JUMAMOSI JUMA 1 LA KWARESIMA
MASOMO
SOMO 1: Kumb.26:16-19
Musa aliwaambia watu: Leo hivi akuamuru Bwana, Mungu wako, kuzifanya amri hizi na hukumu;
basi uzishike na kuzifanya kwa moyo wako wote na roho yako yote. Umemwungama Bwana leo, kuwa
ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo
yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake; naye Bwana amekuungama hivi leo kuwa taifa
iliyotengwa iwe yake yeye, kama alivyokuahidi, na kuwa yakupasa kushika maagizo yake yote;
na kuwa atakutukuza juu ya mataifa yote aliyoyafanya kwa sifa, na jina na heshima, nawe upate
kuwa taifa takatifu kwa Bwana Mungu wako, kama alivyosema.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:1-2,4-5,7-8(K)1
1. Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote.
(K) Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana.
2. Wewe umetuamuru mausia yako,
Ili sisi tuyatii sana.
Ningependa njia zangu ziwe thabiti,
Nizitii amri zako. (K)
3. Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo,
Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako.
Nitazitii amri zako,
Usiniache kabisa. (K)
SHANGILIO: Mdo.16:14
Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi, hivyo Bwana, atakuwa pamoja nanyi.
INJILI: Mt.5:43-48
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie
adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa
wana wa Baba yetu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea
mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu? Hata watoza
ushuru; je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada?
Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu
wa mbinguni alivyo mkamilifu.
MAOMBI
Kwa Ubatizo, sisi sote tumemwungamia Bwana kuwa ndiye Mungu wetu na tegemeo letu katika maisha yetu yote.
Kwa sababu hiyo tunamwomba tukisema:
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Kwa mfungo huu wa Kwaresima, utuongezee sisi sote bidii ya kuyashika maagizo, amri na hukumu zako zote.
Ee Bwana.
2. Utujalie kulitukuza jina lako kwa matendo mema kwa jirani zetu. Ee Bwana.
3. Tunawaombea maadui zetu na wote wenye kutudhulumu, ili kipindi hiki cha Kwaresima kiwaongoe na kuwatakatifuza.
Ee Bwana.
4. Uwasamehe ndugu zetu marehemu walioshindwa kutimiza mapendo ya kidugu walipokuwa hai hapa duniani, ili wapate
nafasi katika makao yako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Bwana Mungu, Mwenye kuwaangazia jua lako wema na wabaya, utujalie kuutambua wema wako katika matukio ya kila
siku na tukaueneze kwa ndugu zetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.