Generic placeholder image

JUMAMOSI JUMA LA 16 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Baba wa milele, Mungu wa pendo,
Ambaye kwa vumbi ulituumba,
Tugeuze kwa neema ya Roho,
Tutie thamani tulio duni.

Utuandae kwa siku ya siku
Atakapokuja Kristo kwa enzi
Kutugeuza tena toka vumbi
Na miili yetu kuing'arisha.

Ee Mungu, hujaonwa, hujaguswa
Viumbe vyote vyakudhihirisha;
Mbegu ya utukufu ndani mwetu
Itachanua tutapokuona.

ANT. I: Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, maana nimeamua kufuata sheria zako.

Zab.119:169-176 XXII Kuomba msaada
Kilio changu kikufikie, Ee Mungu!*
Unipe maarifa kadiri ya ahadi yako.

Ombi langu likufikie;*
uniokoe kama ulivyoahidi.

Nitakutolea sifa kem kem,*
maana wanifundisha kanuni zako.

Nitaimba juu ya agizo lako,*
maana amri zako zote ni za haki.

Daima uwe tayari kunisaidia,*
maana nazifuata amri zako.

Natazamia sana uniokoe, Ee Mungu;*
sheria yako ndiyo furaha yangu.

Unijalie kuishi nipate kukusifu;*
na maagizo yako yanisaidie.

Natangatanga kama kondoo aliyepotea;/
uje kunitafuta miye mtumishi wako,*
maana sikusahau maagizo yako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, maana nimeamua kufuata sheria zako.

ANT. II: Kiti chako cha enzi, Ee Mungu, chadumu milele.

Zab.45 Utenzi wa arusi ya kifalme
Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki (Mt.25:6)

I
Moyo wangu umejaa mawazo mema:/
namtungia mfalme shairi langu,*
ulimi wangu u tayari kama kalamu ya mwandishi mwepesi:

wewe u mzuri kuliko wanadamu wote,/
maneno yako ni fadhili tupu,*
naye Mungu amekubariki milele.

Ewe shujaa, weka upanga wako tayari;*
wewe ni mtukufu na mwenye fahari.

Songa mbele kwa ushindi, utetee haki na ukweli,*
mkono wako ukupatie ushindi mkubwa.

Mishale yako ni mikali,/
hupenya mioyo ya adui za mfalme;*
nayo mataifa huanguka chini yako.

Utawala wako ni kama wa Mungu, wadumu milele;*
wewe wawatawala watu wako kwa haki.

Wapenda uadilifu na kuchukia uovu./
Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuteua,*
na kukumiminia furaha kubwa zaidi kuliko wenzako.

Mavazi yako yanukia marashi na udi,/
wanamuziki wakuimbia katika majumba*
yaliyopambwa kwa pembe za ndovu.

Binti za wafalme ni baadhi ya wanaokulaki,/
naye malkia amesimama kulia kwako,*
amevaa mapambo ya dhahabu safi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Kiti chako cha enzi, Ee Mungu, chadumu milele.

ANT. III: Niliona mji mpya, Yerusalemu, umepambwa kama bi arusi aliye tayari kumlaki mumewe.

II
Nawe binti, sikiliza! Nisikilize kwa makini:*
sahau sasa watu wako na jamaa zako.

Uzuri wako wamvutia mfalme:*
yeye ni bwana wako, lazima umtii.

Watu wa Turo watakuletea zawadi;*
matajiri watataka upendeleo wako.

Binti mfalme anaingia - mzuri kabisa!*
Vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu.

Amevalia vazi la rangi nyingi,*
aongozwa kwa mfalme

akisindikizwa na wanawali wenzake,*
nao pia wanapelekwa kwa mfalme.

Kwa furaha na shangwe wanafika huko,*
na kuingia katika jumba la mfalme.

Ee mfalme, utapata watoto wengi/
watakaotawala badala ya wazee wako;*
utawafanya watawale duniani kote.

Sifa zako nitazieneza kwa vizazi vyote daima,*
nayo mataifa yatakusifu daima na milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Niliona mji mpya, Yerusalemu, umepambwa kama bi arusi aliye tayari kumlaki mumewe.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Dan.6:26b-27
Yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake yatadumu hata mwisho. Yeye huonya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani.

K. Tulieni, mkijua kwamba mimi ni Mungu.
W. Mimi ni mkuu kati ya mataifa; ni mkuu wa ulimwengu.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, Baba Mwenyezi, utujalie mwanga wa Roho Mtakatifu sisi tulio chini ya enzi yako; ili, katika amani na usalama, tuweze kufurahi daima tunapokutukuza. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Rom.15:5-7
Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalie ninyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu, ili ninyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, kama naye Kristo alivyowakaribisheni.

K. Bwana huwafurahia watu wake.
W. Huwapatia wokovu maskini.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, nuru ya mapendo ya milele, utujalie, daima tuwakapo mapendo yako, tuweze kwa hilo hilo kukupenda wewe kuliko yote, na kuwapenda wenzetu kwa ajili yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Filp.4:8,9b
Ndugu zangu, jazeni fikra zenu kwa mambo mema na yanayostahili kusifiwa; mambo ya kweli, bora, ya haki, safi, ya kupendeza na ya heshima. Naye Mungu anayetujalia amani atakuwa pamoja nanyi.

K. Nitakutukuza, Ee Mungu Mfalme wangu.
W. Nitalisifu jina lako milele.

SALA:
Tuombe: Ee Bwana, utujalie amani kamili, ili tuweze kufurahia kukutumikia siku zote za maisha yetu, na mwisho, kwa msaada wa Mama Maria, tufike salama mbele yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.