Generic placeholder image

IJUMAA JUMA LA 13 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Mungu alipomwumba mtu,
Alimpa dunia yote,
Alimpa yote mimea,
Kila ndege kila mnyama;
Na kwa amri yake Bwana
Adamu livipa majina,
Na vyote akavitiisha,
Vidogo na vikubwa pia.

Mungu alimuumba mtu
Kwa mfano na sura yake,
Na alipoufanya uso
Wa mtu tokana udongo
Hapo sura ikatokea
Ya Mwana wake wa pekee:
Neno wake mwenye muili
Kajaa neema na kweli.

Mbingu na dunia pamoja
Sifa zitoe kwake Baba,
Na kwa Mwanae Kristo,
Na kwa Mtakatifu Roho.
Viumbe vyote kwa sauti,
Kwa sauti kubwa vyasema:
Ni Mtakatifu kabisa
Bwana Mwenyezi wa daima.

ANT. I: Ee Bwana, uiponye roho yangu, kwani nimekukosea.

Zab.41 Sala ya mgonjwa
Mmoja wenu, anayekula pamoja nami, atanisaliti (Mk.14:18)

Heri mtu anayewashughulikia maskini,*
Mungu atamsaidia wakati wa shida.

Mungu atamlinda na kumweka hai;/
atamfanikisha katika nchi;*
hatamwacha katika makucha ya adui zake.

Mungu atamsaidia awapo mgonjwa;*
na kumpatia nafuu ya maradhi yake.

Nami nilisema: "Nimekukosea wewe, Ee Mungu,*
unihurumie ukaniponye."

Adui zangu husema mabaya juu yangu;*
wanataka nife na kusahauliwa kabisa.

Wanitembeleapo huwa hawana nia njema;/
wanawaza mabaya juu yangu,*
wafikapo nje huwatangazia wengine.

Wote wanichukiao hunong'onezana juu yangu;*
waniwazia mabaya ya kunidhuru.

Husema: “Maradhi haya yatamwua;*
hatatoka tena kitandani mwake!“

Hata rafiki yangu mkuu ambaye nilimtegemea,/
ambaye alishiriki chakula changu,*
amegeuka na kuanza kunishambulia!

Ee Mungu, unionee huruma!*
Unipe nafuu, nami nitawalipiza.

Hivyo nitajua kwamba umenifadhili,*
ikiwa adui zangu hawatanishinda.

Utanitegemeza, kwani natenda yaliyo sawa;*
utaniweka mbele yako milele.

Asifiwe Mungu, Mungu wa Israeli!*
Asifiwe sasa na milele!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, uiponye roho yangu, kwani nimekukosea.

ANT. II: Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

Zab.46 Mungu yuko upande wetu
Naye ataitwa Emanueli (maana yake, "Mungu yuро рamoја nasi") (Mt.1:23)

Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu;*
yu tayari daima kusaidia wakati wa taabu.

Kwa hiyo hatutaogopa chochote,*
dunia ijapoyeyuka na milima kuanguka baharini;

hata kama bahari ikichafuka na kutisha,*
na vilima vikatikiswa kwa shambulio lake.

Kuna mto ambao maji yake yaufurahisha mji wa Mungu,*
makao matakatifu ya Mungu Mkuu.

Mungu yumo mjini humo, nao hauwezi kutikiswa;*
alfajiri na mapema huuletea msaada.

Mungu anguruma, dunia yayeyuka;*
mataifa yaghadhabika na tawala zatikisika.

Mwenyezi mwenye nguvu, yu pamoja nasi,*
Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.

Njoni mkaone matendo makuu ya Mungu;*
oneni maajabu aliyoyafanya duniani.

Hukomesha vita popote duniani,/
huvunjavunja pinde na mikuki,*
nayo magari ya vita huyateketeza.

Asema: “Nyamazeni!*
jueni kwamba mimi ndimi Mungu!

Mimi natukuzwa na mataifa yote;*
mimi ni mkuu wa ulimwengu wote!"

Mungu, Mungu mwenye nguvu, yu upande wetu,*
Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

ANT. III: Mataifa yote yatakuja kukuabudu, Ee Bwana.

WIMBO: Ufu.15:3-4. Utenzi wa sifa
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!

Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!

Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako? *
Wewe peke yako ni Mtakatifu.

Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina.

Ant. III: Mataifa yote yatakuja kukuabudu, Ee Bwana.

SOMO: Rom.15:1-3
Sisi tulio imara katika imani, tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza mwenzake kwa wema, ili huyo apate kujijenga katika imani. Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: “Kashifa zote walizokutolea wewe, zimenipata mimi.“

KIITIKIZANO
K. Kristo alitupenda, na ametuondolea dhambi zetu kwa damu yake. (W. Warudie)
K. Ametushirikisha ufalme na ukuhani, ili tumtumikie Mungu.
W. Ametuondolea dhambi zetu kwa damu yake.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Kristo...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Bwana amekuja kutusaidia sisi watumishi wake; ameikumbuka huruma yake.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana amekuja kutusaidia sisi watumishi wake; ameikumbuka huruma yake.

MAOMBI
Mungu, Baba yetu atupendaye, ayajua mahitaji yetu yote, na hututunza. Kwa imani na matumaini, tusali:
W. Baba, utuwezeshe kutulia katika upendo wako.

Mwanao Kristo aliteseka na kufa kwa ajili ya Kanisa:
- uwe faraja kwa Wakristo wote watakaoteseka leo usiku. (W.)

Uwaponye na uwatulize wagonjwa;
- uwatie nguvu kwa ushindi wa msalaba. (W.)

Uwe karibu nasi, Ee Mungu Mwenyezi,
- kwa kuwa wewe peke yako ndiye uwezaye kutuokoa na maovu na mikasa inayotuzingira. (W.)

Utuimarishe saa ya kufa,
- ili tufe katika amani yako. (W.)

Uwafikishe marehemu kwenye mwanga wako:
- ili wapate kufarijika mbele yako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tujumlishe masifu na dua zetu kwa maneno ya Kristo, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, tueleweshe mafundisho yatokanayo na mateso ya Mwanao, ili sisi, watu wako, tuweze kuchukua mzigo ambao, kwa ajili yetu, anaufanya uwe mwepesi. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.