IJUMAA BAADA YA JUMATANO YA MAJIVU
MASOMO

SOMO 1: Isa.58:1-9
Bwana Mungu asema hivi: piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao. Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana? Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.51:3-4,5-6a,18-19
1. Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,
Na kufanya maovu mbele za macho yako.
Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo,
Na kuwa safi utoapo hukumu.

(K) Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.

2. Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu;
Mama yangu alinichukua mimba hatiani.
Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; (K)

3. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako,
Uzijenge kuta za Yerusalemu.
Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki,
Na sadaka za kuteketezwa, na kafara.
Ndipo watakapotoa ng'ombe Juu ya madhabahu yako. (K)

SHANGILIO: Ez.18:31
Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; Jifanyieni moyo mpya na roho mpya.

INJILI: Mt.9:14-15
Siku ile: Yesu alipofika ng'ambo, katika nchi ya Wagerasi, wanafunzi wake Yohane wakamwendea, wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga.

MAOMBI
Ndugu zangu katika Kristo, leo tunakumbushwa kuwa mapato ya matendo mema yanayoambatana na mfungo huu wa Kwaresima ni baraka za Mungu. Basi, tumwombe Mungu ili tufunge vema. Ee Mungu, kwa mfungo huu wa Kwaresima twakuomba:

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Utuepushe na anasa zote na utujalie kuwatendea kwa wema wote tunaofanya nao kazi zetu za kila siku.

2. Kufunga kwetu kusiwe sababu ya mashindano na magomvi; bali kutufanye wanyenyekevu na wakarimu kwa wote wenye shida.

3. Tujaliwe nuru angavu na afya njema tupate kuyafanya matukufu yako.

4. Uwashirikishe marehemu wetu uzima wako wa kimungu huko mbinguni.

Ee Bwana Mungu, utujalie busara ya kusoma ishara za nyakati, tupate kujua ni lini na namna gani tunapaswa kufunga, ili mfungo wetu upate kibali mbele yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.