Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 13 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana ni mfalme mkuu; njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Ee Kristo, uliye Mwanga wa mbingu
Uliye Mwanga hasa wa ulimwengu,
Unakuja katika yote nuruyo
Kukata kata wa usiku utando.

Cho chote kisicho kweli ndani yetu
Mbele ya kweli yako na kitoweke,
Kusudi wenye mioyo mitulivu
Leo na tuishi bila usumbufu.

Imani thabiti itusaidie,
Na pia tumaini imara kwako;
E Mungu wa mapendo upya tutie
Pendo lako tulilofuja tutilie.

Utatu Mtakatifu twakusifu
Ndani yako itakoma njaa yetu;
Utuhifadhi ndani yako milele
Katika furaha na amani tele.

ANT. I: Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, atapanda mlima wa Bwana.

Zab.24 Mfalme Mkuu
Milango ilifunguka, Kristo alipoingia mbinguni na mwili wake (Mt. Ireneus)

Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Mungu;*
ulimwengu na wote waishio humo ni mali yake.

Yeye ndiye aliyeijenga dunia juu ya bahari;*
akaisimika imara juu ya maji chini ya ardhi.

Nani astahiliye kupanda mlima wa Mungu?*
Nani astahiliye kuingia Hekaluni mwake?

Ni mtu aliye safi kwa matendo na fikira zake;*
asiyeabudu miungu ya uwongo wala kushuhudia uwongo.

Mwenye sifa hizo atapata baraka kwa Mungu;*
Mungu atamwokoa na kumfadhili.

Hiyo ndiyo hali yao watu wamtafutao Mungu;*
hali ya watu wafikao kwa Mungu wa Yakobo.

Haya! Fungukeni enyi malango;/
fungukeni enyi malango ya kale;*
ili mfalme mtukufu aingie.

Nani huyo mfalme mtukufu?/
Ni Mwenyezi, mwenye nguvu na enzi;*
Mwenyezi, hodari vitani.

Fungukeni enyi malango,/
fungukeni enyi malango ya kale,*
ili mfalme mtukufu aingie.

Ni nani huyo mfalme mtukufu?/
Ni Mungu, mwenye nguvu, na mshindi,*
yeye ndiye mfalme mtukufu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, atapanda mlima wa Bwana.

ANT. II: Msifuni Mfalme wa karne zote, katika matendo yenu yote.

WIMBO: Tob.13:1-5b,7-8 Mungu huadhibu, na pia huokoa
Asifiwe Mungu, Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya. (1Pet.1:3)

Amehimidiwa Mungu aishiye milele,*
Na ufalme wake umebarikiwa.

Kwa maana hurudi, na kurehemu tena:/
Hushusha hata kuzimu, na kuinua tena;*
Wala hakuna awezaye kujiepusha na mkono wake.

Enyi bani Israeli, mshukuruni mbele ya mataifa*
Yeye ambaye ametutawanya katikati yao.

Ni nani huyo mfalme mtukufu?/
Ni Mungu, mwenye nguvu, na mshindi,*
yeye ndiye mfalme mtukufu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Msifuni Mfalme wa karne zote, katika matendo yenu yote.

ANT. III: Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.

Zab.33 Utenzi wa kumsifu Mungu
Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa. (Yoh.2:3)

Enyi waadilifu, furahieni aliyotenda Mungu;*
enyi watu wanyofu, msifuni Mungu.

Msifuni Mungu kwa kupiga kinubi;*
mwimbieni kwa zeze la nyuzi kumi.

Mwimbieni wimbo mpya;*
pigeni ngoma kwa ustadi na kushangilia.

Kwa kuwa neno la Mungu ni la kweli;*
na matendo yake yote ni ya kutegemewa.

Mungu apenda uadilifu na haki,*
dunia imejaa upendo wake mkuu.

Mungu aliumba mbingu kwa amri yake,*
vitu vyote vya mbingu viliumbwa kwa neno lake.

Alikusanya maji ya bahari,*
na vilindi vya bahari akavifunga ghalani.

Dunia yote na imche Mungu!*
Enyi watu wote duniani, mheshimuni!

Yeye alisema, na ulimwengu ukaumbwa;*
aliamuru, na vyote vikawapo.

Mungu hupangua mipango ya mataifa,*
na huyabatili mawazo yao.

Lakini mipango ya Mungu hudumu milele;*
azimio lake ladumu vizazi vyote.

Heri taifa ambalo Mungu wake ndiye Mungu!*
Heri wale aliowachagua kuwa watu wake!

Mungu huangalia chini kutoka mbinguni,*
na kuwaona wanadamu wote.

Kutoka kwenye kiti chake cha enzi,*
huwaangalia wote wakaao duniani.

Yeye huunda mioyo ya watu wote,*
yeye ajua kila kitu wanachofanya.

Mfalme hawi salama kwa kuwa na jeshi kubwa;*
wala shujaa hapati ushindi kwa wingi wa nguvu zake.

Farasi hafai kitu kwa kupata ushindi;*
nguvu zake nyingi haziwezi kumwokoa mtu.

Mungu huwaangalia wale wamchao,*
watu wanaotumainia upendo wake mkuu.

Yeye huwaokoa katika kifo,*
na kuwalisha wakati wa njaa.

Sisi tunamtumainia Mungu.*
Yeye ni msaada wetu na ngao yetu.

Twafurahi kwa sababu yake;*
tunalitegemea jina lake takatifu.

Upendo wako mkuu, ukae nasi, Ee Mungu,*
kama vile sisi tunavyokutumainia wewe.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.

SOMO Rom.13:11b,12-13a
Sasa ndio wakati wa kuamka usingizini; naam, wokovu wetu u karibu zaidi sasa kuliko wakati ule tulipoanza kuamini. Usiku unakwisha na mchana unakaribia. Basi, tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga. Mwenendo wetu uwe wa adabu kama inavyostahili wakati wa mwanga.

KIITIKIZANO
K. Mungu ni msaidizi wangu; nitamtumainia yeye. (W. Warudie)
K. Yeye ni kimbilio langu, na wokovu wangu.
W. Nitamtumainia yeye.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mungu...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Bwana ametupatia Mwokozi shujaa, kama alivyoahidi kwa njia ya manabii wake watakatifu.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana ametupatia Mwokozi shujaa, kama alivyoahidi kwa njia ya manabii wake watakatifu.

MAOMBI
Sisi Wakristo, tulioalikwa kushiriki uzima wa Mungu, tumsifu Bwana Yesu, kuhani mkuu wa imani yetu.
W. Wewe ndiwe Mwokozi na Mungu wetu.

Mfalme mtukufu, umetubatiza na kutuingiza katika ukuhani wa kifalme;
- utuwezeshe kukutolea daima sadaka ya sifa. (W.)

Utusaidie tuzishike amri zako,
- ili kwa njia ya Roho Mtakatifu, tuweze kuishi ndani yako, nawe uishi ndani yetu. (W.)

Utujie, ewe Hekima ya milele:
- ukae na kufanya kazi pamoja nasi siku hii ya leo. (W.)

Utusaidie tuweze kuwafikiria na kuwaonea huruma wote tutakao kutana nao,
- ili wapate kitulizo na furaha. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Bwana utukumbuke katika utawala wako, kwa kuwa kwa kufuata mafundisho yako tunasali: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Bwana, uipokee sala yetu ya asubuhi kwa huruma; kwa nuru ya mapendo ya wokovu wako, utuondolee giza mioyoni mwetu ili, sisi tuliookolewa kwa mwanga wa neema yako, tusirudie matendo ya giza. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.