IJUMAA JUMA LA 34
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Sasa siku imekwisha
Bali Pendo asokoma
Aishi hapa daima;
Vivuli vinatoweka
Bali tumaini shindi
Laondoa kila hofu.
Baba mwenye kutupenda,
Usomtupa ye yote,
Pokea yetu mioyo,
Ilotokana na Pendo;
Tulinde usingizini,
Tutunze tuamkapo,
Daima uwe karibu!
Giza linajiingiza,
Bali Mwanga usoisha
Unaangaza usiku;
Wewe u pamoja nasi,
Milele watujalia
Tuione nguvu mpya;
Kuungama kweli yako,
Kwa upendo tu wamoja,
Sote tuna tumaini
La ile heri ya mbingu,
Na tujaliwe kuona,
Kwa kumiliki mapendo,
Mwanga-milele wa Pendo!
ANT. I: Ee Bwana, niepushe na mauti, miguu yangu isijikwae.
Zab.116:1-9 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Ni lazima sisi sote kupitia katika taabu nyingi ili tuingie katika Ufalme wa Mungu(Mate.14:22)
Nampenda Mungu, kwa maana anisikia,*
maana amesikiliza kilio cha ombi langu.
Yeye hunisikiliza*
kila ninapomlilia.
Hatari ya kifo ilinizunguka,/
vitisho vya kaburi vilinivamia;*
nilijawa mahangaiko na majonzi.
Kisha nikamlilia Mungu:*
"Ee Mungu, tafadhali unisalimishe!”
Mungu amejaa wema na haki;*
Mungu wetu ni mwenye huruma.
Mungu huwalinda wanyofu;*
nilikuwa nimekandamizwa, naye akaniokoa.
Uwe na utulivu mkuu, ee roho yangu,*
kwa maana Mungu amenitendea vyema.
Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu;*
akanilinda nisije nikaanguka.
Basi, nitatembea mbele yake Mungu,*
katika nchi ya watu walio hai.
Asifiwe Mungu, Mungu wa Israeli!*
Asifiwe sasa na milele!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Ee Bwana, niepushe na mauti, miguu yangu isijikwae.
ANT. II: Msaada wangu utatoka kwa Bwana, aliyeumba mbingu na dunia.
Zab.121 Mungu kinga yetu
Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena(Ufu.7:16)
Ninatazama huko juu milimani;*
msaada wangu watoka wapi?
Msaada wangu watoka kwa Mungu,*
aliyeumba mbingu na dunia.
Hatakuacha uanguke;*
mlinzi wako hasinzii.
Mlinzi wa Israeli*
hasinzii wala halali.
Mungu anakulinda na kukukinga;*
yuko pamoja nawe kukulinda.
Mchana jua halitakuumiza,*
wala mwezi wakati wa usiku.
Mungu anakukinga na majanga yote;*
anayalinda salama maisha yako.
Anakulinda ujapo na uendapo,*
sasa na hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Msaada wangu utatoka kwa Bwana, aliyeumba mbingu na dunia.
ANT. III: Njia zako ni za kweli na za haki, Ee Mfalme wa milele.
WIMBO: Ufu.15:3-4 Utenzi Wa sifa
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!
Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!
Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako? *
Wewe peke yako ni Mtakatifu.
Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Njia zako ni za kweli na za haki, Ee Mfalme wa milele.
SOMO: 1Kor.2:7-10a
Hekima tunayotumia ni hekima ya siri ya Mungu, hekima iliyofichika, ambayo Mungu aliiazimia
tangu mwanzo kwa ajili ya utukufu wetu. Ni hekima ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa;
maana wangaliielewa, hawangalimsulibisha Bwana wa utukufu. Lakini, ni kama yasemavyo Maandiko
Matakatifu: "Mambo ambayo jicho halijapata kuyaona wala sikio kuyasikia, Mambo ambayo
binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia, wale wampendao."
Hayo ndiyo mambo Mungu aliyotufunulia kwa njia ya Roho wake.
KIITIKIZANO
K. Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, ili atufikishe kwa Mungu. (W. Warudie)
K. Yeye aliyekufa, alifufuliwa kutoka wafu.
W. Ili atufikishe kwa Mungu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Kristo...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Kumbuka rehema zako, Ee Bwana; kama ulivyowaahidia baba zetu.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana.
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Kumbuka rehema zako, Ee Bwana; kama ulivyowaahidia baba zetu.
MAOMBI
Kristo alimfariji mwanamke mjane aliyekuwa amefiwa na mwanae wa pekee; tumwombe yeye,
ambaye atakuja siku ya mwisho kutufuta machozi yetu.
W. Njoo, Bwana Yesu.
Bwana Yesu, uliwafariji hasa maskini na wenye kusumbuliwa:
- uwaangalie kwa huruma wote wenye shida mbalimbali. (W.)
Malaika alikuletea kitulizo kutoka kwa Baba, usiku ule kabla ya kifo chako:
- tunaomba uwaimarishe na kuwatuliza wale wanaokufa. (W.)
Uwajalie wale walio uhamishoni watambue wema wako;
- waweze kurudi kwao, na hatimaye wafike mbinguni kwa Baba
(W.)
Uwaangalie kwa mapendo, wale wote waliojitenga nawe kwa sababu ya dhambi zao:
- uwapatanishe nawe, na uwaunganishe na Kanisa lako. (W.)
Uwaokoe ndugu zetu marehemu;
- uwajalie ukamilifu wa maisha na furaha mbinguni. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tujumlishe masifu na dua zetu kwa maneno ya Kristo, tukisema:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, Msalaba unatufumbulia fumbo la upendo wako: kwa wasioamini, Msalaba huo ni
kweli kikwazo, lakini kwetu sisi tunaoamini, ni alama ya nguvu na hekima yako.
Utufundishe kutafakari utukufu wa mateso ya Mwanao, ili daima tuweze kuamini na kuona
fahari katika Msalaba wake. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi
na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.