Generic placeholder image

IJUMAA JUMA LA 15 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Mungu alipomwumba mtu,
Alimpa dunia yote,
Alimpa yote mimea,
Kila ndege kila mnyama;
Na kwa amri yake Bwana
Adamu livipa majina,
Na vyote akavitiisha,
Vidogo na vikubwa pia.

Mungu alimuumba mtu
Kwa mfano na sura yake,
Na alipoufanya uso
Wa mtu tokana udongo
Hapo sura ikatokea
Ya Mwana wake wa pekee:
Neno wake mwenye muili
Kajaa neema na kweli.

Mbingu na dunia pamoja
Sifa zitoe kwake Baba,
Na kwa Mwanae Kristo,
Na kwa Mtakatifu Roho.
Viumbe vyote kwa sauti,
Kwa sauti kubwa vyasema:
Ni Mtakatifu kabisa
Bwana Mwenyezi wa daima.

ANT. I: Bwana ni mkuu; Mungu wetu yu juu ya miungu yote.

Zab.135 Sifa kwa Mungu
Ninyi ni ukoo mteule, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani, akawaingizeni katika mwanga wake mkuu (1Pet.2:9)

I
Lisifuni jina la Mungu,*
enyi watumishi wa Mungu,

mnaosimama nyumbani mwa Mungu,*
Hekaluni mwa Mungu wetu.

Msifuni Mungu kwa kuwa ni mwema;*
liimbieni jina lake sifa, maana inafaa.

Mungu amejichagulia Yakobo kuwa wake,*
watu wa Israeli kuwa mali yake mwenyewe.

Najua hakika kuwa Mungu ni mkuu;*
Bwana wetu ni mkuu juu ya miungu yote.

Mungu hufanya yote anayotaka,*
mbinguni, duniani, baharini na vilindini.

Huleta mawingu kutoka mipaka ya dunia;/
hufanya gharika kuu kwa umeme,*
na huvumisha upepo kutoka ghala zake.

Aliwaua wazaliwa wa kwanza kule Misri,*
wazaliwa wa watu na wanyama kadhalika.

Alifanya ishara na maajabu kwako, Ee Misri,*
dhidi ya Farao na maofisa wake wote.

Aliyaangamiza mataifa mengi,*
akawaua wafalme wenye nguvu:

akina Sihoni, mfalme wa Waamori,*
na Ogu, mfalme wa Bashani, na wafalme wote wa Kanaani.

Alichukua nchi zao na kuwapa watu wake;*
aliwapa Waisraeli ziwe urithi wao.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana ni mkuu; Mungu wetu yu juu ya miungu yote.

ANT. II: Wana wa Israeli, msifuni Bwana! Mwimbieni Bwana zaburi kwa kuwa ni mwema.

II
Ee Mungu, jina lako lakumbukwa milele,*
utakumbukwa na watu wa vizazi vyote.

Maana Mungu atawatetea watu wake;*
atakuwa na huruma kwa watumishi wake.

Miungu ya mataifa ni fedha na dhahabu,*
imetengenezwa na mikono ya binadamu.

Ina vinywa, lakini haisemi;*
ina macho, lakini haioni.

Ina masikio, lakini haisikii;*
wala haiwezi hata kuvuta pumzi.

Wote walioifanya wafanane nayo,*
naam, kila mmoja anayeitegemea!

Enyi watu wa Israeli, mtukuzeni Mungu!*
Enyi makuhani, wazao wa Aroni, mtukuzeni Mungu!

Enyi Walawi, mtukuzeni Mungu!*
Enyi wachaji wa Mungu, mtukuzeni.

Atukuzwe Mungu katika Sion,*
katika makao yake Yerusalemu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Wana wa Israeli, msifuni Bwana! Mwimbieni Bwana zaburi kwa kuwa ni mwema.

ANT. III: Mataifa yote yatakuja kukuabudu, Ee Bwana.

WIMBO: Ufu.15:3-4. Utenzi wa sifa
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!

Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!

Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako? *
Wewe peke yako ni Mtakatifu.

Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mataifa yote yatakuja kukuabudu, Ee Bwana.

SOMO: Yak.1:2-4
Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali, kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu. Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa cho chote.

KIITIKIZANO
K. Kristo alitupenda, na ametuondolea dhambi zetu kwa damu yake. (W. Warudie)
K. Ametushirikisha ufalme na ukuhani, ili tumtumikie Mungu.
W. Ametuondolea dhambi zetu kwa damu yake.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Kristo...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Bwana amekuja kutusaidia sisi watumishi wake; amekumbuka huruma yake.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana amekuja kutusaidia sisi watumishi wake; amekumbuka huruma yake.

MAOMBI
Baba, Kristo aliomba tusamehewe makosa yetu kwa njia ya mateso yake. Kama ulivyomkubali yeye, uikubalie pia sala yake kwa ajili ya wakosefu wote.
W. Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.

Kwa njia ya mfuasi wake mpendwa, Yesu ametuachia Maria awe mama yetu;
- pamoja na Mama Maria, tunawaombea watu wote. (W.)

Baba, uwafariji wale wanaokulilia pamoja na Mwanao:
- 'Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?'. (W.)

Utuwezeshe kuwasikia wanaolia: 'Naona kiu';
- utusaidie tuweze kumwona Mwanao, hata katika ndugu zake walio wadogo sana. (W.)

Yesu alimwambia yule mwizi aliyesulibiwa pamoja naye: 'Nakuambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami mahali pema peponi.'
- Baba, yafanye maneno hayo yasikike tena kwa wale watakaokufa leo. (W.)

Tunawaombea wale waliofariki dunia wakiwa na alama ya msalaba:
- wafufuke kwa utukufu pamoja na Kristo, wakati sauti yake itakaposikika tena ulimwenguni: 'Yametimia.' (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tujumlishe masifu na dua zetu kwa maneno ya Kristo, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Bwana, Baba Mwema, ulitaka Mwanao Yesu Kristo afe msalabani ili atukomboe. Ujalie neema tuweze kuishi hivi, ili kwa kushiriki mateso yake tuimarishwe kwa nguvu ya ufufuko wake, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.