IJUMAA JUMA 1 LA KWARESIMA
MASOMO

SOMO 1: Eze.18:21-28
Bwana asema hivi: mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki, hakika ataishi, hatakufa. Dhambi zake zote alizozitenda hazitakumbukwa juu yake hata mojawapo; katika haki yake aliyoitenda ataishi. Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana MUNGU; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi? Bali mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, na kufanya machukizo yote kama yale afanyayo mtu mwovu, je, ataishi? Katika matendo yake yote ya haki aliyoyatenda halitakumbukwa hata mojawapo. Katika kosa lile alilolikosa, naam, katika dhambi yake aliyoitenda, atakufa. Lakini ninyi mwasema, Njia ya Bwana si sawa. Sikilizeni sasa, Enyi nyumba ya Israeli; Je! Njia yangu siyo iliyo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa? Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, akafa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa. Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai. Kwa sababu atafakari, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.130(K)3
1. Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia.
Bwana, uisikie sauti yangu.
Masikio yako na yaisikilize Sauti ya dua zangu.

(K) Bwana kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana nani angesimama?

2. Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
Ee Bwana, nani angesimama?
Lakini kwako kuna msamaha, Ili Wewe uogopwe. (K)

3. Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja,
Na neno lake nimelitumainia.
Nafsi yangu inamngoja Bwana,
Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,
Naam, walinzi waingojao asubuhi.
Ee Israeli, umtarajie Bwana; (K)

4. Maana kwa Bwana kuna fadhili,
Na kwake kuna ukombozi mwingi.
Yeye atamkomboa Israeli na maovu yake yote. (K)

SHANGILIO: Yoe.2:12-13
Hata sasa, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, Asema Bwana, kwa maana mimi ndiye mwenye neema, Nimejaa huruma.

INJILI: Mt.5:20-26
Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.

MAOMBI
Ndugu, mtu mwenye dhambi anafananishwa na mtu aliyekufa kwani anakosa uzima ndani yake. Kwaresima ni kipindi cha neema chenye kutuletea uzima mpya kwa mema tunayotenda. Ee Mungu, twakuomba:

Kiitikio: Mungu wa matumaini, utusikie.
1. Hali ya utakatifu wa viongozi wa dini na ya wahubiri wote wa neno lako iwe kichocheo kwa wote wanoutafuta wokovu ili waupate.

2. Utuepushe na hukumu tusizostahili kuzitoa kwa ndugu zetu wazima na wafu.

3. Utupe ari ya kupatana na wenzetu tuliokosana nao kabla ya kukutolea wewe sadaka takatifu.

4. Uwasamehe dhambi zote ndugu zetu waliofariki dunia na uwajalie uzima wa milele.

Tunaomba hayo yote kwako wewe uliye Mtakatifu, ili nasi tuwe watakatifu kama wewe. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.