IJUMAA JUMA 2 LA KWARESIMA
MASOMO

SOMO 1: Mwa.37:3-4,12-13,17-28
Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa. Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika hii iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula; wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? Haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali. Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:16-21(K)5
1. Akaiita njaa iijilie nchi,
Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
Alimpeleka mtu mbele yao,
Yusufu aliuzwa utumwani.

(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.

2. Walimwumiza miguu yake kwa pingu,
Akatiwa katika minyororo ya chuma.
Hata wakati wa kuwadia neno lake,
Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)

3. Mfalme alituma watu akamfungua,
Mkuu wa watu akamwachia.
Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,
Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)

SHANGILIO: Yn.3:16
Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee; Kila mtu amwaminiye huwa na uzima wa milele.

INJILI: Mt.21:33-43,45-46
Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu, Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza wakawatenda vile vile. Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake. Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake. Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata, waliwaogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.

MAOMBI
Ndugu zangu, sisi sote tu wafanya kazi katika shamba la Bwana. Tuombe neema ya Mungu ili siku ya mwisho tupate tuzo lake. Ee Mwenyezi, Bwana wetu twakuomba:

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uweke watendakazi wema katika shamba lako, yaani Kanisa, ili watuongoze vema kwenye njia ya wokovu.

2. Kwa ujumbe huu wa Kwaresima, watu wote wenye mamlaka wajiweke chini ya utawala wa Mwanao, ili wafanye kile tu chenye kukupendeza wewe na watu wako.

3. Utuepushe na wivu, chuki, tamaa ya mali au madaraka, ili vipaji ulivyomjalia kila mmoja wetu viwe sababu ya furaha, amani na upendo wa kidugu kati yetu.

4. Uwapokee marehemu wetu katika ufalme wako, hasa wale waliouawa kwa sababu ya kuvitumia vema vipaji ulivyowajalia.

Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Mwanao, Bwana na Mwokozi wetu. Amina.