IJUMAA JUMA 13 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Amo.8:4-6,9-12
Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi, tupate kuuza nafaka? Mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu, tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano. Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana Mungu, nitalifanya jua litue wakati wa adhuhuri, nami nitaitia nchi giza wakati wa nuru wa mchana. Nami nitazigeuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio; nami nitatia nguo za magunia katika viuno vyote, na upaa katika kila kichwa; nami nitayafanya haya kuwa kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu. Angalia, siku zinakuja, asema Bwana Mungu, ambazo nitaleta njaa katika nchi, si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana. Nao watatangatanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazini hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:2,10,20,30,40,131(K)Mt.4:4
1. Heri wazitiio shuhuda zake,
wamtafutao kwa moyo wote.
Kwa moyo wangu wote nimekutafuta,
usiniache nipotee mbali na maagizo yako.

(K) Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

2. Roho yangu imepondeka kwa kutamani,
hukumu zako kila wakati.
Nimeichagua njia ya uaminifu,
na kuziweka hukumu zako mbele yangu. (K)

3. Tazama, nimeyatamani mausia yako,
unihuishe kwa haki yako.
Nalifungua kinywa changu nikatweta,
maana naliyatamani maagizo yako. (K)

SHANGILIO: Zab.147:12,15
Aleluya, aleluya!
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya!

INJILI: Mt.9:9-13
Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata. Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.