetengemaa!
Humo ndimo makabila yanafika,/.
naam, makabila ya Israeli,*
kumshukuru Mungu kama alivyoagiza.
Humo mna mahakama ya haki,*
mahakama ya kifalme ya Daudi.
Uombeeni Yerusalemu amani;*
“Wote wakupendao wafanikiwe!
Ukumbini mwako kuwe na amani,*
majumbani mwako kuweko usalama!“
Kwa ajili ya jamaa na ndugu zangu,*
Ee Yerusalemu, nakutakia amani!
Kwa ajili ya nyumba ya Mungu, Mungu wetu,*
ninakuombea upate fanaka!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Baada ya siku tatu wakamwona Yesu hekaluni, ameketi kati ya
walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.
ANT. II: Yesu akarudi pamoja nao Nazareti, akawa anawatii.
Zab.127 Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
Mungu asipoijenga nyumba,*
waijengao wanajisumbua bure.
Mungu asipoulinda mji,*
waulindao wanakesha bure.
Mnaamka mapema asubuhi na kuchelewa kulala usiku,/
mkihangaika na kutoka jasho kupata chakula chenu.*
Kwa nini mnajihangaisha hivyo?
Kama mnampenda Mungu*
atawajalieni yote mngali usingizini!
Watoto ni zawadi itokayo kwa Mungu;*
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.
Watoto unaowapata ukiwa kijana,*
ni kama mishale mikononi mwa askari.
Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.*
Hatashindwa akutanapo na adui mahakamani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Yesu akarudi pamoja nao Nazareti, akawa anawatii.
ANT. III: Yesu alivyozidi kukua, aliongezeka hekima, akazidi
kupendwa na Mungu na watu.
WIMBO: Ef.1:3-10
Atukuzwe Mungu na Baba*
ya Bwana wetu Yesu Kristo!
Maana katika kuungana na Kristo/
ametubariki kwa kutujalia*
zawadi zote za kiroho mbinguni.
Kabla ya kuumbwa ulimwengu,/
Mungu alituteua tuwe wake*
katika kuungana na Kristo
ili tuwe watakatifu*
na bila hitilafu mbele yake.
Kwa sababu ya upendo wake,*
Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani
kutuleta kwake kama watoto wake*
kwa njia ya Yesu Kristo.
Ndivyo alivyopenda na kunuia.*
Basi, tumsifu Mungu
kwa sababu ya neema yake tukufu*
katika Mwanae mpenzi!
Maana kwa damu yake Kristo/
sisi tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.
Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake*
aliyotukirimia bila kipimo!
Kwa hekima na ujuzi wake wote*
Mungu alitekeleza kile alichonuia,
akatujulisha mpango wake uliofichika,/
ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza*
kwa njia ya Kristo.
Mpango huo*
ambao angeutimiza wakati utimiapo,
ni kukusanya pamoja viumbe vyote,/
kila kitu mbinguni na duniani,*
chini ya Kristo.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Yesu alivyozidi kukua, aliongezeka hekima, akazidi
kupendwa na Mungu na watu.
SOMO: Flp.2:6-7
Kristo Yesu, kwa asili alikuwa daima Mungu; lakini hakufikiri kwamba kule kuwa sawa na Mungu
ni kitu cha kung'ang'ania kwa nguvu. Bali, kwa hiari yake mwenyewe, aliachilia hayo yote,
akajitwalia hali ya mtumishi, akawa sawa na wanadamu, akaonekana kama wanadamu.
KIITIKIZANO
K. Ilipasa alingane na ndugu zake kwa kila hali, ili aweze kuwa mwenye huruma. (W. Warudie)
K. Alikuja duniani, akaishi kati ya watu.
W. Ili aweze kuwa mwenye huruma.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Ilipasa alingane...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
'Mwanangu, kwa nini umetutendea hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa mahangaiko.
'Yeye akawajibu: 'Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua ya kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?'
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. 'Mwanangu, kwa nini umetutendea hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa
tukikutafuta kwa mahangaiko. 'Yeye akawajibu: 'Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua ya kwamba inanipasa
kuwa katika nyumba ya Baba yangu?'
MAOMBI
Tumwabudu Mwana wa Mungu Aliye Hai, aliyepata kuwa mwana katika familia ya kibinadamu.
W. Bwana Yesu, zibariki familia zetu.
Kwa utii wako kwa Mama Maria na Mtakatifu Yosefu,
- utufundishe jinsi ya kuwaheshimu viongozi, na jinsi ya kushika taratibu. (W.)
Kwa mapendo yaliyotawala nyumba yako,
- uzijalie familia zetu neema ya kupenda uelewano na amani. (W.)
Kusudi lako la kwanza lilikuwa kumheshimu Baba yako.
- Mungu na awe kiini cha maisha ya familia zetu. (W.)
Wazazi wako walikukuta ukifundisha katika nyumba ya Baba yako.
- Utusaidie tufanane nawe katika kutimiza kwanza matakwa ya Baba. (W.)
Kwa kuungana tena na Mama Maria na Yosefu katika furaha ya mbinguni,
- uwakaribishe ndugu zetu marehemu katika familia ya watakatifu. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu, Baba yetu, umetupatia Familia Takatifu ya Nazareti iwe mfano bora wa familia ya Kikristo.
Kwa kufuata mfano wa upendo kati ya Yesu, Maria na Yosefu, na mfano wa maisha yao ya kifamilia,
tujaliwe kufika nyumbani kwako kwenye amani na furaha. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu
Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.