Generic placeholder image

JUMAMOSI JUMA LA 16 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Tuisikilize sauti ya Bwana, tukaingie katika amani yake.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Imbeni, enyi viumbe vyote,
Muimbieni Mungu kwa shangwe!
Kwa furaha mtumikieni,
Mkiimba za ibada tenzi!
Huku mkiimba sifa zake,
Njooni! Njooni mbele zake!
Msifuni Mwenyezi!

Jueni ya kwamba Mungu wetu
Ni Bwana wa zote nyakati!
Yeye ndiye mwumba wetu sisi;
Sisi sote tu viumbe vyake!
Tu watu aliotuumba,
Tu kondoo anaotulisha!
Msifuni Mwenyezi!

Wa fadhili ni mwingi kabisa,
Tumwabuduye wetu Bwana;
Ni wa kudumu wake wema,
Upendo wake mwisho hauna!
Neno lake Yeye ni amini,
La milele, halibadiliki!
Msifuni Mwenyezi!

ANT. I: Ni vema kuliimbia jina lako, Ee Uliye Juu, na kutangaza fadhili zako asubuhi.

Zab.92 Wimbo wa kumsifu Mungu
Matendo ya Mwana wa pekee wa Mungu yanasifiwa (Mt. Athanasius)

Ni vema kukushukuru, Ee Mungu,*
kuimba kwa heshima yako, Ee Mungu Mkuu.

Ni vema kutangaza upendo wako mkuu asubuhi,*
na uaminifu wako kila usiku,

kwa muziki wa zeze na kinanda,*
kwa sauti tamu ya kinubi.

Ee Mungu, matendo yako makuu yanifurahisha;*
nitashangilia kwa sababu ya mambo yote uliyotenda.

Matendo yako, Ee Mungu, ni makuu mno!*
Mawazo yako ni mazito mno!

Mtu mpumbavu hawezi kufahamu,*
wala mjinga hajui jambo hili:

kwamba waovu waweza kusitawi kama nyasi;*
watenda maovu waweza kupata fanaka,

lakini mwisho wao wote ni kuangamia milele;*
maana wewe, Ee Mungu, ni mkuu milele.

Maana tazama, Ee Mungu,/
adui zako hakika wataangamia;*
Wote watendao maovu, watatawanyika!

Wewe umenipa nguvu kama nyati;*
umenimiminia mafuta ya furaha.

Kwa macho nimeona adui zangu wameshindwa;*
nimesikia kilio chao watendao maovu.

Waadilifu husitawi kama mtende;*
hukua kama mwerezi wa Lebanon!

Kama mti uliopandwa katika nyumba ya Mungu,*
wanasitawi katika nyua za Mungu wetu.

Ingawa wamezeeka, wataendelea kuwa na nguvu;*
wapate kuutangaza uadilifu wa Mungu,

na kwamba hamna uovu wowote,*
kwake yeye aliye ngome yangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ni vema kuliimbia jina lako, Ee Uliye Juu, na kutangaza fadhili zako asubuhi..

ANT. II: Nitawapeni moyo mpya, na kuwatia roho mpya.

WIMBO: Eze.36:24-28 Bwana atawapa watu wake uzima mpya
Watakuwa watu wake, naye atakuwa Mungu wao; jina lake ni Mungu pamoja nao (Ufu.21:3)

Nitawatwaa kati ya mataifa,/
nami nitawakusanya na kuwatoa katika chi zote,*
na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe.

Nami nitawanyunyizia maji safi,*
nanyi mtakuwa safi;

nitawatakaseni na uchafu wenu wote,*
na vinyago vyenu vyote.

Nami nitawapa ninyi moyo mpya,*
nami nitatia roho mpya ndani yenu,

nami nitatoa moyo wa jiwe/
uliomo ndani ya mwili wenu,*
nami nitawapa moyo wa nyama.

Nami nitatia roho yangu ndani yenu,*
na kuwaendesha katika sheria zangu,

nanyi mtazishika hukumu zangu,*
na kuzitenda.

Nanyi mtakaa katika nchi ile*
niliyowapa baba zenu,

nanyi mtakuwa watu wangu,*
nami nitakuwa Mungu wenu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Nitawapeni moyo mpya, na kuwatia roho mpya.

ANT. III: Vinywa vya watoto vyakusifu, Bwana.

Zab.8 Utukufu wa Mungu na cheo cha binadamu
Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa Kanisa, akiwa ndio mkuu wa vitu vyote (Ef.1:22)

Ee Mwenyezi, Bwana wetu,/
jina lako latukuka kote duniani!*
Utukufu wako wafika hata mbinguni;

wasifika na vinywa vya watoto wadogo na wachanga/
Wewe uko imara mbele ya wapinzani wako;*
wawakomesha maadui na waasi.

Nikiangalia anga,/
kazi ya vidole vyako mwenyewe,*
mwezi na nyota ulivyoviumba:

mtu ni nini, Ee Mungu, hata umfikirie?*
Mwanadamu ni nini hata umjali?

Hata hivyo, ulimfanya mdogo kidogo tu,/
kuliko wewe mwenyewe,*
na umemvika taji ya utukufu na heshima.

Ulimpa mamlaka juu ya kazi zako zote;*
uliviweka viumbe vyote chini ya miguu yake:

kondoo, ng'ombe na wanyama wa porini;*
ndege, samaki na viumbe vyote vya baharini.

Ee Mwenyezi, Bwana wetu:*
Jina lako latukuka duniani kote!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Vinywa vya watoto vyakusifu, Bwana.

SOMO: 2Pet.3:13-14
Kufuatana na ahadi zake, twangojea mbingu mpya na dunia mpya ambayo imejaa uadilifu. Kwa hiyo, wapenzi wangu, mkiwa mnangojea Siku hiyo, fanyeni bidii kuwa safi kabisa, bila hatia mbele ya Mungu, na kuwa na amani naye.

KIITIKIZANO
K. Midomo yangu itafurahi nitakapokuimbia. (W. Warudie)
K. Ulimi wangu utasimulia haki yako.
W. Nitakapokuimbia.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Midomo...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Bwana, iongoze miguu yetu katika njia ya amani.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana, iongoze miguu yetu katika njia ya amani.

MAOMBI
Karama ya Mungu haikuwa roho ya woga, bali Roho wa nguvu, upendo na kiasi. Kwa imani na matumaini, tunaomba:
W. Baba, umtume kwetu Roho wako.

Utukuzwe, Ee Mungu, Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo:
- kwa njia ya Kristo umetujalia mema yote ya kiroho. (W.)

Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Mama Maria alimleta Kristo duniani;
- kwa njia ya Kanisa Kristo na azaliwe tena leo katika mioyo ya watu. (W.)

Baba, Roho wako atuondoe katika upweke,
- na atuwezeshe kufungua macho ya vipofu, kumhubiri Neno wako ambaye ni nuru, na kunufaika pamoja maishani. (W.)

Jitihada zetu za kuutafuta utawala wako zisishindwe kwa sababu ya ubinafsi au woga;
- Roho Mtakatifu ahuishe ulimwengu, ili familia zetu zioneshe kuwa kweli dunia imekombolewa. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Kwa mara nyingine tena, tumtukuze na kumwomba Baba kwa maneno ya Kristo mwenyewe, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, Nuru ya kweli isiyo na mwisho, ulifukuze giza la dhambi asubuhi hii, na uzijaze akili zetu matumaini ya ujio wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.