SIKUKUU YA FAMILIYA TAKATIFU
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ee fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Yosefu na Maria, mama wa Yesu, waliyastaajabia yaliyokuwa
yanasemwa juu yake.
Adhuhuri
Ant.: Maria aliyaweka hayo yote, akayatafakari moyoni mwake.
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Macho yangu yameuona wokovu uliouandaa machoni pa watu wote.
Zab.118 Sala ya shukrani
Huyu ndiye lile jiwe mlilokataa ninyi waashi, ambalo sasa limekuwa jiwe kuu la msingi
(mate.4:11)
I
Mshukuruni Mungu, kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.
Watu wa Israeli waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."
Wazao wa Aroni waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."
Wote wamchao Mungu waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."
Katika taabu yangu nilimlilia Mungu,*
naye akanisikiliza na kuniokoa.
Mungu yuko nami, siogopi kitu;*
mwanadamu atanifanya nini?
Mungu yuko nami, ananisaidia;*
nami nitashuhudia kushindwa kwa adui zangu.
Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kumtegemea mwanadamu.
Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kuwategemea viongozi wa dunia.
Watu wote wasiomjua Mungu walinizingira,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II
Walinizunguka kila upande,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.
Walinivamia kwa wingi kama nyuki,/
lakini wakateketea kama kichaka motoni;*
kwangu nguvu ya Mungu nikawapondaponda.
Nilishambuliwa mno karibu nishindwe,*
lakini Mungu alinisaidia.
Mungu hunijalia nguvu na uhodari;*
yeye mwenyewe ameniokoa.
Sikilizeni sauti za furaha na ushindi/
katika mahema ya watu waadilifu;*
"Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!
Mkono wa Mungu umeleta ushindi!*
Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!"
Sitakufa, bali nitaishi,*
na kutangaza matendo ya Mungu.
Mungu ameniadhibu sana,*
lakini hakuniacha nife.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
III
Nifungulie milango ya Hekalu;*
nitaingia na kumshukuru Mungu!
Huu ndio mlango wa Mungu,*
ambao waadilifu waweza kupitia.
Nakushukuru, Ee Mungu, kwa kunisikiliza;*
kwa sababu wewe umeniokoa.
Jiwe walilolikataa waashi,*
limekuwa jiwe kuu la msingi.
Jambo hili limefanywa na Mungu;*
nalo ni jambo la ajabu mno kwetu.
Hii ndiyo siku aliyoifanya Mungu;*
basi, tushangilie na kufurahi.
Utuokoe, Ee Mungu, utuokoe!*
Ee Mungu, tunakusihi, utupe fanaka!
Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mungu!*
Twakubariki toka nyumbani mwa Mungu.
Mungu ni Mungu, naye ni mwema kwetu./
Shikeni matawi mikononi, anzeni sherehe,*
mkiandamana mpaka madhabahuni.
Ndiwe, Mungu wangu, ninakushukuru*
ninakutukuza, Ee Mungu wangu.
Mshukuruni Mungu kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Kabla ya Adhuhuri
Ant.: Yosefu na Maria, mama wa Yesu, waliyastaajabia yaliyokuwa
yanasemwa juu yake.
Adhuhuri
Ant.: Maria aliyaweka hayo yote, akayatafakari moyoni mwake.
Baada ya Adhuhuri
Ant.: Macho yangu yameuona wokovu uliouandaa machoni pa watu wote.
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Kol.3:12-13
Ninyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo, basi, vaeni moyo wa huruma,
wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo
lo lote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe ninyi.
K. Bwana atufundisha njia zake.
W. Tutatembea katika mapito yake.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Kol.3:14-15
Zaidi ya hayo yote, zingatieni upendo, kwani upendo huunganisha kila kitu katika umoja ulio
kamili. Nayo amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu; maana kwa ajili hiyo ninyi mmeitwa katika
mwili huo mmoja. Tena muwe na shukrani!
K. Tangu ujana wangu, dhiki na huzuni vimeniandama.
W. Nimeinuliwa ili nitupwe chini, na kuachwa mwenye fadhaa.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Kol.3:17
Kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa jina la Bwana Yesu na kumshukuru Mungu
Baba kwa njia yake.
K. Bwana atawapa mwongozo wanao wote.
W. Atawajalia watoto wako wote amani maridhawa.
SALA:
Tuombe: Mungu, Baba yetu, umetupatia Familia Takatifu ya Nazareti iwe mfano bora wa familia
ya Kikristo. Kwa kufuata mfano wa upendo wa maisha yao ya kifamilia, tujaliwe kufika nyumbani
kwako kwenye amani na furaha. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.