Generic placeholder image

IJUMAA JUMA LA 20 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Jinsi Bwana alivyo mwema! Litukuzeni jina lake takatifu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Mimi mzabibu mtakatifu,
Autunzao Babangu.
Kila tawi lisozaa matunda,
Baba yangu hulikata.
Kila tawi lizaalo lakini,
Hulichenga kwa makini;
Hulichenga ili lipate zaa
Mengi ajabu matunda.

Jueni mkikaa ndani yangu,
Nitakaa ndani yenu.
Lipate kuzaa matunda tawi,
Sheti liungane na mti.
Kwa hiyo basi ninyi mtashindwa
Kuzaa yenu matunda,
Ikiwa ninyi pamoja na mimi
Si mmoja mzabibu.

Mimi ndo uzaao mzabibu,
Ninyi mu matawi yangu.
Yeye ndani yangu anayekaa
Ndani yake nitakaa.
Na hapo ndipo mtakapozaa
Matunda mengi ajaa,
Lakini cho chote hamtazaa,
Mbali nami mkikaa.

ANT. I: Uniumbie moyo safi, Ee Mungu; unitie roho thabiti.

Zab.51 Kuomba msamaha
Jirekebisheni upya rohoni na katika fikra zenu. Vaeni hali mpya ya utu (Ef.4:23-24)

Unihurumie, Ee Mungu,*
kwa sababu ya upendo wako mkuu;

ufutilie mbali uovu wangu,*
kwa sababu ya huruma yako kuu.

Unioshe kabisa kosa langu;*
unisafishe dhambi yangu.

Nakiri kabisa makosa yangu,*
daima naiona waziwazi dhambi yangu.

Nimekukosea wewe peke yako,*
nimetenda yaliyo mabaya mbele yako.

Hivyo wafanya sawa unaponihukumu,*
una haki kabisa unaponiadhibu.

Mimi ni mkosefu tangu kuzaliwa kwangu,*
mwenye dhambi tangu tumboni mwa mama yangu.

Wewe wataka unyofu wa ndani;*
hivyo nifundishe hekima moyoni.

Uniondolee dhambi, nitakate;*
unioshe, niwe mweupe pе.

Hapo nitaweza kufurahi tena;*
nitashangilia tena ingawa uliniponda.

Ugeuze uso wako, usiziangalie dhambi zangu;*
ukayafute makosa yangu yote.

Ee Mungu, uniumbie moyo safi,*
uweke ndani yangu roho mpya na thabiti.

Usinitupe mbali nawe;*
usiniondolee Roho wako mtakatifu.

Unifanye nifurahi tena kwa kuniokoa,*
unijalie moyo radhi wa utii.

Hapo nitawafundisha wakosefu mwongozo wako,*
nao wenye dhambi watarudi kwako.

Ee Mungu, Mungu mwokozi wangu, uniokoe na kifo,*
nami nitatangaza kwa furaha uadilifu wako.

Ifumbue midomo yangu, Ee Bwana,*
nipate kutangaza sifa zako.

Kwa kweli wewe hupendezwi na sadaka,/
ama sivyo mimi ningalikutolea.*
Wewe huna haja na sadaka za kuteketezwa.

Sadaka yangu kwako, Ee Mungu, ni moyo mnyofu;*
wewe, Ee Mungu, hukatai moyo mnyofu na mtiifu.

Ee Mungu, uutendee mji Sion mema:*
jenga tena upya kuta za Yerusalemu.

Hapo utapendezwa na sadaka za kweli;/
dhabihu na sadaka za kuteketezwa*
na fahali watatolewa sadaka madhabahuni pako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Uniumbie moyo safi, Ee Mungu; unitie roho thabiti.

ANT. II: Furahi, Ee Yerusalemu, maana kwa njia yako watu wote watakusanywa pamoja mbele ya Bwana.

WIMBO: Tob.13:8-11,13-15 Shukrani ya taifa lililokombolewa
Akanionesha mji mtakatifu, yaani Yerusalemu,... uking'aa kwa utukufu wa Mungu (Ufu.21:10-11)

Naam, nitaushangilia ukuu wake.*
Watu wote wamtolee shukrani katika Yerusalemu.

Ee Yerusalemu! ulio Mji Mtakatifu!/
Atakurudi kwa ajili ya matendo ya wanao; *
Tena atawarehemu watoto wa wenye haki.

Mshukuruni BWANA kwa utauwa;*
Mhimidini Mfalme wa milele.

Maskani yake ijengwe tena ndani yako kwa furaha,/
Ili awafurahishe ndani yako walio wafungwa,*
Na kuwapenda daima ndani yako walio na huzuni.

Mataifa mengi watakuja kutoka mbali,*
Hata kulijia jina la BWANA Mungu,

Wenye tunu mikononi mwao,*
Naam, tunu kwa Mfalme wa mbinguni.

Vizazi vya vizazi watakusifu,*
Na kukuimbia nyimbo za furaha.

Furahi, na kuwashangilia watoto wa wenye haki./
Kwa maana watakusanywa pamoja,*
Na kumhimidi BWANA wa wenye haki.

Wa heri wote wakupendao;*
Watafurahiwa kwa ajili ya amani yako.

Wa heri walioyahuzunikia mapigo yako,*
Kwa sababu watakufurahia;

Wakati watakapoiona fahari yako yote,/
Wakafurahishwa wenyewe hata milele.*
Roho yangu imhimidi Mungu, Mfalme mkuu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Furahi, Ee Yerusalemu, maana kwa njia yako watu wote watakusanywa pamoja mbele ya Bwana.

ANT. III: Sion, msifu Mungu wako, aliyelipeleka neno lake duniani.

Zab.147:12-20 Ni vizuri kumsifu Mungu
Njoo! Mimi nitakuonyesha bibi arusi, mkewe Mwana-kondoo! (Ufu.21:9)

Ee Yerusalemu, umsifu Mungu!*
Umsifu Mungu wako, ee Sion!

Maana ameiimarisha milango yako,*
amewabariki watu waliomo kwako.

Ameweka amani mipakani mwako;*
anakushibisha kwa ngano safi kabisa.

Yeye hupeleka amri yake duniani,*
na neno lake hutekelezwa upesi.

Hutandaza theluji kama pamba,*
hutawanya umande kama majivu.

Huleta mvua ya mawe/
vipande vikubwa vikubwa kama mkate*
na kwa ubaridi wake maji huganda.

Kisha hutoa amri, na maji hayo huyeyuka;*
huvumisha upepo wake, nayo hutiririka.

Humjulisha Yakobo ujumbe wake,*
na Israeli amri na maagizo yake.

Lakini watu wengine hakuwafanyia hayo;*
watu wengine hawayajui maagizo yake.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Sion, msifu Mungu wako, aliyelipeleka neno lake duniani.

SOMO: Gal.2:19b-20
Mimi nimeuawa pamoja na Kristo msalabani, na sasa naishi, lakini si mimi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu. Maisha haya ninayoishi sasa naishi kwa imani, imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili yangu.

KIITIKIZANO
K. Namwita Bwana, aliye Mkuu kabisa, maana amenisaidia. (W. Warudie)
K. Na anijie kutoka mbinguni na kuniokoa.
W. Maana amenisaidia.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Namwita...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Mwangaza utokao juu umetufikia.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Mwangaza utokao juu umetufikia.

MAOMBI
Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote, na mzaliwa wa kwanza kutoka wafu. Vitu vyote hupatanishwa kwa njia yake, kwa kuwa yeye alileta amani kwa kifo chake msalabani. Tumwombe:
W. Bwana Yesu, njoo kwetu leo.

Kwa ubatizo tumeshirikishwa kifo chako:
- utuondolee uroho na wivu, na ututie nguvu na upole wa moyo wako. (W.)

Kwa njia ya Roho Mtakatifu tuliyepewa, sisi tumetiwa muhuri;
- utuimarishe katika utumishi wako, na utusaidie tukushuhudie katika jumuiya yetu. (W.)

Kabla ya kuteswa kwako, ulitamani kula karamu ya pasaka pamoja na wafuasi wako:
- kwa kushiriki Ekaristi Takatifu, utujalie tushiriki pia ufufuko wako. (W.)

Unaendelea kufanya kazi kwa njia ya waamini wako:
- kwa kuwatumia hao, ondoa dhuluma na uharibifu, ukajenge dunia mpya yenye ustawi, uhuru na matumaini. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tunapoungojea ujio wa utawala wa Mungu, tusali tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, utujalie neema zako zote sisi ambao tumekusanyika hapa kusali. Kadiri unavyofanya kazi ndani yetu ili kutudumisha katika njia zako, tupatiwe kitulizo katika maisha haya, na furaha za milele katika maisha yajayo. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.