Generic placeholder image

JUMAMOSI JUMA LA 15 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Bwana Mungu na wa vyote Muumba,
Ulimwengu nawe wategemezwa.
Vyote hubadilika na kuoza,
Wewe hapana, wabaki ni Mpya.

Ndiwe faraja na ya mtu kinga,
U Mwamba juu yake wa kujenga.
Ndiwe makao tulivu ya roho,
Yote hutimilika ndani yako.

Asifiwe Baba na Mwana Mungu,
Asifiwe Roho Mtakatifu;.
Na utukuzwe Utatu milele,
Nguvu yetu maisha yetu yote.

ANT. I: Bwana, uwe mdhamini wa mtumishi wako, ili apate mema.

Zab.119:121-128 XVI Utii kwa sheria ya Mungu
Nimefanya mambo mema na maadilifu;*
usiniache katika makucha ya adui zangu.

Uahidi kunisaidia mimi mtumishi wako;*
usikubali wenye kiburi wanidhulumu.

Macho yangu yamechoka kungojea msaada wako,*
kungojea ukombozi ulioahidi.

Unitendee mimi mtumishi wako*
kadiri ya upendo wako mkuu, unifundishe amri zako.

Mimi ni mtumishi wako, unipe maarifa,*
nipate kujua mafundisho yako.

Ee Mungu, sasa ni wakati wa kufanya kitu,*
kwa maana watu wanavunja sheria yako.

Naam, nayapenda maagizo yako,*
kuliko hata dhahabu safi kabisa.

Kwa hiyo nafuata amri zako zote;*
kila njia potovu naichukia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana, uwe mdhamini wa mtumishi wako, ili apate mema.

ANT. II: Mwelekeeni Bwana, mpate kutiwa mwanga.

Zab.34 Sifa kwa wema wa Mungu
Mmeonja na kuona kuwa Bwana ni mwenye fadhili (1Pet.2:3)

I
Nitamtukuza Mungu nyakati zote,*
sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.

Nitamwonea Mungu fahari,*
wanaodhulumiwa wasikie na wafurahi.

Mtukuzeni Mungu pamoja nami,*
sote pamoja tulisifu jina lake.

Nilimwomba Mungu, naye akanisikiliza,*
akaniondolea hofu zangu zote.

Mgeukieni Mungu, mpate kufurahi;*
hamtapata kamwe kusikitika.

Maskini alimlilia Mungu, naye akamsikiliza,*
na kumwokoa katika shida zake zote.

Malaika wa Mungu huwalinda wote wamchao,*
na kuwaokoa katika hatari.

Jioneeni wenyewe jinsi Mungu alivyo mwema.*
Heri wanaokimbilia usalama kwake.

Mcheni Mungu, enyi watakatifu wake;*
wenye kumcha hawakosi mahitaji yao.

Hata simba huona njaa kwa kutindikiwa;*
bali wanaomtii Mungu wana kila kitu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Mwelekeeni Bwana, mpate kutiwa mwanga.

ANT. III: Bwana yu karibu na wale waliovunjika moyo.

II
Njoni, enyi vijana, mkanisikilize,*
nami nitawafundisheni kumcha Mungu.

Je, wapenda kufurahia maisha;*
kuishi maisha marefu na ya fanaka?

Basi, acha kusema mabaya;*
achana na hila.

Jiepushe na uovu, utende mema;*
tafuta amani na kuizingatia.

Mungu huwaangalia waadilifu,*
na kusikiliza malalamiko yao;

lakini huwapinga watendao mabaya,*
awaondoa duniani, wasahauliwa kabisa.

Waadilifu wakimlilia Mungu, huwasikiliza,*
na kuwaokoa katika taabu zao zote.

Mungu yu karibu na waliovunjika moyo;*
huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.

Mateso ya mwadilifu ni mengi,*
lakini Mungu humwokoa katika yote.

Mungu humlinda mtu mwadilifu,*
hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.

Ubaya utawaangamiza watu waovu;*
wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.

Mungu atawaokoa watu wake, *
wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana yu karibu na wale waliovunjika moyo.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Sam.15:22
Je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.

K. Nitatukuzwa kwa sadaka ya sifa.
W. Nitawaonesha waadilifu wokovu wa Mungu.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, Baba Mwenyezi, utujalie mwanga wa Roho Mtakatifu sisi tulio chini ya enzi yako; ili, katika amani na usalama, tuweze kufurahi daima tunapokutukuza. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Gal.5:26;6:2
Basi, tusijivune, tusichokozane wala kuoneana wivu. Chukulianeni mizigo yenu, na hivyo mtatimiza sheria ya Kristo.

K. Jinsi ilivyo vema! Jinsi inavyopendeza! Ndugu wakikaa pamoja kwa umoja!
W. Hapo ndipo Bwana huwapa baraka zake.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, mwanga wa mapendo ya milele, utujalie, daima tuwakapo mapendo yako, tuweze kwa pendo hilo hilo kukupenda wewe zaidi kuliko yote, na kuwapenda wenzetu kwa ajili yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Mika 6:8
Ee mwanadamu, yeye amekuonesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!

K. Nazifurahia sheria zako, Bwana.
W. Sitalisahau neno lako.

SALA:
Tuombe: Ee Bwana, utujalie amani kamili, ili tuweze kufurahia kukutumikia siku zote za maisha yetu, na mwisho, kwa msaada wa Mama Maria, tufike salama mbele yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.