JUMAMOSI JUMA 21 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: 1Kor.1:26-31
Ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu. Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi; kusudi, kama ilivyoandikwa, Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.33:12-13,18-21(K)12
1. Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
Toka mbinguni Bwana huchungulia,
Huwatazama wanadamu wote pia.

(K) Heri taifa ambalo Bwana aliowachagua kuwa urithi wake.

2. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

3. Nafsi zetu zinamngoja Bwana,
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Maana mioyo yetu itamfurahia,
Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu. (K)

SHANGILIO: Zab.25:4,5
Aleluya, aleluya!
Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako.
Aleluya!

INJILI: Mt.25:14-30
Yesu aliwaelezea wanafunzi wake mfano huu: Mtu aliyetaka kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao. Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na uaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema mtumwa mwema na uaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako. Bwana wake akajibu, akamwambia, wewe mtumwa mbaya na ulegevu, ulijua yakuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake. Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi. Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alichonacho atanyang’anywa. Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.