Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 13 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Ewe Nguvu na Tegemeo
La viumbe vyote po pote,
Unadumu milele yote
Bila hata kutikisika;
Lakini kwa utaratibu
Waongoza mabadiliko
Yote ya mwanga kila siku,
Na saa baada ya saa.

Kipe kitambo cha maisha
Mwisho mtulivu kabisa,
Jioni isiyofunikwa
Na vivuli vinavyonuka,
Utujalie tufe vema,
Tufe kitakatifu sana,
Ili tuvikwe utukufu
Wa asubuhi ya milele.

Utusikie, Ewe Baba
Mhisani mwenye huruma,
Kwa njia ya Yesu Kristo,
Neno wako hata milele,
Ambaye, pamoja na Roho,
Roho wako Mtakatifu,
Anaabudiwa milele
Na kila kilo na uhai.

ANT. I: Bwana atampa ushindi Masiha wake.

Zab.20 Kuomba msaada
Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana,ataokolewa (Mate.2:21)

Mungu akusikilize uwapo taabuni;*
Jina la Mungu wa Yakobo liwe ngao yako.

Mungu akupelekee msaada kutoka Hekaluni mwake;*
akutegemeze kutoka mlima Sion.

Ayakumbuke matoleo yako yote;*
sadaka zako za kuteketezwa azipokee.

Akujalie unayotamani moyoni mwako;*
aifanikishe mipango yako yote.

Hapo tutapiga vigelegele kwa ajili ya ushindi wako;/
tutatweka bendera kulitukuza jina la Mungu wetu.*
Mungu akutimizie matakwa yako yote!

Sasa najua kwamba,*
Mungu amemjalia ushindi mfalme wake mteule;

atamsikiliza kutoka patakatifu pake mbinguni;*
atamjalia ushindi mkuu kwa nguvu yake.

Wengine wanajigamba kwa magari yao ya vita;/
wengine wanajigamba kwa farasi wao.*
Lakini sisi twamtegemea Mungu, Mungu wetu.

Hao watajikwaa na kuanguka;*
lakini sisi tutainuka na kuimarika.

Ee Mungu, umjalie mfalme ushindi;*
utusikilize tunapokuomba.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana atampa ushindi Masiha wake.

ANT. II: Tutaimba na kusifu uwezo wako.

Zab.21:1-7,13 Shukrani kwa ushindi
Alikubali kuwa mtu, ili aweze kufufuka na kuishi milele na milele (Mt. Ireneus)

Mfalme anashangilia, Ee Mungu,/
kwa sababu ya nguvu uliyomjalia;*
anafurahi kwa sababu ya ushindi uliompa.

Umemtimizia matakwa ya moyo wake;*
wala hukumkatalia ombi lake.

Umemjia, ukampa baraka na fanaka;*
umemvika taji la dhahabu safi.

Alikuomba maisha, nawe ukampa;*
maisha marefu ya kudumu daima.

Kwa msaada wako ametukuka sana;*
wewe umemjalia fahari na heshima.

Wamjalia baraka zako daima;*
wamjaza furaha kwa kuweko kwako.

Mfalme anamtumainia Mungu;*
kwa upendo wake Mungu Mkuu, atakuwa salama daima.

Utukuzwe, Ee Mungu, kwa sababu ya nguvu zako!*
Tutaimba na kuusifu uwezo wako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Tutaimba na kusifu uwezo wako.

ANT. III: Bwana, ulitufanya tuwe ufalme na makuhani wako, ili tumtumikie Mungu wetu.

WIMBO: Ufu.4:11;5:9,10,12 Wimbo wa waliokombolewa
Wewe ni Bwana na Mungu wetu,*
unastahili utukufu na heshima na nguvu;

maana wewe uliumba vitu vyote,/
na kwa matakwa yako*
kila kitu kimepewa uhai na uzima.

Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu*
na kuivunja mihuri yake,

kwa sababu wewe umechinjwa,/
na kwa damu yako umemnunulia Mungu*
watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani/
wamtumikie Mungu wetu,*
nao watatawala duniani.

Mwanakondoo aliyechinjwa*
anastahili kupokea

uwezo, utajiri, hekima,*
nguvu, heshima, utukufu na sifa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana, ulitufanya tuwe ufalme na makuhani wako, ili tumtumikie Mungu wetu.

SOMO: 1Yoh.3:1a,2
Oneni, basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na, kweli, ndivyo tulivyo. Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba, wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye, kwani tutamwona vile alivyo.

KIITIKIZANO
K. Ee Bwana, neno lako litadumu milele. (W. Warudie)
K. Na ukweli wako utadumu kizazi hata kizazi.'
W. Neno lako litadumu milele.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Ee Bwana...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Roho imemfurahia Mungu, mwokozi wangu yangu.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk. 1:46 - 55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Roho imemfurahia Mungu, mwokozi wangu yangu.

MAOMBI
Kwa njia ya Kristo tumepata kuwa wana wa Mungu; na katika yeye twajua tutakavyokuwa baada ya kufika kwa Baba. Kwa imani na matumaini tunaomba:
W. Kwa huruma yako, Ee Bwana, isikie sala yetu.

Uwaongoze wote wenye madaraka, na viongozi wote wa serikali:
- na uwajalie hekima na haki. (W.)

Wewe ni Bwana na chanzo cha uhuru wetu:
- uwafikishe kwenye uhuru wa watoto wako watu ambao wapo katika vifungo vya akili au vya mwili. (W.)

Uwape vijana ujasiri na nguvu.
- Uwasaidie waweze kuchagua kazi, na kufikia uamuzi wa busara kuhusu maisha yao. (W.)

Uwajalie uvumilivu wa daima wote ambao wamepita umri wa ujana;
- ifungue mioyo ya vijana, ili waweze kuelewana na kupatana nao. (W.)

Uwapokee marehemu katika ufalme wako wa milele;
- thibitisha tumaini letu la kutawala nawe milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Kufuatana na mafundisho ya Bwana wetu, kwa imani na matumaini tunasali: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Tunakushukuru, Ee Bwana, Mungu Mwenyezi, kwa kutulinda hadi jioni hii. Tunakuomba kwa unyenyekevu, sala tunayokutolea ipendeze machoni pako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.