IJUMAA JUMA 3 LA KWARESIMA
MASOMO

SOMO 1: Hos.14:1-9
Bwana asema: Ee Israeli, mrudie Bwana, Mungu wako; maana umeanguka kwa sababu ya uovu wako. Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Bwana; mkamwambie, Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo mtakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng'ombe.
Ashuru hatatuokoa; hatutapanda farasi; wala hatutaiambia tena kazi ya mikono yetu, Ninyi ndinyi miungu yetu; maana kwako wewe wasio na baba hupata rehema. Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha. Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyinyoro, na kuieneza mizizi yake kama Lebanoni. Matawi yake yatatanda, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama Lebanoni. Na wao wakaao chini ya uvuli wake watarejea; watafufuka kama ngano, na kuchanua maua kama mzabibu; harufu yake itakuwa kama harufu ya divai ya Lebanoni. Efraimu atasema, Mimi nina nini tena na sanamu? Mimi nimeitika, nami nitamwangalia. Mimi ni kama mberoshi wenye majani mabichi. Kwangu mimi yamepatikana matunda yako. Ni nani aliye na hekima, naye atayafahamu mambo haya? Ni nani aliye na busara, naye atayajua? Kwa maana njia za Bwana zimenyoka, nao wenye haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.81:6-10,13,16
1. Maneno yake nisiyemjua naliyasikia.
Nimelitenga bega lake na mzigo,
Mikono yake ikaachana na kikapu.
Katika shida uliniita nikakuokoa.

(K) Mimi ndimi Bwana Mungu wako, Sikiliza sauti yangu.

2. Nalikuitikia katika sitara ya radi;
Nalikujaribu penye maji ya Meriba.
Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya,
Ee Israeli, kama ukitaka kunisikiliza. (K)

3. Usiwe na mungu mgeni ndani yako;
Wala usimsujudie mungu mwingine.
Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,
Niliyekupandisha toka nchi ya Misri. (K)

4. Laiti watu wangu wangenisikiliza,
Na Israeli angeenenda katika njia zangu;
Naam, ningewalisha kwa unono wa ngano,
Ningewashibisha kwa asali itokayo mwambani. (K)

SHANGILIO: Zab.95:7,8
Leo msifanye migumu mioyo yenu; Lakini msikie sauti yake Bwana.

INJILI: Mk.12:28-34
Mmojawapo wa waandishi alifika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa amewajibu vema, akamwuliza, Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza? Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi. Yule mwandishi akamwambia, Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye; na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhahibu zote pia. Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo.

MAOMBI
Ndugu, leo tunakumbushwa tena kuishika Amri Kuu ya Mapendo na kualikwa kumrudia Mungu kwa moyo mnyofu. Na hivi tuombe neema yake Mungu tukisema:

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Ee Mungu wetu, utujalie Kipindi hiki cha Kwaresima kituongezee ari ya kukupenda wewe zaidi ya chochote.

2. Utukumbushe daima kuwa kukupenda wewe ni kushika amri zako na kuwatendea mema jirani zetu.

3. Utudumishe katika utumishi wako mtakatifu; na kamwe tusithubutu kuanzisha au kuyaendekeza mashindano yasiyotufaa kwa wokovu.

4. Marehemu wetu wapate kitulizo na faraja kwa kuuona uso wako mtukufu huko mbinguni.

Ee Bwana Mungu, amri zako ni dira yetu na kipimo cha uaminifu wetu kwako na kwa jirani zetu. Utupe moyo wa kukupenda zaidi na zaidi. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.