JUMAMOSI JUMA 17 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Yer.26:11-16,24
Makuhani, na manabii, waliwaambia wakuu na watu wote, wakisema, Mtu huyu amestahili kufa, kwa sababu ametabiri juu ya mji huu, kama mlivyosikia kwa masikio yenu. Ndipo Yeremia akawaambia wakuu wote na watu wote, akisema, Bwana ndiye aliyenituma kuitabiri juu ya nyumba hii, na juu ya mji huu, maneno hayo yote mliyoyasikia. Basi sasa, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, mkaisikilize sauti ya Bwana, Mungu wenu; naye Bwana atayaghairi mabaya aliyoyanena juu yenu. Lakini kwangu mimi, tazama, mimi nipo hapa mikononi mwenu; nitendeni myaonayo kuwa mema na haki mbele ya macho yenu. Lakini jueni yakini ya kuwa, mkiniua, mtajiletea juu yenu damu isiyo na hatia; itakuwa juu yenu, na juu ya mji huu, na juu ya wenyeji wake; kwa maana ni kweli Bwana amenituma kwenu, kuwaambieni yote mliyoyasikia. Ndipo wakuu na watu wote wakawaambia makuhani, na manabii, wakisema, Mtu huyu hastahili kuuawa; kwa maana amesema nasi katika jina la Bwana, mungu wetu. Mkono wa Ahikamu, mwana wa Shafani, ulikuwa pamoja na Yeremia, wasimtie katika mikono ya watu auawe.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.69:14-15,29-30,32–33(K)14
1. Uniponye kwa kunitoa matopeni,
Wala usiniache nikazama.
Na niponywe nao wanaonichukia,
Na katika vilindi vya maji.
Mkondo usinigharikishe, wala vilindi visinimeze,
Wala shimo lisifumbe kinywa chake juu yangu.

(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, Ee Mungu.

2. Nami niliye maskini na mtu wa huzuni.
Mungu, wokovu wako utaniinua.
Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
Nami nitamtukuza kwa shukrani. (K)

3. Walioonewa watakapoona watafurahi,
Enyi mumtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafungwa wake. (K)

SHANGILIO: Zab.119:18
Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.

INJILI: Mt.14:1-12
Mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, Huyo ndiye Yohane Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake. Maana Herode alikuwa amemkamata Yohane, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye. Kwa sababu Yohane alimwambia, Si halali kwako kuwa naye. Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohane kuwa nabii. Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Heorode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lolote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohane Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu akamkata kichwa Yohane mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.