IJUMAA JUMA LA 34
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.
Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie -
Ulio mwetu mioyoni -
Mioyo mingine iwashwe.
Kutokana na mwako wake.
Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.
ANT. I: Fadhili zako na ziwe faraja kwangu, kulingana na ahadi yako.
Zab.119:73-80 X Uadilifu wa sheria ya Mungu
Wewe mwenyewe umeniumba na kunitegemeza;*
unijalie akili nijifunze maagizo yako.
Wakuchao wataniona na kufurahi,*
kwa sababu nimelitumainia neno lako.
Najua kwamba hukumu zako ni adili, Ee Mungu,*
na kwamba umeniadhibu kwani wewe ni mwaminifu.
Upendo wako mkuu wanifariji,*
kama ulivyoniahidi mimi mtumishi wako.
Unionee huruma nipate kuishi,*
maana sheria yako ni furaha yangu.
Wenye kiburi waaibike maana wamenifanyia hila,*
lakini mimi nitayatafakari maagizo yako.
Wote wakuchao na waje kwangu,*
wapate kuzijua kanuni zako.
Nizishike amri zako kikamilifu,*
nisije nikaaibishwa.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Fadhili zako na ziwe faraja kwangu, kulingana na ahadi yako.
ANT. II: Uniokoe, Ee Mungu, na wale wanaonishambulia.
Zab.59:1-4,9-10,16-17 Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
Maneno haya ya Mwokozi na yawafundishe watu wote kumtumainia Baba yake kama
watoto wachaji (Eusebius wa Kaisaria)
Ee Mungu wangu, uniokoe na adui zangu;*
unikinge na hao wanaonishambulia.
Uniokoe na hao watu waovu;*
unisalimishe na hao wauaji!
Tazama! Wananivizia waniue;*
watu wakatili wanajiunga dhidi yangu.
Bila ya kosa, hatia au dhambi yangu,/
wanakimbia, Ee Mungu, kujiweka tayari.*
Uinuke, Ee Mungu, ukatazame na kunisaidia!
Nitakuimbia sifa, ewe uliye nguvu yangu;*
maana wewe, Ee Mungu, ni ngome yangu.
Mungu wangu atanijia kwa upendo wake mkuu,*
ataniwezesha mpaka niwaone adui zangu wameshindwa.
Lakini mimi nitaimba sifa za nguvu yako;*
nitashangilia upendo wako mkuu asubuhi;
maana wewe umekuwa ngome yangu imara,*
na kimbilio langu wakati wa shida.
Ewe uliye nguvu yangu, nitakusifu;/
Ee Mungu, wewe u ngome yangu;*
Mungu unayenipenda!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Uniokoe, Ee Mungu, na wale wanaonishambulia.
ANT. III: Ana heri mtu yule ambaye Mungu anamrudi; maana Mungu hujeruhi na kuponya.
Zab.60 Ushindi baada ya kushindwa
Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini. jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu(Yoh.16:33)
Ee Mungu, umetutupa na kututawanya*
umewaka hasira, tafadhali uturudishe.
Umeitetemesha nchi na kuipasua;*
uzibe nyufa zake kwani inabomoka.
Umewatwika watu wako mateso;*
tunayumbayumba kama waliolewa mvinyo.
Umewaashiria wale wanaokuheshimu,*
wapate kuukwepa mshale.
Uwasalimishe hao watu uwapendao;*
utuokoe kwa mkono wako, na kutusikiliza.
Mungu amesema kutoka patakatifu pake:/
"Sasa nitakwenda kwa shangwe kuigawa Shekemu;*
bonde la Sukoti nitaligawa sehemu sehemu.
Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu;/
Efraimu ni kofia yangu ya chuma,*
na Yuda ni fimbo yangu ya enzi.
Moabu ni kama bakuli langu la kunawia,/
kiatu changu nitakitupia Edomu ili kuimiliki.*
Nitapiga kelele ya ushindi juu ya Filistia.“
Ni nani atakayenipeleka kwenye mji wa ngome?*
Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu?
Je, umetuacha kabisa, Ee Mungu?*
Je, huendi tena na majeshi yetu?
Utupatie msaada dhidi ya adui zetu,*
maana msaada wa binadamu haufai kitu.
Tutashinda, Mungu akiwa upande wetu,*
yeye atawaponda adui zetu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Ana heri mtu yule ambaye Mungu anamrudi; maana Mungu hujeruhi na kuponya.
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Kum.1:31b
BWANA alikuchukua kama mtu amchukuavyo mwanawe, njia yote, mliyoiendea, hata mkafikilia mahali hapa.
K. Nitegemeze, Bwana, kadiri ya ahadi yako, nami nitaishi.
W. Na matumaini yangu yasiwe bure.
SALA:
Tuombe: Bwana Yesu Kristo, saa hii ulikwenda njia ya msalaba, kufa kwa ajili ya wokovu wa watu
wote. Kwa huruma yako utusamehe makosa tuliyoyafanya, na kwa uwezo wako utusaidie
tusianguke tena. Unayeishi na kutawala daima na milele.
W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu
---
Adhuhuri: Bar.4:28-29
Kama ilivyokuwa nia yenu kumwasi Mungu, Rudini sasa, mtafuteni mara kumi zaidi; Maana
Yeye aliyeyaleta mapigo haya juu yenu Atawarudishia furaha ya milele pamoja na wokovu wenu.
K. Katika Bwana kuna huruma.
W. Katika yeye kuna utimilifu wa wokovu.
SALA:
Tuombe: Ee Bwana Yesu Kristo, ambaye saa kama hii, dunia nzima ilipokuwa imefunikwa na giza,
ulitundikwa msalabani, ukauawa bila kosa, kwa ajili ya ukombozi wetu; utujalie daima
mwanga huo utakaotufikisha kwenye uzima wa milele. Unayeishi na kutawala daima na milele.
W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Hek.1:13-15
Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea. Kwa maana aliviumba
vitu vyote ili vipate kuwako, na nguvu za uzazi zilizomo ulimwenguni ni za kuleta siha,
wala hakuna ndani yake sumu yo yote ya uharibifu, wala ahera haina milki kama ya
kifalme hapa duniani; maana haki yaishi milele.
K. Bwana ameiokoa nafsi yangu na mauti.
W. Nami nitajimudu mbele yake katika nchi ya walio hai.
SALA:
Tuombe: Ee Bwana Yesu Kristo, ulipokuwa msalabani ulimwahidia ufalme wako yule mwizi aliyetubu;
kwa imani, matumaini na toba tunakuomba huruma yako, ili baada ya kufa kwetu tufurahie
kuingizwa nawe mbinguni. Unayeishi na kutawala daima na milele.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.