Generic placeholder image

IJUMAA JUMA LA 16 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Baba wa milele, Mungu wa pendo,
Ambaye kwa vumbi ulituumba,
Tugeuze kwa neema ya Roho,
Tutie thamani tulio duni.

Utuandae kwa siku ya siku
Atakapokuja Kristo kwa enzi
Kutugeuza tena toka vumbi
Na miili yetu kuing'arisha.

Ee Mungu, hujaonwa, hujaguswa,
Viumbe vyote vyakudhihirisha;
Mbegu ya utukufu ndani mwetu
Itachanua tutapokuona.

ANT. I: Bwana, waipendao sheria yako wana amani tele.

Zab.119 XXI (161-168)
Wakuu wanidhulumu bila kisa,*
lakini mimi naziheshimu sheria zako kwa moyo wote.

Nafurahi kwa sababu ya ahadi yako,*
kama mtu aliyekuta kitu cha thamani.

Nachukia kabisa uwongo,*
lakini naipenda sheria yako.

Nakusifu mara saba kila siku,*
kwa sababu ya hukumu zako za haki.

Wapendao sheria yako wana amani kuu;*
hakuna kinachoweza kuwaangusha.

Ee Mungu, nakungojea uniokoe;*
natimiza amri zako.

Nashika mafundisho yako,*
nayapenda kwa moyo wote.

Natii amri na maagizo yako;*
wewe waona kila kitu nifanyacho.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana, waipendao sheria yako wana amani tele.

ANT. II: Jamii yote ya waamini, ilikuwa na nia moja na roho moja.

Zab.133 Uzuri wa umoja wa kidugu
Tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu (1Yoh.4:7)

Ni jambo zuri na la kupendeza mno*
ndugu kuishi pamoja kwa moyo mmoja.

Ni kama mafuta safi kabisa/
yatiririkayo kichwani na ndevuni mwa Aroni,*
hata mpaka katika vazi lake shingoni.

Ni kama umande wa mlima Hermoni,*
unaoanguka juu ya milima ya Sion.

Hapo ndipo Mungu alipoahidi baraka yake,*
uhai usio na mwisho.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Jamii yote ya waamini, ilikuwa na nia moja na roho moja.

ANT. III: Ee Bwana, uliye kimbilio langu kuu, uniepushe na mikono ya waovu.

Zab.140:1-8,12-13 Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi (Mt.26:45)

Ee Mungu, uniokoe na watu wabaya,*
unikinge na watu wakatili.

Watu hao huwaza mabaya daima,*
huzusha magomvi kila siku.

Ndimi zao hatari kama nyoka wa sumu;*
maneno yao ni kama sumu ya joka.

Ee Mungu, unilinde na makucha ya wabaya;*
unikinge na wakatili wanaonuia kuniangusha.

Wenye kiburi wamenitegea mitego,/
wametandaza kamba kama wavu,*
wameficha mitego njiani wanikamate.

Namwambia Mungu, “Wewe ndiwe Mungu wangu."*
Usikilize, Ee Mungu, sauti ya ombi langu.

Ee Mungu, Bwana wangu, mwamba wa usalama wangu,*
umenikinga wakati wa vita.

Ee Mungu, usiwape waovu wanayotaka;*
wala mipango yao usiifanikishe.

Najua kwamba Mungu atamlinda mnyonge,*
na kuzitetea haki za mhitaji.

Hakika waadilifu watalisifu jina lako;*
wanyofu watakaa kwako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Ee Bwana, uliye kimbilio langu kuu, uniepushe na mikono ya waovu.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Rom.12:17a,19b-21
Msilipe ovu kwa ovu; maana Maandiko matakatifu yasema: "Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza, asema Bwana.“ Zaidi ya hayo, Maandiko yasema: "Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe cha kunywa. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake." Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema.

K. Fadhili za Bwana zadumu milele.
W. Huwatendea haki wale washikao amri zake.

SALA:
Tuombe: Bwana Yesu Kristo, saa hii ulikwenda njia ya msalaba, kufa kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Kwa huruma yako utusamehe makosa tuliyoyafanya, na kwa uwezo wako utusaidie tusianguke tena. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: 1Yoh.3:16
Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi, vile vile, tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu.

K. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.
W. Upendo wake mkuu ni wa milele.

SALA:
Tuombe: Ee Bwana Yesu Kristo, ambaye saa kama hii, dunia nzima ilipokuwa imefunikwa na giza, ulitundikwa msalabani, ukauawa bila kosa, kwa ajili ya ukombozi wetu; utujalie daima mwanga huo utakaotufikisha kwenye uzima wa milele. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: 1Yoh.4:9-11
Mungu alionesha upendo wake kwetu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tuwe na uzima kwa njia yake. Hivi ndivyo upendo ulivyo: si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kutuondolea dhambi zetu. Wapenzi wangu, ikiwa Mungu alitupenda hivyo, basi, nasi tunapaswa kupendana.

K. Ee Mungu, mlinzi wetu, utuelekezee macho yako.
W. Uangalie uso wa mtumishi wako.

SALA:
Tuombe: Ee Bwana Yesu Kristo, ulipokuwa msalabani ulimwahidia ufalme wako yule mwizi aliyetubu; kwa imani, matumaini na toba tunakuomba huruma yako, ili baada ya kufa kwetu tufurahie kuingizwa nawe mbinguni. Unayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.