IJUMAA JUMA 21 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Kor.1:17-25
Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika. Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa. Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu? Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa. Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu. Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.33:1-2,4-5,10-11(K)5
1. Mpigeni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.

(K) Bwana anajaza nchi na fadhili zake.

2. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)

3. Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa,
Huyatangua makusudi ya watu.
Shauri la Bwana lasimama milele,
Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi. (K)

SHANGILIO: Yn.17:17
Aleluya, aleluya!
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya!

INJILI: Mt.25:1-13
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. Watano wao walikuwa wapumbavu na watano wenye busara. Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao. Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika. Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie. Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa. Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie. Akajibu akasema, Amin, nawambia, siwajui ninyi. Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.