Generic placeholder image

JUMAMOSI JUMA LA 26 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Tuisikilize sauti ya Bwana, tukaingie katika amani yake.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Imbeni, enyi viumbe vyote,
Muimbieni Mungu kwa shangwe!
Kwa furaha mtumikieni,
Mkiimba za ibada tenzi!
Huku mkiimba sifa zake,
Njooni! Njooni mbele zake!
Msifuni Mwenyezi!

Jueni ya kwamba Mungu wetu
Ni Bwana wa zote nyakati!
Yeye ndiye mwumba wetu sisi;
Sisi sote tu viumbe vyake!
Tu watu aliotuumba,
Tu kondoo anaotulisha!
Msifuni Mwenyezi!

Wa fadhili ni mwingi kabisa,
Tumwabuduye wetu Bwana;
Ni wa kudumu wake wema,
Upendo wake mwisho hauna!
Neno lake Yeye ni amini,
La milele, halibadiliki!
Msifuni Mwenyezi!

ANT. I: Ee Bwana, tunatangaza rehema zako asubuhi, na uaminifu wako wakati wa usiku.

Zab.92 Wimbo wa kumsifu Mungu
Matendo ya Mwana wa pekee wa Mungu yanasifiwa (Mt. Athanasius)

Ni vema kukushukuru, Ee Mungu,*
kuimba kwa heshima yako, Ee Mungu Mkuu.

Ni vema kutangaza upendo wako mkuu asubuhi,*
na uaminifu wako kila usiku,

kwa muziki wa zeze na kinanda,*
kwa sauti tamu ya kinubi.

Ee Mungu, matendo yako makuu yanifurahisha;*
nitashangilia kwa sababu ya mambo yote uliyotenda.

Matendo yako, Ee Mungu, ni makuu mno!*
Mawazo yako ni mazito mno!

Mtu mpumbavu hawezi kufahamu,*
wala mjinga hajui jambo hili:

kwamba waovu waweza kusitawi kama nyasi;*
watenda maovu waweza kupata fanaka,

lakini mwisho wao wote ni kuangamia milele;*
maana wewe, Ee Mungu, ni mkuu milele.

Maana tazama, Ee Mungu,/
adui zako hakika wataangamia;*
Wote watendao maovu, watatawanyika!

Wewe umenipa nguvu kama nyati;*
umenimiminia mafuta ya furaha.

Kwa macho nimeona adui zangu wameshindwa;*
nimesikia kilio chao watendao maovu.

Waadilifu husitawi kama mtende;*
hukua kama mwerezi wa Lebanon!

Kama mti uliopandwa katika nyumba ya Mungu,*
wanasitawi katika nyua za Mungu wetu.

Ingawa wamezeeka, wataendelea kuwa na nguvu;*
wapate kuutangaza uadilifu wa Mungu,

na kwamba hamna uovu wowote,*
kwake yeye aliye ngome yangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, tunatangaza rehema zako asubuhi, na uaminifu wako wakati wa usiku.

ANT. II: Utangazeni ukuu wa Mungu wetu.

WIMBO: Kum.32:1-12 Fadhili alizowatendea Mungu watu wake
Mara ngapi nimejaribu kuwakusanya kwangu watoto wako, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake (Mt.23:37)

Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitanena;*
Na nchi isikie maneno ya kinywa changu.

Mafundisho yangu yatadondoka kama mvua,*
Maneno yangu yatatonatona kama umande;

Kama manyunyu juu ya majani mabichi;*
Kama matone ya mvua juu ya mimea.

Maana nitalitangaza Jina la BWANA;*
Mpeni ukuu Mungu wetu.

Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu;*
Maana, njia zake zote ni haki.

Mungu wa uaminifu, asiye na uovu,*
Yeye ndiye mwenye haki na adili.

Wametenda mambo ya uharibifu,/
Hawawi watoto wake, hii ndiyo ila yao;*
Wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka.

Je! mnamlipa BWANA hivi,*
Enyi watu wapumbavu na wajinga?

Je! yeye siye baba yako aliyekununua?*
Amekufanya, na kukuweka imara.

Kumbuka siku za kale,*
Tafakari miaka ya vizazi vingi;

Mwulize baba yako, naye atakuonesha;*
Wazee wako, nao watakuambia.

Yeye Aliye Juu alipowapa mataifa urithi wao,*
Alipowabagua wanadamu,

Aliweka mipaka ya watu*
Kwa kadiri ya hesabu ya wana wa Israeli.

Maana, sehemu ya BWANA ni watu wake,*
Yakobo ni kura ya urithi wake.

Alimkuta katika nchi ya ukame,*
Na katika jangwa tupu litishalo;

Alimzunguka, akamtunza;*
Akamhifadhi kama mboni ya jicho;

Mfano wa tai ataharikishaye kiota chake;*
Na kupapatika juu ya makinda yake,

Alikunjua mbawa zake, akawatwaa,*
Akawachukua juu ya mbawa zake;

BWANA peke yake alimwongoza,*
Wala hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Utangazeni ukuu wa Mungu wetu.

ANT. III: Bwana, jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani kote!

Zab.8 Utukufu wa Mungu na cheo cha binadamu
Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa Kanisa, akiwa ndio mkuu wa vitu vyote (Ef.1:22)

Ee Mwenyezi, Bwana wetu,/
jina lako latukuka kote duniani!*
Utukufu wako wafika hata mbinguni;

wasifika na vinywa vya watoto wadogo na wachanga/
Wewe uko imara mbele ya wapinzani wako;*
wawakomesha maadui na waasi.

Nikiangalia anga,/
kazi ya vidole vyako mwenyewe,*
mwezi na nyota ulivyoviumba:

mtu ni nini, Ee Mungu, hata umfikirie?*
Mwanadamu ni nini hata umjali?

Hata hivyo, ulimfanya mdogo kidogo tu,/
kuliko wewe mwenyewe,*
na umemvika taji ya utukufu na heshima.

Ulimpa mamlaka juu ya kazi zako zote;*
uliviweka viumbe vyote chini ya miguu yake:

kondoo, ng'ombe na wanyama wa porini;*
ndege, samaki na viumbe vyote vya baharini.

Ee Mwenyezi, Bwana wetu:*
Jina lako latukuka duniani kote!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana, jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani kote!

SOMO: Rom.12:14-16a
Watakieni baraka wote wanaowadhulumu ninyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani. Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wenye kulia. Muwe na wema ule ule, kwa kila mtu. Msijitakie makuu, bali jishughulisheni na watu wadogo.

KIITIKIZANO
K. Midomo yangu itafurahi nitakapokuimbia. (W. Warudie)
K. Ulimi wangu utasimulia haki yako.
W. Nitakapokuimbia.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Midomo...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Bwana, iongoze miguu yetu katika njia ya amani.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana, iongoze miguu yetu katika njia ya amani.

MAOMBI
Mungu Baba ametufanya tuwe ndugu za Mwanae wa pekee, na kwa wakati wote amekaa nasi na kututunza katika mapendo yake. Tumwombe atujalie mahitaji yetu.
W. Bwana, utusaidie katika shughuli zetu.

Tunawaombea wote wanaoshughulika na mipango na ujenzi, katika miji na vijiji vyetu:
- wajalie wazingatie yote yanayothaminiwa na jumuiya. (W.)

Washushie Roho wako wanasanaa, mafundi na wanamuziki:
- kazi zao zilete mabadiliko, furaha na mwamko mpya katika maisha yetu. (W.)

Uwe nasi kama msingi katika yote tunayojenga;
- maana bila Wewe hatuwezi kufanya cho chote vizuri. (W.)

Umetuumba upya katika ufufuko wa Mwanao:
- utupe nguvu ya kuanzisha maisha mapya, na kujenga ulimwengu mpya. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Kwa mara nyingine tena, tumtukuze na kumwomba Baba kwa maneno ya Kristo mwenyewe, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Bwana, tunakushukuru kwa mawazo, maneno na matendo: na kwa kuwa uzima wetu ni kipawa chako, twakuomba sisi wenyewe pamoja na vyote tulivyo navyo, tuwe mali yako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.