IJUMAA JUMA LA 1 MAJILIO
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.
Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Manabii walitabiri kwamba Mwokozi atazaliwa na bikira.
Adhuhuri
ANT.: Malaika Gabrieli alimwambia Maria, 'Furahi, wewe uliyependelewa
sana! Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote.'
Baada ya Adhuhuri
ANT.: Maria alihangaishwa sana na amkio hilo, akajiuliza: 'Salamu hii
ina maana gani?' Akawaza: 'Nitamzaa Mfalme bila kupoteza ubikira!'
Zab.119:25-32 IV Mwongozo wa Mungu
Nagaagaa chini mavumbini,*
unipe tena uhai kama ulivyoahidi.
Nimeungama niliyotenda, nawe ukanisikiliza;*
unifundishe mwongozo wako.
Unifundishe namna ya kushika amri zako,*
nami nitayatafakari matendo yako ya ajabu.
Niko hoi kwa uchungu;*
unirudishie nguvu kama ulivyoahidi.
Uniepushe na njia ya upotovu;*
unijalie niijue sheria yako.
Nimechagua njia ya uaminifu;*
nimezingatia hukumu zako.
Ee Mungu, nimefuata maagizo yako;*
usikubali niaibishwe!
Nitafuata maagizo yako,*
maana unanipa maarifa zaidi.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.26 Sala ya mtu mwema
Mungu ametuteua tuwe watu wake katika kuungana na Kristo, ili tuwe watakatifu na bila
hitilafu mbele yake (uf.1:4)
Ee Mungu, unitetee,/
maana nimeishi bila hatia,*
nakutumainia wewe bila kusita.
Unijaribu, Ee Mungu, na kunichunguza;*
upime moyo wangu na akili yangu.
Upendo wako mkuu waniongoza;*
nimeishi kufuatana na ukweli wako.
Siandamani na watu wapotovu;*
sishirikiani na watu wanafiki.
Nachukia kujumuika na wabaya;*
wala sitaandamana na waovu.
Nanawa mikono yangu, Ee Mungu,*
kuonyesha kwamba sina hatia;
najiunga na maandamano ya ibada,*
kuzunguka madhabahu yako,
nikiimba wimbo wa kukushukuru,*
na kutangaza matendo yako ya ajabu.
Ee Mungu, napenda makao yako,*
mahali unapokaa utukufu wako.
Usinipatilize pamoja na wenye dhambi,*
wala usinitupe pamoja na wauaji:
Watu ambao matendo yao ni maovu daima,*
watu ambao daima hula rushwa.
Lakini mimi hutenda yaliyo sawa;*
unihurumie na kunikomboa.
Kama nikiwa imara na salama,*
nitamsifu Mungu kati ya jamii kubwa ya watu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.28:1-3,6-9 Kuomba msaada
Nakushukuru Baba, kwa kuwa wewe wanisikiliza (Yoh.11:41)
Nakulilia, Ee Mungu, mwamba wa usalama wangu!/
Unisikilize, usiwe kama kiziwi kwangu;*
nisije nikawa kama wale washukao shimoni kwa wafu.
Unisikilize niombapo msaada,/
niinuapo mikono yangu,*
kuelekea mahali pako patakatifu.
Usinihukumu pamoja na watu wabaya,*
pamoja na watu watendao maovu:
watu wasemao maneno mazuri,*
kumbe wamejaa uhasama moyoni mwao.
Atukuzwe Mungu,*
maana amesikiliza ombi langu.
Mungu ndiye nguvu yangu na ngao yangu;*
namtumainia yeye kwa moyo wangu wote.
Ananisaidia na kunifurahisha;*
nitamsifu kwa tenzi za shangwe.
Mungu ni nguvu ya watu wake;*
humkinga na kumwokoa mfalme wake mteule.
Ee Mungu, uwaokoe watu wako;/
uwabariki hao watu walio mali yako.*
Uwachunge na kuwalinda hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Manabii walitabiri kwamba Mwokozi atazaliwa na bikira.
Adhuhuri
ANT.: Malaika Gabrieli alimwambia Maria, 'Furahi, wewe uliyependelewa
sana! Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote.'
Baada ya Adhuhuri
ANT.: Maria alihangaishwa sana na amkio hilo, akajiuliza: 'Salamu hii
ina maana gani?' Akawaza: 'Nitamzaa Mfalme bila kupoteza ubikira!'
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Yer.29:11,13
Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani, wala si ya mabaya,
kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtanitafuta, na kuniona, mtakaponitafuta kwa
moyo wenu wote.
K. Mataifa yatalicha jina lako, Bwana.
W. Na wafalme wote wa dunia watatukuza utukufu wako.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Yer.30:18
BWANA asema hivi: Tazama, nitarudisha tena hema za Yakobo zilizohamishwa, na kuyahurumia makao
yake; nao mji huo utajengwa juu ya magofu yake wenyewe, nalo jumba litakaliwa, kama ilivyokuwa
desturi yake.
K. Utukumbuke, Ee Bwana, kwa upendo wako ulio nao kwa watu wako.
W. Njoo, utuokoe.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Bar.3:5-6a
Usiyakumbuke maovu ya baba zetu, bali ukumbuke sasa uweza wako na jina lako. Maana wewe
ndiwe Bwana MUNGU wetu.
K. Njoo, Ee Bwana, usikawie.
W. Uwafungue watu wako kutoka dhambi zao.
SALA:
Tuombe: Kusanya uwezo wako, Bwana; uje kutuokoa na hukumu itakayotupata kwa sababu ya dhambi
zetu. Uje na utufanye huru. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.