Generic placeholder image

IJUMAA JUMA LA 15 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Mshukuruni Bwana, kwa kuwa pendo lake kuu ni la milele.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Tunakutukuza Baba
Ee Bwana wa uhai
Kila kiumbe kizima
Wewe chakuelekea
Chanzo cha utakatifu
Na kisima cha neema
Wewe ni asili yetu
Na pia kikomo chetu.

Tunakushukuru Wewe
Kristo Mkombozi
Mzigo wetu ulibeba
Wa dhambi na aibu
Kwa ushindi wa fumbo
Uliangamiza dhambi
Na kwa kufa kwako
Uliyashinda mauti.

Njoo Roho Mtakatifu
Moto wenye kupekua
Mwali wake moto huo
Uovu huteketeza.
Shuka chini kwetu sisi
Lete mwanga na upendo
Njoo ukakae kwetu
Kwa utulivu na amani.

Twakusifu, twakusifu
Utatu Mungu Mmoja
Utatu wenye kutisha
Kwa adhama na uweza
Ndiwe Bwana wa vyote
Utawalaye milele
Katika utukufu
Na mwanga wa milele.

ANT. I: Nimekukosea wewe peke yako; Bwana, unihurumie.

Zab.51 Kuomba msamaha
Jirekebisheni upya rohoni na katika fikra zenu. Vaeni hali mpya ya utu (Uf.4:23-24)

Unihurumie, Ee Mungu,*
kwa sababu ya upendo wako mkuu;

ufutilie mbali uovu wangu,*
kwa sababu ya huruma yako kuu.

Unioshe kabisa kosa langu;*
unisafishe dhambi yangu.

Nakiri kabisa makosa yangu,*
daima naiona waziwazi dhambi yangu.

Nimekukosea wewe peke yako,*
nimetenda yaliyo mabaya mbele yako.

Hivyo wafanya sawa unaponihukumu,*
una haki kabisa unaponiadhibu.

Mimi ni mkosefu tangu kuzaliwa kwangu,*
mwenye dhambi tangu tumboni mwa mama yangu.

Wewe wataka unyofu wa ndani;*
hivyo nifundishe hekima moyoni.

Uniondolee dhambi, nitakate;*
unioshe, niwe mweupe pе.

Hapo nitaweza kufurahi tena;*
nitashangilia tena ingawa uliniponda.

Ugeuze uso wako, usiziangalie dhambi zangu;*
ukayafute makosa yangu yote.

Ee Mungu, uniumbie moyo safi,*
uweke ndani yangu roho mpya na thabiti.

Usinitupe mbali nawe;*
usiniondolee Roho wako mtakatifu.

Unifanye nifurahi tena kwa kuniokoa,*
unijalie moyo radhi wa utii.

Hapo nitawafundisha wakosefu mwongozo wako,*
nao wenye dhambi watarudi kwako.

Ee Mungu, Mungu mwokozi wangu, uniokoe na kifo,*
nami nitatangaza kwa furaha uadilifu wako.

Ifumbue midomo yangu, Ee Bwana,*
nipate kutangaza sifa zako.

Kwa kweli wewe hupendezwi na sadaka,/
ama sivyo mimi ningalikutolea.*
Wewe huna haja na sadaka za kuteketezwa.

Sadaka yangu kwako, Ee Mungu, ni moyo mnyofu;*
wewe, Ee Mungu, hukatai moyo mnyofu na mtiifu.

Ee Mungu, uutendee mji Sion mema:*
jenga tena upya kuta za Yerusalemu.

Hapo utapendezwa na sadaka za kweli;/
dhabihu na sadaka za kuteketezwa*
na fahali watatolewa sadaka madhabahuni pako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Nimekukosea wewe peke yako; Bwana, unihurumie.

ANT. II: Bwana, twazijua dhambi zetu; tumekukosea wewe.

WIMBO: Yer.14:17-21 Maombolezo ya watu wakati wa njaa na vita
Utawala wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema (Mk.1:15)

Macho yangu na yatiririke machozi,*
usiku na mchana, wala yasikome;

kwa maana bikira, binti ya watu wangu,/
amevunjika mavunjiko makuu,*
kwa jeraha isiyoponyeka.

Nikitoka kwenda shambani,*
tazama, wako huko waliouawa kwa upanga!

na nikiingia mjini,*
tazama, wamo humo wanaougua kwa sababu ya njaa!

maana nabii na kuhani, wote wawili,/
huenda huko na huko katika nchi,*
wala hawana maarifa.

Je! umemkataa Yuda kabisa?*
roho yako imeichukia Sion?

Mbona umetupiga,*
tusiwe na dawa ya kutuponya?

Tulitazamia amani,*
lakini hayakuja mema yo yote;

tulitazamia wakati wa kupona,*
na tazama, kufadhaika tu!

Ee BWANA, tunakiri uovu wetu,/.
na ubaya wa baba zetu;*
maana tumekutenda dhambi.

Usituchukie, kwa ajili ya jina lako;/
usikifedheheshe kiti cha enzi cha utukufu wako;*
kumbuka, usilivunje agano ulilofanya nasi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana, twazijua dhambi zetu; tumekukosea wewe.

ANT. III: Bwana ni Mungu; sisi tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.

Zab.100 Wimbo wa sifa
Bwana awaita wote aliowakomboa, waimbe utenzi wa ushindi (Mt. Athanasius)

Mwimbieni Mungu*
enyi walimwengu wote!

Mwabuduni Mungu kwa furaha,*
nendeni kwake mkiimba kwa shangwe!

Jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mungu./
Yeye ndiye aliyetuumba, nasi tu mali yake;*
sisi ni watu wake, na kondoo wa malisho yake.

Pitieni milango ya Hekalu lake kwa shukrani,/
ingieni katika makao yake kwa sifa.*
Mpeni shukrani, na kulisifu jina lake.

Mungu ni mwema;/
upendo wake mkuu ni wa milele,*
na uaminifu wake wadumu milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana ni Mungu; sisi tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.

SOMO: 2Kor.12:9b-10
Basi, ni radhi kabisa kujivunia udhaifu wangu, ili uwezo wake Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo nakubali kwa radhi udhaifu, madharau, taabu, udhalimu na mateso, kwa ajili ya Kristo; maana ninapokuwa dhaifu, ndipo ninapokuwa na nguvu.

KIITIKIZANO
K. Asubuhi unifanye, Ee Bwana, nitambue mapendo yako. (W. Warudie)
K. Unijulishe njia gani nipite.
W. Nitambue mapendo yako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Asubuhi...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Bwana amewajia watu wake, na kuwakomboa.

WIMBO WA ZAKARIA Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana amewajia watu wake, na kuwakomboa.

MAOMBI
Tunaye kuhani mkuu, anayeweza kutuonea huruma katika unyonge wetu, ambaye, kwa kuwa amefanana nasi, alishawishiwa kwa kila namna, lakini hakutenda dhambi. Na tumwombe:
W. Utuoneshe wema na huruma yako.

Bwana, kwa ajili ya furaha ambayo ungeipata baadaye, ulikubali kufa msalabani;
- utushirikishe kifo chako, ili tuweze pia kushiriki furaha yako. (W.)

Bwana ulisema, 'Kila aonaye kiu, na aje kwangu, anywe':
- uwape sasa Roho wako wale wanaokuonea kiu. (W.)

Uliwatuma wafuasi wako kuihubiri Habari Njema kwa kila taifa:
- uwabariki wanaume na wanawake, ambao wanatolea siku hizi maisha yao kuihubiri Injili. (W.)

Uwasaidie wale wanaotaabika, watambue kwamba Baba anawatunza,
- kwani Yeye huwapenda kama ampendavyo Mwanae wa pekee. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tunapoungojea ujio wa utawala wa Mungu, tusali tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Baba Mwenyezi, ifanye nuru yako iangaze akili zetu hivi, hata tunapoishi kadiri ya amri zako, tuweze kukufuata wewe, kiongozi wetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.