Generic placeholder image

JUMAMOSI JUMA LA 33
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.

ANT. I: Ee Bwana, uniongoze kadiri ya amri zako.

Zab.119:33-40 Kuomba maarifa
Ee Mungu, unioneshe kanuni zako,*
nami nitazishika mpaka mwisho.

Unieleweshe sheria yako,*
niishike kwa moyo wangu wote.

Uniongoze nishike amri zako,*
maana humo napata furaha.

Unipe ari ya kufuata sheria zako,*
sio tamaa ya kupata utajiri.

Uniepushe, nisifuate mambo ya upuuzi;*
unifadhili kama ulivyoahidi.

Unitimizie mimi mtumishi wako ahadi yako;*
ahadi unayowapa wanaokuheshimu.

Uniokoe na lawama ninazoogopa;*
maana hukumu zako ni safi.

Natamani sana kuzitii amri zako;*
unijalie uhai maana wewe ni mwadilifu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ee Bwana, uniongoze kadiri ya amri zako.

ANT. II: Wamtafutao Bwana hawapungukiwi baraka.

Zab.34 Sifa kwa wema wa Mungu
Mmeonja na kuona kuwa Bwana ni mwenye fadhili (1Pet.2:3)

I
Nitamtukuza Mungu nyakati zote,*
sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.

Nitamwonea Mungu fahari,*
wanaodhulumiwa wasikie na wafurahi.

Mtukuzeni Mungu pamoja nami,*
sote pamoja tulisifu jina lake.

Nilimwomba Mungu, naye akanisikiliza,*
akaniondolea hofu zangu zote.

Mgeukieni Mungu, mpate kufurahi;*
hamtapata kamwe kusikitika.

Maskini alimlilia Mungu, naye akamsikiliza,*
na kumwokoa katika shida zake zote.

Malaika wa Mungu huwalinda wote wamchao,*
na kuwaokoa katika hatari.

Jioneeni wenyewe jinsi Mungu alivyo mwema.*
Heri wanaokimbilia usalama kwake.

Mcheni Mungu, enyi watakatifu wake;*
wenye kumcha hawakosi mahitaji yao.

Hata simba huona njaa kwa kutindikiwa;*
bali wanaomtii Mungu wana kila kitu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Wamtafutao Bwana hawapungukiwi baraka.

ANT. III: Itafute amani, ukaifuatie.

II
Njoni, enyi vijana, mkanisikilize,*
nami nitawafundisheni kumcha Mungu.

Je, wapenda kufurahia maisha;*
kuishi maisha marefu na ya fanaka?

Basi, acha kusema mabaya;*
achana na hila.

Jiepushe na uovu, utende mema;*
tafuta amani na kuizingatia.

Mungu huwaangalia waadilifu,*
na kusikiliza malalamiko yao;

lakini huwapinga watendao mabaya,*
awaondoa duniani, wasahauliwa kabisa.

Waadilifu wakimlilia Mungu, huwasikiliza,*
na kuwaokoa katika taabu zao zote.

Mungu yu karibu na waliovunjika moyo;*
huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.

Mateso ya mwadilifu ni mengi,*
lakini Mungu humwokoa katika yote.

Mungu humlinda mtu mwadilifu,*
hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.

Ubaya utawaangamiza watu waovu;*
wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.

Mungu atawaokoa watu wake, *
wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Itafute amani, ukaifuatie.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: 1Fal.8:60-61
Watu wote wa ulimwengu wajue ya kuwa BWANA ndiye Mungu; hakuna mwingine. Mioyo yenu na iwe kamili kwa BWANA, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo.

K. Ndiwe Mungu wangu, unifundishe mapito yako.
W. Uniwezeshe kuishi kadiri ya ukweli wako.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, Baba Mwenyezi, utujalie mwanga wa Roho Mtakatifu sisi tulio chini ya enzi yako; ili, katika amani na usalama, tuweze kufurahi daima tunapokutukuza. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Yer.17:9-10
Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha, nani awezaye kuujua? Mimi, BWANA, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha matunda ya matendo yake.

K. Unisamehe makosa yangu yote.
W. Unizuie nisiwe na kiburi.

SALA:
Tuombe: Bwana Mungu, mwanga wa mapendo ya milele, utujalie, daima tunapowaka mapendo yako, tuweze kwa pendo hilo hilo kukupenda wewe zaidi kuliko yote, na kuwapenda wenzetu kwa ajili yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu..

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Hek.7:27a;8:1
Nayo ni moja, ina uwezo wa kutenda yote; Hekima huenea kwa nguvu nyingi toka pembe hii hata pembe hii ya dunia na kuyaratibisha mambo yote kwa jinsi ya kufaa.

K. Ee Bwana, jinsi gani matendo yako yalivyo makuu.
W. Jinsi gani miradi yako ni ya kustaajabisha.

SALA:
Tuombe: Ee Bwana, utujalie amani kamili, ili tuweze kufurahia kukutumikia siku zote za maisha yetu, na mwisho, kwa msaada wa Mama Maria, tufike salama mbele yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.