SIKUKUU YA FAMILIYA TAKATIFU
JUMAPILI KATIKA OKTAVA YA NOEL
Familiya ya YESU, MARIA na YOSEFU

ANTIFONA YA KUINGIA: LK2:16
Wachungaji wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yosefu, na yule mtoto mchanga amelala horini.

Utukufu husemwa

KOLEKTA:
Ee Mungu, umependa kutuonesha mifano bora ya Familia takatifu. Utujalie kwa wema ili kwa kuiga mifano yake ya fadhila za nyumbani na vifungo vya mapendo, tuweze kufaidi tuzo za milele katika furaha ya nyumba yako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Ybs.3:2-6,12-14
Bwana amempa baba utukufu mintarafu wana, na kuithibitisha haki ya mama mintarafu watoto. Anayemheshimu baba yake atafanya malipizi ya dhambi, naye anayemtukuza mama yake huweka akiba iliyo azizi. Anayemheshimu babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa. Anayemtukuza baba yake ataongezewa siku zake; akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye. Mwanangu, umsaidie baba yako katika uzee wake; wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake. Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana; kwa maana sadaka apewayo baba haitasahauliwa, na badala ya dhambi itahesabiwa kwa kukuthibitisha.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.128:1-5(K)1
1. Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika njia zake
Taabu ya mikono yako hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema.

(K) Heri kila mtu amchaye Bwana,
aendaye katika njia zake.

2. Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni
Wakiizunguka meza yako. (K)

3. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana,
Bwana akakubariki toka Sayuni.
Uone uheri wa Yerusalemu.
Siku zote za maisha yako. (K)

SOMO 2: Kol3:12-21
Ndugu zangu, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani katika hekima yote, mkifundishana na yenu kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye. Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao. Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana. Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

SHANGILIO: Kol.3:15,16
Aleluya, aleluya!
Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu;
Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu.
Aleluya!

Nenda Injili na maombi mwaka B
Nenda Injili na maombi mwaka C

INJILI NA MAOMBI MWAKA A
INJILI: Mt.2:13-15,19-23
Mamajusi walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa Nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu. Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli. Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya, akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazarayo.

Ikiwa sikukuu hii inaadhimishwa siku ya Dominika, Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu zangu, tumwombe sasa Mungu katika shida zetu, tukikumbuka hasa familia zetu. Ee Bwana Yesu Kristo, Kanisa lako lote ni familia kubwa ya watoto wa Mungu.
Tuitikie: Linda familia zetu, Ee Bwana!

1. Uwasaidie viongozi wa Kanisa letu yaani Baba Mt. J.., Maaskofu, Mapadre na wote wenye madaraka katika Kanisa kulitunza na kuliongoza Kanisa lako kwa busara.

2. Uwahimize viongozi wetu watengeneze sera na mipango inayofaa kwa ajili ya kuinua na kusitawisha familia zetu.

3. Uzisaidie familia zote zenye shida katika bidii yao ya kutatua matatizo yao.

4. Uwakumbushe wazazi wajibu wa kuwalea watoto wao katika misingi na maadili mema.

5. Uwaongoze vijana wetu kujitayarisha vema kwa maisha ya familia.

Ee Mungu, uyapokee maombi yetu na uyasikilize. Tunaomba hayo kwa jina la Kristo, Bwana wetu. Amina.

------------------------

INJILI NA MAOMBI MWAKA B
INJILI: Somo refu Lk.2:22-40
Zilipotimia siku za kutakasika kwao kama ilivyo torati ya Musa, walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Palikuwa na Nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ileile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyo agizwa katika sheria ya Bwana walirejea Galilaya, mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

INJILI: Somo fupi Lk.2:22,39-40
Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa, walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya, mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

Ikiwa sikukuu hii inaadhimishwa siku ya Dominika, Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu wapendwa, tumwabudu Mwana wa Mungu aliyekubali kuwa Mwana-familia wa kibinadamu. Tumwombe tukisema: Ubariki familia zetu, Ee Bwana! Ee Mtoto Yesu, uliyewatii wanadamu, baba yako mlishi Yosef na mama yako Bikira Maria: Tunakuomba:

1. Uwakumbushe watoto wote kwamba deni lao kwa wazazi na walezi wao ni heshima kamili.

2. Uwape wazazi na walezi bidii ya kuhakikisha kuwa watoto wao wanalelewa katika misingi ya maadili bora.

3. Uzibariki kazi za walimu na uwatie moyo ili wafanye kazi zao kwa bidii na busara.

4. Uwasaidie watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu kupata mahitaji yao ya lazima.

5. Utengeneze hali nzuri ya maisha ya watoto wasitoroke nyumbani na kujiunga na vikundi visivyofaa.

Ee Mungu Baba, ulikubali Mwana wako Yesu Kristo aishi katika familia ili kujifunza njia zetu za hapa duniani. Uyapokee maombi yetu kwa njia ya huyu Mwana wako anayetufahamu kabisa. Amina.

------------------------

INJILI NA MAOMBI MWAKA C
INJILI: Lk.2:41-52
Wazee wake Yesu huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake wa miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.

Ikiwa sikukuu hii inaadhimishwa siku ya Dominika, Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu zangu, tumwombe Mwana wa Maria atufundishe kuwatii na kuwajali wakubwa wetu. Tumwombe,

1. Utusaidie kuwaheshimu na kuwatunza wazazi wetu.

2. Uwatie Watoto moyo wa kuwasaidia na kuwatunza wazazi na walezi wao.

3. Uamshe moyo wa mapendo kwa wanafamilia ili kuhudumiana na kuvumiliana katika matatizo yao.

4. Uzisaidie na kuziunganisha familia zilizotengana kwa sababu ya magomvi na fitina.

5. Uwapokee marehemu wanafamilia, walimu na walezi wetu katika uzima wa milele.

Ee Mungu, Mwanao alipoishi miaka thelathini katika familia, alionja taabu za familia. Malezi ni kazi nzito. Uwape baraka zako wanafamilia ili waweze kuungana na kufanya kazi kwa pamoja. Tunakuomba kwa njia ya Mwanao, Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakutolea sadaka ya upatanisho, tukikuomba kwa unyenyekevu, uzithibitishe kabisa familia zetu katika neema na amani yako kwa maombezi ya Bikira Mama wa Mungu na Yosefu mwenye heri. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI wa Kuzaliwa kwa Bwana, I, II au III.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Bar.3:38
Mungu wetu ameonekana duniani, akakaa na watu.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Baba mwenye huruma, unayetulisha sakramenti za mbinguni, utuwezeshe kuiga daima mifano ya Familia takatifu, ili baada ya taabu za hapa duniani, tuunganike nayo katika ushirika wa milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.