IJUMAA JUMA LA 1 MAJILIO
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Muumba wa nyota za usiku,
Mwanga wa milele wa taifa,
Mkombozi wetu sisi sote,
Utusikie tukuitapo.
Kwa mwili wa Maria 'likuja,
Tuokoke dhambi na aibu,
Kwa neema yako Mkombozi
Sasa njoo tuponye wadhambi.
Na siku ya hukumu ya mwisho,
Sisi tutakapofufuliwa,
Fika Mkombozi mwenye baraka,
Tupeleke rahani milele.
Irvin Udulutsch OSB
ANT. I: Ee Bwana, uiponye roho yangu, kwani nimekukosea.
Zab.41 Sala ya mgonjwa
Mmoja wenu, anayekula pamoja nami, atanisaliti (Mk.14:18)
Heri mtu anayewashughulikia maskini,*
Mungu atamsaidia wakati wa shida.
Mungu atamlinda na kumweka hai;/
atamfanikisha katika nchi;*
hatamwacha katika makucha ya adui zake.
Mungu atamsaidia awapo mgonjwa;*
na kumpatia nafuu ya maradhi yake.
Nami nilisema: "Nimekukosea wewe, Ee Mungu,*
unihurumie ukaniponye."
Adui zangu husema mabaya juu yangu;*
wanataka nife na kusahauliwa kabisa.
Wanitembeleapo huwa hawana nia njema;/
wanawaza mabaya juu yangu,*
wafikapo nje huwatangazia wengine.
Wote wanichukiao hunong'onezana juu yangu;*
waniwazia mabaya ya kunidhuru.
Husema: “Maradhi haya yatamwua;*
hatatoka tena kitandani mwake!“
Hata rafiki yangu mkuu ambaye nilimtegemea,/
ambaye alishiriki chakula changu,*
amegeuka na kuanza kunishambulia!
Ee Mungu, unionee huruma!*
Unipe nafuu, nami nitawalipiza.
Hivyo nitajua kwamba umenifadhili,*
ikiwa adui zangu hawatanishinda.
Utanitegemeza, kwani natenda yaliyo sawa;*
utaniweka mbele yako milele.
Asifiwe Mungu, Mungu wa Israeli!*
Asifiwe sasa na milele!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Ee Bwana, uiponye roho yangu, kwani nimekukosea.
ANT. II: Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
Zab.46 Mungu yuko upande wetu
Naye ataitwa Emanueli (maana yake, "Mungu yuро рamoја nasi") (Mt.1:23)
Mungu ni kimbilio letu na nguvu yetu;*
yu tayari daima kusaidia wakati wa taabu.
Kwa hiyo hatutaogopa chochote,*
dunia ijapoyeyuka na milima kuanguka baharini;
hata kama bahari ikichafuka na kutisha,*
na vilima vikatikiswa kwa shambulio lake.
Kuna mto ambao maji yake yaufurahisha mji wa Mungu,*
makao matakatifu ya Mungu Mkuu.
Mungu yumo mjini humo, nao hauwezi kutikiswa;*
alfajiri na mapema huuletea msaada.
Mungu anguruma, dunia yayeyuka;*
mataifa yaghadhabika na tawala zatikisika.
Mwenyezi mwenye nguvu, yu pamoja nasi,*
Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.
Njoni mkaone matendo makuu ya Mungu;*
oneni maajabu aliyoyafanya duniani.
Hukomesha vita popote duniani,/
huvunjavunja pinde na mikuki,*
nayo magari ya vita huyateketeza.
Asema: “Nyamazeni!*
jueni kwamba mimi ndimi Mungu!
Mimi natukuzwa na mataifa yote;*
mimi ni mkuu wa ulimwengu wote!"
Mungu, Mungu mwenye nguvu, yu upande wetu,*
Mungu wa Yakobo ni kimbilio letu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni
ngome yetu.
ANT. III: Mataifa yote yatakuja kukuabudu, Ee Bwana.
WIMBO: Ufu.15:3-4. Utenzi wa sifa
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!
Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!
Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako? *
Wewe peke yako ni Mtakatifu.
Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina.
Ant. III: Mataifa yote yatakuja kukuabudu, Ee Bwana.
SOMO: 2Pet.3:8b-9
Mbele ya Bwana, hakuna tofauti kati ya siku moja na miaka elfu; kwake yote ni mamoja. Bwana
hakawii kutimiza yale aliyoahidi kama watu wengine wanavyofikiri kuwa atakawia. Yeye ana saburi
kwa ajili yenu, maana hapendi hata mmoja wenu apotee, bali huwavuta wote wapate kutubu.
KIITIKIZANO
K. Bwana, Mungu Mwenyezi, njoo kwetu, utuokoe.
W. Bwana, Mungu Mwenyezi, njoo kwetu, utuokoe.
K. Utuoneshe uso wa tabasamu, nasi tutakuwa salama.
W. Njoo kwetu, utuokoe.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana, Mungu Mwenyezi, njoo kwetu, utuokoe.
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Nimemwita mwanangu atoke Misri. Atakuja kuwaokoa watu wake.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Nimemwita mwanangu atoke Misri. Atakuja kuwaokoa watu wake.
MAOMBI
Tunapojitayarisha kusherehekea kuzaliwa kwa Kristo, tunaomba ili Kanisa lizaliwe upya wakati huu.
W. Bwana, zaliwa ndani yetu.
Bwana Yesu, mwana wa Maria,
- njoo tena kwetu duniani. (W.)
Utusaidie tuweze kuonesha huruma na heshima kwa wagonjwa wa akili,
- kwa kuwa sisi sote tu watoto wa Mungu. (W.)
Kwa njia ya mahubiri ya Kanisa kuhusu ujio wako,
- uwaangazie wale wautafutao ukweli. (W.)
Ulizaliwa ili ufe kwa ajili ya dhambi zetu:
- tutakapokufa utujalie tuupate uzima wako. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tujumlishe masifu na dua zetu kwa maneno ya Kristo, tukisema:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Kusanya uwezo wako, Bwana; uje kutuokoa na hukumu itakayotupata kwa sababu ya dhambi zetu.
Uje na utufanye huru. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi
na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.