Generic placeholder image

JUMAMOSI JUMA LA 26 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.

Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie -
Ulio mwetu mioyoni -
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.

Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho.
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.

ANT. I: Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita, asema Bwana.

Zab.119:81-88 XI Sala wakati wa kudhulumiwa
Niko hoi kwa kukungojea uniokoe;*
naweka tumaini langu katika neno lako.

Macho yangu yanafifia nikingojea ulichoahidi.*
Nauliza:“Utakuja lini kunifariji?”

Nimekunjamana kama kiriba katika moshi,*
hata hivyo sijasahau amri zako.

Nitasubiri mpaka lini?*
Utawaadhibu lini wenye kunidhulumu?

Wenye kiburi, wasiojali sheria yako,*
wamenichimbia mashimo kunitega.

Amri zako zote ni za kuaminika;/
watu waongo wananidhulumu,*
tafadhali unisaidie!

Karibu wangefaulu kuniangamiza,*
lakini mimi sijavunja amri zako.

Unisalimishe kadiri ya upendo wako mkuu,*
nipate kuzingatia maagizo yako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita, asema Bwana.

ANT. II: Wewe, Ee Bwana, umekuwa kimbilio langu, ngome yangu dhidi ya adui.

Zab.61 Kuomba ulinzi
Sala ya mwadilifu atamaniye mambo ya mbinguni (Mt. Hilari)

Usikie kilio changu, Ee Mungu;*
usikilize sala yangu.

Ninakulilia ugenini humu;*
nikiwa nimevunjika moyo.

Unipeleke kwenye mwamba wa usalama,/
maana wewe ndiwe kimbilio langu,*
kinga yangu imara dhidi ya adui.

Uniruhusu nikae hemani mwako milele*
nipate usalama chini ya mabawa yako.

Ee Mungu, umezipokea nadhiri zangu,*
umenijalia mema uliyowaahidia wakuchao.

Umjalie mfalme maisha marefu,*
miaka yake iwe ya vizazi vingi.

Atawale milele mbele yako, Ee Mungu;*
mapendo na uaminifu wako vimlinde.

Hapo nitakuimbia nyimbo za sifa,*
nikizitekeleza kila siku nadhiri zangu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Wewe, Ee Bwana, umekuwa kimbilio langu, ngome yangu dhidi ya adui.

ANT. III: Bwana, unikinge na vitisho vya adui.

Zab.64 Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
Zaburi hii hasa yatualika kuyafikiria mateso ya Bwana (Mt. Augustino)

Usikie, Ee Mungu, usikilize lalamiko langu;*
unilinde maisha yangu na vitisho vya adui.

Unikinge na njama za waovu,*
na ghasia za watu wabaya.

Wananoa ndimi zao kama upanga,*
wanafyatua maneno ya ukatili kama mishale.

Toka mafichoni wanamshambulia mtu mnyofu,*
wanamshambulia ghafula bila kuogopa.

Wanashirikiana katika nia yao mbaya;/
wanapatana mahali pa kuficha mitego yao.*
Wakifikiri: “Hakuna atakayeweza kuiona!”

Hufanya njama zao na kusema:/
"Sasa tumekamilisha mpango.*
Nani atagundua hila zetu?”

Mipango ya siri imefichika moyoni mwa mtu!/
Lakini Mungu atawapiga mishale,*
na kuwajeruhi ghafula.

Atawaangamiza kwa sababu ya maneno yao;*
kila atakayewaona atatikisa kichwa.

Hapo watu wote wataogopa;/
watatangaza aliyotenda Mungu,*
na kufikiri juu ya matendo yake.

Waadilifu watafurahia aliyotenda Mungu,/
watakimbilia usalama kwake.*
Watu wote wema wataona fahari.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana, unikinge na vitisho vya adui.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Kum.8:5b-6
Kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo BWANA, Mungu wako, akurudivyo. Nawe uzishike amri za BWANA, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha.

K. Uchaji wa Bwana ni mtakatifu, wadumu milele.
W. Sheria za Bwana ni za kweli, na zote ni za haki.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, Baba Mwenyezi, utujalie mwanga wa Roho Mtakatifu sisi tulio chini ya enzi yako; ili, katika amani na usalama, tuweze kufurahi daima tunapokutukuza. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: 1Fal.2:2b-3
Uwe hodari, ujioneshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya BWANA, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako.

K. Bwana, uniongoze katika njia ya amri zako.
W. Maana furaha yangu imo katika amri zako.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, mwanga wa mapendo ya milele, utujalie, daima tuwakapo mapendo yako, tuweze kwa pendo hilo hilo kukupenda wewe kuliko yote, na kuwapenda wenzetu kwa ajili yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Yer.6:16
Simameni katika njia kuu, mkaone, mkaulize habari za mapito ya zamani, I wapi njia iliyo njema? Mkaende katika njia hiyo, nanyi mtajipatia raha katika nafsi zenu.

K. Mapenzi yako ni urithi wangu milele.
W. Maana katika hayo moyo wangu unapata furaha.

SALA:
Tuombe: Ee Bwana, utujalie amani kamili, ili tuweze kufurahia kukutumikia siku zote za maisha yetu, na mwisho, kwa msaada wa Mama Maria, tufike salama mbele yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.