Generic placeholder image

JUMAMOSI JUMA LA 15 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Dunia na vyote viijazavyo, ni mali ya Bwana: njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Ilikuwa hamu ya moyo wangu,
Kuuona uso wake Mungu;
Ilikuwa hamu ya moyo wangu,
Makaoni mwake kupumzika.

Kidhi, Bwana, hamu ya moyo wangu,
Nikazanapo kujisafisha;
Kidhi, Bwana, hamu ya moyo wangu,
Kuachana na mambo ya dunia.

Ilikuwa hamu ya moyo wangu,
Mfalme wangu kumfuata;
Ilikuwa hamu ya moyo wangu,
Kwimba masifu yake ya milele.

Ilikuwa hamu ya moyo wangu,
Lango la mbingu kulifikia,
Nikute ninachokitamani,
Kinang'aa safi kama jua.

Hiyo ni bado hamu ya moyo wangu,
Ni nini kitakachonizuia
Kuipata haja ya moyo wangu
Kuuona uso wako, Ee Bwana!

ANT. I: Ee Bwana, wewe u karibu nasi: njia zako ni ukweli.

Zab.119:145-152 XIX Kuomba usalama
Nakulilia kwa moyo wangu wote;/
unisikilize, Ee Mungu,*
nami nitazishika kanuni zako.

Nakusifu mara saba kila siku,*
nipate kuyashika mafundisho yako.

Asubuhi na mapema naamka niombe msaada;*
nitaitumainia kabisa ahadi yako.

Nakaa macho usiku kucha,*
ili niyatafakari maagizo yako.

Kwa upendo wako mkuu, Ee Mungu, unisikilize;*
uoneshe huruma yako, ukanisalimishe.

Wadhalimu wangu wakatili wanakaribia,*
watu ambao hawaishiki kamwe sheria yako.

Lakini wewe u karibu nami, Ee Mungu,*
na maagizo yako yote ni ya kuaminika.

Tangu zamani nimejifunza maagizo yako;*
wewe umeyaweka yadumu hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, wewe u karibu nasi: njia zako ni ukweli.

ANT. II: Bwana, hekima yako iwe nami, ili inisaidie na ifanyekazi pamoja nami.

WIMBO: Hek.9:1-6,9-11 Ee Bwana, unijalie hekima
Nitawapeni hekima na uwezo wa kusema hivyo kwamba maadui wenu hawataweza kustahimili wala kupinga (Lk.21:15)

Ee Mungu wa baba zetu,/
BWANA, mwenye kuihifadhi rehema yako,*
umevifanya vitu vyote kwa neno lako;

na kwa hekima yako ukamwumba mwanadamu,*
ili avitawale viumbe vilivyoumbwa nawe,

na kumiliki ulimwengu katika utakatifu na kwa haki,*
na kutoa hukumu kwa unyofu wa moyo.

Nakusihi unipe Hekima,/
ambayo huketi karibu nawe*
katika kiti chako cha enzi,

wala usinikatae mimi*
miongoni mwa watumishi wako.

Mimi niliye mtumwa wako,*
na mwana wa mjakazi wako,

mtu dhaifu asiye na siku nyingi,*
wala sina nguvu kufahamu hukumu na sheria.

Kwa maana mtu ajapokuwa ni mkamilifu*
miongoni mwa wanadamu,

pasipo Hekima itokayo kwako*
atahesabiwa kuwa si kitu.

Na pamoja nawe hukaa Hekima,*
ijuayo matendo yako,

ikawapo hapo ulipoumba ulimwengu,/
ikayatambua yakupendezayo*
na yaliyo mema sawasawa na amri zako.

Uipeleke kutoka mbingu takatifu,*
na kutoka kwa kiti chako kitukufu,

ili ikae nami na kutenda kazi pamoja nami,*
nijifunze yale yakupendezayo.

Kwa maana huyajua mambo yote*
na kuyafahamu;

na katika kutenda kwangu/
itaniongoza kwa njia za kiasi,*
na kunilinda katika utukufu wake.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana, hekima yako iwe nami, ili inisaidie na ifanye kazi pamoja nami.

ANT. III: Kweli ya Bwana itasimama imara milele.

Zab.117 Kumsifu Mungu
Nawaambieni,.. nao watu wa mataifa mengine wamtukuze Mungu kwa sababu ya huruma yake (Rom.15:8-9)

Enyi mataifa yote, msifuni Mungu!*
Enyi watu wote, msifuni!

Upendo wake mkuu kwetu ni thabiti;*
na uaminifu wake wadumu milele!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Kweli ya Bwana itasimama imara milele.

SOMO: Filp.2:14-15
Fanyeni kila kitu bila kunung'unika na bila ubishi, ili mpate kuwa watu safi, wasio na lawama, kama watoto wanyofu wa Mungu wanaoishi katika ulimwengu mbaya na uliopotoka. Mtang'ara kati yao kama nyota zinavyoliangaza anga.

KIITIKIZANO
K. Nilikuita, Ee Bwana; wewe ndiwe kimbilio langu. (W. Warudie)
K. Nimebakiwa na Wewe peke yako, katika nchi ya walio hai.
W. Wewe ndiwe kimbilio langu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Nilikuita...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Uwaangazie, Bwana, watu wakaao gizani, na katika uvuli wa mauti.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Uwaangazie, Bwana, watu wakaao gizani, na katika uvuli wa mauti.

MAOMBI
Tangu milele Mungu alimchagua Maria awe Mama ya Kristo. Kwa sababu hiyo Maria yu juu ya viumbe vingine vyote, vya mbinguni na duniani. Pamoja naye twasema:
W. Roho yangu yamtukuza Bwana.

Baba, Mwanao Yesu alilikabidhi Kanisa mamaye, ambaye ni mfano kamili kwetu, jinsi ya kuwa na imani:
- utuwezeshe kulipokea neno lako kwa imani, kama Mama Maria alivyofanya. (W.)

Bikira Maria aliisikiliza sauti yako, akamleta Neno wako duniani:
- kwa kuitikia mwito wako, utuwezeshe nasi pia kumleta Mwanao kwa watu. (W.)

Ulimwimarisha Mama Maria hata akaweza kusimama karibu na msalaba, na ukamjaza furaha siku ya ufufuko wa Mwanao:
- kwa maombezi yake utufariji, na uliimarishe tumaini letu. (W.)

Utusaidie wakati wa shida na matatizo;
- utuimarishe ndani yako kwa imani na matumaini, ili tuweze kutekeleza matakwa yako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Kwa mara nyingine tena, tumtukuze na kumwomba Baba kwa maneno ya Kristo mwenyewe, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, uliye asili na chanzo cha wokovu wetu, ujalie maisha yetu ya sasa yautangaze utukufu wako hivi hata tupate kukusifu milele mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.