JUMAMOSI BAADA YA JUMATANO YA MAJIVU
MASOMO
SOMO 1: Isa.58:9b-14
Bwana asema hivi: Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena
maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa;
ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye Bwana
atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa
yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.
Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa,
Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia. Kama ukigeuza mguu
wako usiihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha,
na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala
kuyatafuta yakupendezayo wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika Bwana;
nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana
kinywa cha Bwana kimenena hayo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.86:1-2,3-4,5-6
1. Ee Bwana, utege sikio lako unijibu,
Maana mimi ni maskini na mhitaji,
Unihifadhi nafsi yangu,
Maana mimi ni mcha Mungu.
Wewe uliye Mungu wangu,
Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
(K) Ee Bwana, unifundishe njia yako; Nitakwenda katika kweli yako.
2. Wewe, Bwana, unifadhili,
Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako,
Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe, Bwana. (K)
3. Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema,
Umekuwa tayari kusamehe,
Na mwingi wa fadhili,
Kwa watu wote wakuitao.
Ee Bwana, uyasikie maombi yangu;
Uisikilize sauti ya dua zangu. (K)
SHANGILIO: Eze.33:11
Ufungue Moyo wetu, ee Bwana, ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
INJILI: Mk.3:20-21
Siku ile: Yesu akaona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate.
Akaacha vyote, akaondoka, akamfuata. Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa
na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao.
Ikawa Mafarisayo na waandishi wakawanung’unukia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na
kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana
haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi,
wapate kutubu.
MAOMBI
Ndugu zangu, Bwana anatuita sisi wakosefu ili tupate wokovu. Lakini twahitaji neema ya Mungu ili
kuitikia mwaliko huo. Basi, tuombe: Ee Bwana Mungu, twakuomba:-
Kiitikio: Bwana utusikie, Bwana utusikilize.
1. Wote wanaoitikia mwaliko wako wa kutubu wasikose kutimiza wajibu wao wa matendo ya huruma kwa wahitaji.
2. Utupe sisi sote moyo wa kuwapenda wakosefu na kuwaleta kwako.
3. Utusamehe kosa la kutotimiza sawasawa wajibu wetu wa kuwasaidia wenye shida, tunapotumia vipaji
ulivyotujalia.
4. Wagonjwa wetu waunganishe mateso yao na ya Kristo Mwokozi wetu na kuyavumilia mpaka mwisho.
Ee Mungu, Mwanao alikuja kwa ajili ya wenye dhambi, ili watubu na kuokoka. Utujalie kukiri daima udhaifu
wetu na tuwe tayari kujirekebisha, ili mateso yake yasipotee bure. Kwa huyo Kristo Bwana wetu. Amina.