Generic placeholder image

IJUMAA JUMA LA 1 MAJILIO
MASIFU YA ASUBUHI

ANTIFONA YA MWALIKO:
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

Ant. ya Mwaliko
Tumwabudu Bwana, mfalme atakayekuja.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Sikieni sauti ya mjumbe
'Kristo yu karibu', yasema,
'Tupieni mbali za giza ndoto,
Na mkaribisheni Kristo,
Yeye aliye nuru ya mchana!'

Roho iloshikana na dunia
Iamshwe na hilo onyo kali;
Yesu Kristo ni lake jua,
Liondoalo ulegevu wote,
Asubuhi uwinguni hung'aa.

Basi na atakapokuja tena
Kwa utukufu na vitisho vingi,
Na kuifunika hofu dunia,
Na atokee katika mawingu
Aje na kuwa wetu mtetezi.

ANT. I: Bwana, utapendezwa na sadaka za haki, zitakazotolewa altareni pako.

Zab.51 Kuomba msamaha
Jirekebisheni upya rohoni na katika fikra zenu. Vaeni hali mpya ya utu (Uf.4:23-24)

Unihurumie, Ee Mungu,*
kwa sababu ya upendo wako mkuu;

ufutilie mbali uovu wangu,*
kwa sababu ya huruma yako kuu.

Unioshe kabisa kosa langu;*
unisafishe dhambi yangu.

Nakiri kabisa makosa yangu,*
daima naiona waziwazi dhambi yangu.

Nimekukosea wewe peke yako,*
nimetenda yaliyo mabaya mbele yako.

Hivyo wafanya sawa unaponihukumu,*
una haki kabisa unaponiadhibu.

Mimi ni mkosefu tangu kuzaliwa kwangu,*
mwenye dhambi tangu tumboni mwa mama yangu.

Wewe wataka unyofu wa ndani;*
hivyo nifundishe hekima moyoni.

Uniondolee dhambi, nitakate;*
unioshe, niwe mweupe pе.

Hapo nitaweza kufurahi tena;*
nitashangilia tena ingawa uliniponda.

Ugeuze uso wako, usiziangalie dhambi zangu;*
ukayafute makosa yangu yote.

Ee Mungu, uniumbie moyo safi,*
uweke ndani yangu roho mpya na thabiti.

Usinitupe mbali nawe;*
usiniondolee Roho wako mtakatifu.

Unifanye nifurahi tena kwa kuniokoa,*
unijalie moyo radhi wa utii.

Hapo nitawafundisha wakosefu mwongozo wako,*
nao wenye dhambi watarudi kwako.

Ee Mungu, Mungu mwokozi wangu, uniokoe na kifo,*
nami nitatangaza kwa furaha uadilifu wako.

Ifumbue midomo yangu, Ee Bwana,*
nipate kutangaza sifa zako.

Kwa kweli wewe hupendezwi na sadaka,/
ama sivyo mimi ningalikutolea.*
Wewe huna haja na sadaka za kuteketezwa.

Sadaka yangu kwako, Ee Mungu, ni moyo mnyofu;*
wewe, Ee Mungu, hukatai moyo mnyofu na mtiifu.

Ee Mungu, uutendee mji Sion mema:*
jenga tena upya kuta za Yerusalemu.

Hapo utapendezwa na sadaka za kweli;/
dhabihu na sadaka za kuteketezwa*
na fahali watatolewa sadaka madhabahuni pako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana, utapendezwa na sadaka za haki, zitakazotolewa altareni pako.

ANT. II: Wazao wote wa Israeli watapewa haki, na watatukuka katika Bwana.

WIMBO: Isa.45:15-25 Watu wote watamwongokea Bwana.
Kwa heshina ya jina la Yesu, viumbe vyote...vipige magoti mbele yake (Filp.2:10)

Hakika wewe u Mungu ujifichaye nafsi yako,*
Ee Mungu wa Israeli, Mwokozi.

Watatahayarika, naam, watafadhaika, wote pia;*
wale wafanyao sanamu wataingia fadhaa pamoja.

Bali Israeli wataokolewa na BWANA*
kwa wokovu wa milele;

ninyi hamtatahayarika,*
wala kufadhaika, milele na milele.

Maana BWANA, aliyeziumba mbingu, asema hivi:*
"Yeye ni Mungu;

ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya;*
ndiye aliyeifanya imara;

hakuiumba ukiwa,*
aliumba ili ikaliwe na watu.

Mimi ni BWANA,*
wala hapana mwingine.

Sikusema kwa siri,*
katika mahali pa nchi ya giza;

sikuwaambia wazao wa Yakobo:*
Nitafuteni bure.

Mimi, BWANA, nasema haki;*
nanena mambo ya adili.

Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja,*
ninyi wa mataifa mliookoka.

Hawana maarifa/
wale wachukuao mti wa sanamu yao ya kuchonga;*
wamwombao Mungu asiyeweza kuokoa.

Hubirini, toeni habari;*
naam, na wafanye mashauri pamoja;

ni nani aliyeonesha haya tangu zamani za kale?*
ni nani aliyeyahubiri hapo zamani?

Si mimi, BWANA?*
wala hapana Mungu zaidi ya mimi;

Mungu mwenye haki, mwokozi;*
hapana mwingine zaidi ya mimi.

Niangalieni mimi, mkaokolewe,*
enyi ncha zote za dunia;

maana mimi ni Mungu;*
hapana mwingine.

Kwa nafsi yangu nimeapa,/
neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki,*
wala halitarudi,

ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa,*
kila ulimi utaapa.

Mmoja ataniambia,*
Kwa BWANA, peke yake, iko haki na nguvu;

naam, watu watamwendea yeye,*
na wote waliomkasirikia watatahayarika.

Katika BWANA wazao wote wa Israeli*
watapewa haki, na kutukuka.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Wazao wote wa Israeli watapewa haki, na watatukuka katika Bwana.

ANT. III: Njooni mbele ya Bwana, mkiimba kwa furaha.

Zab.100 Wimbo wa sifa
Bwana awaita wote aliowakomboa, waimbe utenzi wa ushindi (Mt. Athanasius)

Mwimbieni Mungu*
enyi walimwengu wote!

Mwabuduni Mungu kwa furaha,*
nendeni kwake mkiimba kwa shangwe!

Jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mungu./
Yeye ndiye aliyetuumba, nasi tu mali yake;*
sisi ni watu wake, na kondoo wa malisho yake.

Pitieni milango ya Hekalu lake kwa shukrani,/
ingieni katika makao yake kwa sifa.*
Mpeni shukrani, na kulisifu jina lake.

Mungu ni mwema;/
upendo wake mkuu ni wa milele,*
na uaminifu wake wadumu milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Njooni mbele ya Bwana, mkiimba kwa furaha.

SOMO: Yer.30:21,22
Na mkuu wao atakuwa mtu wa kwao wenyewe, naye mwenye kuwatawala atakuwa mtu wa jamaa yao; nami nitamkaribisha, naye atanikaribia; maana ni nani aliye na moyo wa kuthubutu kunikaribia? Asema BWANA. Nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

KIITIKIZANO
K. Utukufu wa Bwana utakung'aria, Ee Yerusalemu. Kama jua Bwana atachomoza juu yako. (W. Warudie)
K. Utukufu wake utajitokeza katikati yako.
W. Kama jua Bwana atachomoza juu yako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utukufu wa Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Mtazameni yeye aliye Mungu na binadamu: yu aja kutoka kizazi cha Daudi, na hukalia kiti cha enzi, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mtazameni yeye aliye Mungu na binadamu: yu aja kutoka kizazi cha Daudi, na hukalia kiti cha enzi, aleluya.

MAOMBI
Baba alitaka wanadamu wamwone yeye katika Mwanae mpendwa.
W. Jina lako litukuzwe!

Kristo alituletea habari njema:
- kwa njia yetu dunia isikie habari hiyo, na kupata tumaini. (W.)

Tunakusifu na kukushukuru, wewe uliye Bwana wa mbingu na dunia:
- uliye tumaini na furaha ya watu wa vizazi vyote. (W.)

Ujio wa Kristo uliunde upya Kanisa kwa kuamsha ari na nguvu yake,
- ili litoe huduma kwa watu. (W.)

Tunawaombea Wakristo wote wanaoteseka kwa sababu ya imani yao:
- uwadumishe katika tumaini lao. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tunapoungojea ujio wa utawala wa Mungu, tusali tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Kusanya uwezo wako, Bwana; uje kutuokoa na hukumu itakayotupata kwa sababu ya dhambi zetu. Uje na utufanye huru. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.