Generic placeholder image

IJUMAA JUMA LA 15 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Bwana Mungu na wa vyote Muumba,
Ulimwengu nawe wategemezwa.
Vyote hubadilika na kuoza,
Wewe hapana, wabaki ni Mpya.

Ndiwe faraja na ya mtu kinga,
U Mwamba juu yake wa kujenga,
Ndiwe makao tulivu ya roho,
Yote hutimilika ndani yako.

Asifiwe Baba na Mwana Mungu,
Asifiwe Roho Mtakatifu;
Na utukuzwe Utatu milele,
Nguvu yetu maisha yetu yote.

ANT. I: Tulimwona amedharauliwa na watu, mtu wa huzuni na masikitiko.

Zab.22 Kilio (Zaburi ya Daudi)
Yesu akalia kwa sauti kubwa:"Eli, Eli, lama sabakthani?” (Mt.27:46)

I
Mungu wangu, Mungu wangu!*
Kwa nini umeniacha?

Mbona uko mbali sana kunisaidia,*
mbali na maneno ya kilio changu?

Mungu wangu! Nalia mchana lakini husikilizi;*
napiga yowe usiku, lakini nafuu sipati.

Hata hivyo, wewe ni mtakatifu;*
wewe unayesifiwa na watu wa Israeli.

Wazee wetu walikutegemea;*
walikutegemea, nawe ukawaokoa.

Walikulilia hatarini, wakasalimika;*
walikutumainia, nao hawakuaibika.

Lakini mimi ni mdudu tu, wala si mtu;*
nimepuuzwa na kudharauliwa na kila mtu.

Wote wanionao wananicheka;*
wananifyonya na kutikisa vichwa.

Wanasema: "Si ulimtumainia Mungu?*
Kwa nini sasa hakuokoi?

Kama anapendezwa nawe,*
basi, na akusalimishe!"

Lakini wewe, Ee Mungu,/
ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,*
na kunilinda nilipokuwa mtoto mchanga.

Nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu;*
tangu nilipozaliwa wewe u Mungu wangu.

Usikae mbali nami, kwani taabu imekaribia;*
uwe karibu, maana hakuna wa kunisaidia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Tulimwona amedharauliwa na watu, mtu wa huzuni na masikitiko.

ANT. II: Wakagawana mavazi yake kwa kupiga kura.

II
Adui wengi wanizunguka kama fahali;*
wamenisonga kama fahali wakali wa Bashani!

Wanafunua vinywa vyao kama simba,*
tayari kunishambulia na kunirarua.

Nimekwisha kama maji yaliyomwagika;/.
mifupa yangu yote imeteguka;*
moyo wangu ni kama nta iliyoyeyuka.

Koo langu limekauka kama kigae;/
ulimi wangu wanata kinywani mwangu.*
Umeniacha mfu mavumbini.

Genge la waovu limenizunguka;/
wananizingira kama kundi la mbwa;*
mikono na miguu wamenitoboa.

Nimebaki mifupa mitupu;*
adui zangu waniangalia na kunisimanga.

Wanagawiana nguo zangu;*
wanalipigia kura vazi langu.

Ee Mungu, usisimame mbali nami.*
Ewe unisaidiaye, uje upesi kunisaidia.

Niokoe na upanga!*
Niepushe na mbwa hawa!

Niokoe kinywani mwa simba;*
mimi ni dhaifu mbele ya nyati hawa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Wakagawana mavazi yake kwa kupiga kura.

ANT. III: Familia zote za mataifa, zitaabudu mbele ya Bwana.

III Shukrani
Nitawatangazia ndugu zangu matendo yako;*
nitakusifu katika jamii yao:

"Enyi watumishi wa Mungu, msifuni!/
Enyi wana wa Yakobo, mtukuzeni Mungu;*
enyi watu wote wa Israeli, mwabuduni.

Maana yeye hadharau unyonge wa maskini,/
wala kupuuza mateso yao;*
hawapi kisogo, bali huwajibu wamwombapo msaada."

Wewe wanijalia kukusifu/
katika jamii kubwa ya watu;*
nitatimiza nadhiri zangu mbele yao wakuchao.

Maskini watakula na kushiba;/
wanaomtafuta Mungu watamsifu.*
Wafanikiwe milele!

Ulimwengu wote utakumbuka/
na kumrudia Mungu;*
jamaa zote za mataifa zitamwabudu.

Maana Mungu ni mfalme;*
yeye anayetawala mataifa.

Wenye kiburi wote watasujudu mbele yake;*
wote ambao hufa watamwabudu.

Vizazi vijavyo vitamtumikia;*
watu watavisimulia habari za Bwana,

na watatangaza matendo yake ya wokovu,/
kwa watu wasiozaliwa bado;*
kwamba: “Mungu amefanya hayo!”

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Familia zote za mataifa, zitaabudu mbele ya Bwana.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Rom.1:16b-17
Injili yenyewe ni nguvu ya Mungu inayowaokoa wote wanaoamini: Wayahudi kwanza, na wasio Wayahudi pia. Kwa maana injili inaonesha wazi jinsi Mungu anavyowafanya watu wawe na uhusiano mwema naye: Jambo hili hufanyika kwa imani, tangu mwanzo mpaka mwisho. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye uhusiano mwema na Mungu kwa imani, ataishi."

K. Katika Bwana nyoyo zetu zitafurahia.
W. Kwani tumeliamini jina lake takatifu.

SALA:
Tuombe: Bwana Yesu Kristo, saa hii ulikwenda njia ya msalaba, kufa kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Kwa huruma yako utusamehe makosa tuliyoyafanya, na kwa uwezo wako utusaidie tusianguke tena. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Rom.3:21-22a
Njia ya Mungu ya kuwafanya watu wawe na uhusiano mwema naye imekwisha dhihirishwa, tena bila kutegemea Sheria. Sheria na manabii hushuhudia jambo hili. Mungu huwafanya watu wawe na uhusiano mwema naye kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo.

K. Maagizo ya Bwana ni ya adili, huufurahisha moyo.
W. Amri ya Bwana ni wazi, huyatia macho mwanga.

SALA:
Tuombe: Ee Bwana Yesu Kristo, ambaye saa kama hii, dunia nzima ilipokuwa imefunikwa na giza, ulitundikwa msalabani ukauawa bila kosa, kwa ajili ya ukombozi wetu; utujalie daima mwanga huo utakaotufikisha kwenye uzima wa milele. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Ef.2:8-9
Kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu. Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu.

K. Ee Bwana, njia yako ijulikane duniani.
W. Na mataifa yote yautambue wokovu wako.

SALA:
Tuombe: Ee Bwana Yesu Kristo, ulipokuwa msalabani ulimwahidia ufalme wako yule mwizi aliyetubu; kwa imani, matumaini na toba, tunakuomba huruma yako, ili baada ya kufa kwetu tufurahie kuingizwa nawe mbinguni. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.