Generic placeholder image

JUMAMOSI JUMA LA 33
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Dunia na vyote viijazavyo, ni mali ya Bwana: njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Ilikuwa hamu ya moyo wangu,
Kuuona uso wake Mungu;
Ilikuwa hamu ya moyo wangu,
Makaoni mwake kupumzika.

Kidhi, Bwana, hamu ya moyo wangu,
Nikazanapo kujisafisha;
Kidhi, Bwana, hamu ya moyo wangu,
Kuachana na mambo ya dunia.

Ilikuwa hamu ya moyo wangu,
Mfalme wangu kumfuata;
Ilikuwa hamu ya moyo wangu,
Kwimba masifu yake ya milele.

Ilikuwa hamu ya moyo wangu,
Lango la mbingu kulifikia,
Nikute ninachokitamani,
Kinang'aa safi kama jua.

Hiyo ni bado hamu ya moyo wangu,
Ni nini kitakachonizuia
Kuipata haja ya moyo wangu
Kuuona uso wako, Ee Bwana!

ANT. I: Macho yangu yakutazamia kabla ya kucha.

Zab.119:145-152 XIX Kuomba usalama
Nakulilia kwa moyo wangu wote;/
unisikilize, Ee Mungu,*
nami nitazishika kanuni zako.

Nakusifu mara saba kila siku,*
nipate kuyashika mafundisho yako.

Asubuhi na mapema naamka niombe msaada;*
nitaitumainia kabisa ahadi yako.

Nakaa macho usiku kucha,*
ili niyatafakari maagizo yako.

Kwa upendo wako mkuu, Ee Mungu, unisikilize;*
uoneshe huruma yako, ukanisalimishe.

Wadhalimu wangu wakatili wanakaribia,*
watu ambao hawaishiki kamwe sheria yako.

Lakini wewe u karibu nami, Ee Mungu,*
na maagizo yako yote ni ya kuaminika.

Tangu zamani nimejifunza maagizo yako;*
wewe umeyaweka yadumu hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Macho yangu yakutazamia kabla ya kucha.

ANT. II: Bwana ni nguvu yangu, na wokovu wangu: nitaimba sifa zake.

WIMBO: Kut.15:1-4a,8-13,17-18 Utenzi wa ushindi baada ya kuvuka Bahari ya Shamu
Wale waliomshinda yule mnyama waliimba wimbo wa Musa, Mtumishi wa Mungu (Ufu.15:2-3)

Nitamwimbia BWANA,*
kwa maana ametukuka sana;

Farasi na mpanda farasi *
amewatupa baharini.

BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu;*
Naye amekuwa wokovu wangu.

Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu;*
Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.

BWANA ni mtu wa vita,*
BWANA ndilo jina lake.

Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini;*
Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa,

Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa chungu,*
Vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.

Adui akasema,/
Nitafuatia, nitapata, nitagawanya nyara,*
Nafsi yangu itashibishwa na wao;

Nitaufuta upanga wangu,*
Mkono wangu utawaangamiza.

Ulivuma kwa upepo wako,*
bahari ikawafunikiza;

Wakazama kama risasi*
ndani ya maji makuu.

Ee BWANA, katika miungu*
ni nani aliye kama wewe?

Mtukufu katika utakatifu,/
Mwenye kuogopwa katika sifa zako,*
mfanya maajabu?

Ulinyosha mkono wako wa kuume,*
Nchi ikawameza.

Wewe kwa rehema zako/
Umewaongoza watu uliowakomboa,*
Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu.

Utawaingiza, na kuwapanda*
katika mlima wa urithi wako,

Mahali pale ulipojifanyia,*
Ee BWANA, ili upakae,

Pale patakatifu ulipopaweka imara,*
BWANA, kwa mikono yako.

BWANA atawala*
Milele na milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana ni nguvu yangu, na wokovu wangu: nitaimba sifa zake.

ANT. III: Msifuni Bwana, enyi mataifa yote.

Zab.117 Kumsifu Mungu
Nawaambieni,.. nao watu wa mataifa mengine wamtukuze Mungu kwa sababu ya huruma yake (Rom.15:8-9)

Enyi mataifa yote, msifuni Mungu!*
Enyi watu wote, msifuni!

Upendo wake mkuu kwetu ni thabiti;*
na uaminifu wake wadumu milele!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Msifuni Bwana, enyi mataifa yote.

SOMO: 2Pet.1:10-11
Ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuufanya huo wito wenu mlioitiwa na Mungu uwe jambo la kudumu katika maisha yenu; kama mkiishi namna hiyo hamtaanguka. Kwa namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika Utawala wa milele wa Bwana na Mkombozi wetu Yesu Kristo.

KIITIKIZANO
K. Nilikuita, Ee Bwana; wewe ndiwe kimbilio langu. (W. Warudie)
K. Nimebakiwa na Wewe peke yako, katika nchiya walio hai.
W. Wewe ndiwe kimbilio langu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Nilikuita...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Uwaangazie, Bwana, watu wakaao gizani, na katika uvuli wa mauti.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Uwaangazie, Bwana, watu wakaao gizani, na katika uvuli wa mauti.

MAOMBI
Kristo alijifanya mtu ili atufanye sisi tuwe wana wa Mungu, na anatuombea kwa Mungu Baba. Tumshukuru kwa huruma na upendo wake, tukiomba:
W. Tufungulie hazina ya mapendo yako.

Umetuangaza katika ubatizo;
- tunakutolea siku yetu ya leo. (W.)

Utujalie tukusifu siku nzima;
- utuwezeshe kushika neno lako ko kote tuendako. (W.)

Utufundishe kuitikia neno lako kama Maria Mama yetu;
- neno hilo lizae matunda ndani yetu. (W.)

Utusaidie wakati wa shida na matatizo;
- utuimarishe ndani yako kwa imani na matumaini, ili tuweze kutekeleza matakwa yako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Kwa mara nyingine tena, tumtukuze na kumwomba Baba kwa maneno ya Kristo mwenyewe, tukisema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Bwana, fahari ya ufufuo ituangazie mioyo na akili zetu, ikitawanya vivuli vya mauti na kutuingiza kwenye uangavu wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.