Generic placeholder image

IJUMAA JUMA LA 13 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.

ANT. I: Nitashika amri zako, utakaponijalia moyo msikivu.

Zab.119:25-32 IV Mwongozo wa Mungu
Nagaagaa chini mavumbini,*
unipe tena uhai kama ulivyoahidi.

Nimeungama niliyotenda, nawe ukanisikiliza;*
unifundishe mwongozo wako.

Unifundishe namna ya kushika amri zako,*
nami nitayatafakari matendo yako ya ajabu.

Niko hoi kwa uchungu;*
unirudishie nguvu kama ulivyoahidi.

Uniepushe na njia ya upotovu;*
unijalie niijue sheria yako.

Nimechagua njia ya uaminifu;*
nimezingatia hukumu zako.

Ee Mungu, nimefuata maagizo yako;*
usikubali niaibishwe!

Nitafuata maagizo yako,*
maana unanipa maarifa zaidi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Nitashika amri zako, utakaponijalia moyo msikivu.

ANT. II: Namtumainia Bwana; nami sijatetereka.

Zab.26 Sala ya mtu mwema
Mungu ametuteua tuwe watu wake katika kuungana na Kristo, ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake (uf.1:4)

Ee Mungu, unitetee,/
maana nimeishi bila hatia,*
nakutumainia wewe bila kusita.

Unijaribu, Ee Mungu, na kunichunguza;*
upime moyo wangu na akili yangu.

Upendo wako mkuu waniongoza;*
nimeishi kufuatana na ukweli wako.

Siandamani na watu wapotovu;*
sishirikiani na watu wanafiki.

Nachukia kujumuika na wabaya;*
wala sitaandamana na waovu.

Nanawa mikono yangu, Ee Mungu,*
kuonyesha kwamba sina hatia;

najiunga na maandamano ya ibada,*
kuzunguka madhabahu yako,

nikiimba wimbo wa kukushukuru,*
na kutangaza matendo yako ya ajabu.

Ee Mungu, napenda makao yako,*
mahali unapokaa utukufu wako.

Usinipatilize pamoja na wenye dhambi,*
wala usinitupe pamoja na wauaji:

Watu ambao matendo yao ni maovu daima,*
watu ambao daima hula rushwa.

Lakini mimi hutenda yaliyo sawa;*
unihurumie na kunikomboa.

Kama nikiwa imara na salama,*
nitamsifu Mungu kati ya jamii kubwa ya watu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Namtumainia Bwana; nami sijatetereka.

ANT. III: Moyo wangu wamtumainia Bwana, na hivi nimehifadhiwa.

Zab.28:1-3,6-9 Kuomba msaada
Nakushukuru Baba, kwa kuwa wewe wanisikiliza (Yoh.11:41)

Nakulilia, Ee Mungu, mwamba wa usalama wangu!/
Unisikilize, usiwe kama kiziwi kwangu;*
nisije nikawa kama wale washukao shimoni kwa wafu.

Unisikilize niombapo msaada,/
niinuapo mikono yangu,*
kuelekea mahali pako patakatifu.

Usinihukumu pamoja na watu wabaya,*
pamoja na watu watendao maovu:

watu wasemao maneno mazuri,*
kumbe wamejaa uhasama moyoni mwao.

Atukuzwe Mungu,*
maana amesikiliza ombi langu.

Mungu ndiye nguvu yangu na ngao yangu;*
namtumainia yeye kwa moyo wangu wote.

Ananisaidia na kunifurahisha;*
nitamsifu kwa tenzi za shangwe.

Mungu ni nguvu ya watu wake;*
humkinga na kumwokoa mfalme wake mteule.

Ee Mungu, uwaokoe watu wako;/
uwabariki hao watu walio mali yako.*
Uwachunge na kuwalinda hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Moyo wangu wamtumainia Bwana, na hivi nimehifadhiwa.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Filp.2:2b-4
Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake. Muwe na fikra moja, upendo mmoja, moyo mmoja na nia moja. Msifanye cho chote kwa moyo wa fitina, au kwa majivuno ya bure; mwe na unyenyekevu ninyi kwa ninyi, na kila mmoja amwone mwenzake kuwa bora kuliko yeye mwenyewe. Pasiwe na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe tu, bali faida ya mwenzake.

K. Njia za Bwana ni uaminifu na upendo.
W. Hizo ndizo njia zao washikao agano lake, na kutekeleza matakwa yake.

SALA:
Tuombe: Bwana Yesu Kristo, saa hii ulikwenda njia ya msalaba, kufa kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Kwa huruma yako utusamehe makosa tuliyoyafanya, na kwa uwezo wako utusaidie tusianguke tena. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: 2Kor.13:4
Hata kama alisulibiwa kwa sababu ya udhaifu, lakini sasa anaishi kwa uwezo wa Mungu. Sisi pia tu dhaifu kwa kuungana naye, lakini tutaishi naye kwa uwezo wa Mungu kwa ajili yenu.

K. Roho yangu inalala katika mavumbi.
W. Ee Bwana, unihuishe kwa neno lako.

SALA:
Tuombe: Ee Bwana Yesu Kristo, ambaye saa kama hii, dunia nzima ilipokuwa imefunikwa na giza, ulitundikwa msalabani, ukauawa bila kosa, kwa ajili ya ukombozi wetu, utujalie daima mwanga huo utakaotufikisha kwenye uzima wa milele. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Kol.3:12-13
Ninyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo, basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. Vumilianeni na kusamehea na iwapo mmoja wenu analo jambo lo lote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa ķusameheana kama Bwana alivyowasamehe ninyi.

K. Bwana ni huruma na upendo.
W. Yeye ni mwingi wa huruma, si mwepesi wahasira.

SALA:
Tuombe: Ee Bwana Yesu Kristo, ulipokuwa msalabani ulimwahidia ufalme wako yule mwizi aliyetubu; kwa imani, matumaini na toba, tunakuomba huruma yako, ili baada ya kufa kwetu tufurahie kuingizwa nawe mbinguni. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.