IJUMAA JUMA 12 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: 2Fal.25:1-12
Ikawa katika mwaka wa kenda wa kutawala kwake, katika mwezi wa kumi, na siku ya kumi ya mwezi huo, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaja, yeye na jeshi lake lote, kupigana na Yerusalemu, akapanga hema zake kuukabili; nao wakajenga ngome juu yake pande zote. Basi mji huo ulihusuriwa hata mwaka wa kumi na moja wa mfalme Sedekia. Siku ya kenda ya mwezi wa nne njaa ilikuwa nzito ndani ya mji, hata hapakuwa na chakula kwa watu wa nchi. Ndipo mahali pakabomolewa katika ukuta wa mji, watu wote wa vita wakakimbia usiku kwa njia ya lango lililokuwa kati ya zile kuta mbili, karibu na bustani ya mfalme; (basi wale Wakaldayo walikuwa wakiuzuia mji pande zote;) mfalme akaenda kwa njia ya Araba. Lakini jeshi la Wakaldayo wakamfuatia mfalme, wakampata katika nchi tambarare ya Yeriko; na jeshi lake lote walikuwa wametawanyika na kumwacha. Ndipo wakamkamata mfalme, wakamchukua kwa mfalme wa Babeli huko Ribla; wakatoa hukumu juu yake. Wakawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake, wakampofusha macho Sedekia, wakamfunga kwa pingu, wakamchukua mpaka Babeli. Hata mwezi wa tano, siku ya saba ya mwezi, ndio mwaka wa kumi na kenda wa mfalme Nebukadreza, mfalme wa Babeli, Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, mtumishi wa mfalme wa Babeli, akaingia Yerusalemu. Akaiteketeza nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme; na nyumba zote za Yerusalemu, naam, kila nyumba kubwa aliiteketeza kwa moto. Na jeshi lote la Wakaldayo, waliokuwa pamoja na huyo amiri wa askari walinzi, wakazibomoa kuta za Yerusalemu pande zote. Na mabaki ya watu waliosalia katika mji, nao wale walioasi, na kumkimbilia mfalme wa Babeli, na mabaki ya watu wote wengine, watu hao Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua mateka. Lakini huyo amiri wa askari walinzi akawaacha watu walio maskini ili wawe watunza mizabibu na wakulima.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.137:1-6(K)6
1. Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi,
Tukalia tulipoikumbuka Sayuni.
Katika miti iliyo katikati yake
Tulivitundika vinubi vyetu.

(K) Ulimi wangu ugandamane nisipokukumbuka.

2. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie;
Na waliotuonea walitaka furaha;
Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.(K)

3. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?
Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe,
Mkono wangu wa kuume na usahau.(K)

4. Ulimi wangu na ugandamane
Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.
Nisipoikuza Yerusalemu Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu. (K)

SHANGILIO: Mt.8:17
Aleluya, aleluya!
Kristo mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu.
Aleluya!

INJILI: Mt.8:1-4
Yesu aliposhuka mlimani, makutano mengi walimfuata. Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika. Yesu akamwambia, Angalia, usimwambie mtu; ila enenda zako, ukajioneshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, iwe ushuhuda kwao.