Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 13 LA MWAKA
SALA ZA MCHANA

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.

ANT. I: Heri wanaoishi kadiri ya sheria ya Bwana.

Zab.119:1-8 Sheria ya Mungu
Kumpenda Mungu ni kuzitii amri zake(1Yoh.5:3)

Heri watu wanaoishi bila kosa,*
wanaozingatia sheria ya Mungu.

Heri wanaofuata amri zake,*
wanaomtii kwa moyo wote,

ambao hawatendi uovu kamwe;*
bali daima huzingatia mwongozo wake.

Ee Mungu, umetupatia sheria zako*
ili tuzishike kiaminifu.

Laiti mwenendo wangu uimarike,*
kwa kuzishika kanuni zako!

Nikizingatia maagizo yako yote,*
hapo kweli sitaaibishwa.

Nitakusifu kwa moyo mnyofu,*
nikijifunza hukumu zako adilifu.

Nitazishika sheria zako;*
usiniache hata kidogo.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Heri wanaoishi kadiri ya sheria ya Bwana.

ANT. II: Nitafurahi moyoni kwa kuokolewa nawe.

Zab.13 Kuomba msaada
Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote (Rom.15:13)

Ee Mungu, utanisahau kabisa mpaka lini?*
Utajificha mbali nami mpaka lini?

Mpaka lini nitakuwa na huzuni rohoni mwangu,/
na sikitiko moyoni siku hata siku?*
Mpaka lini adui zangu watafurahia taabu yangu?

Ee Mungu, Mungu wangu;*
uniangalie na kunijibu.

Uniangazie macho yangu,*
nisipatwe na usingizi wa kifo.

Usikubali adui zangu waseme: "Tumemweza huyu!“*
Usiwaache hao wafurahie kuanguka kwangu.

Lakini mimi nautumainia upendo wako mkuu;*
moyo wangu na ufurahie wokovu utokao kwako.

Nitakuimbia wewe, Ee Mungu,*
kwa sababu umenijalia mema.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Nitafurahi moyoni kwa kuokolewa nawe.

ANT. III: Mungu aliwafanya watu wote wafungwa wa ukaidi, ili awadhihirishie wote huruma yake.

Zab.14. Uovu wa watu
Pale dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi (Rom.5:20)

Wapumbavu hujisemea: “Hakuna Mungu."/
Wote ni wafisadi, wametenda mambo ya kuchukiza;*
hakuna atendaye chochote kilicho chema!

Toka mbinguni Mungu awachungulia wanadamu,/
aone kama kuna yeyote mwenye busara,*
kama kuna mtu anayemcha Mungu.

Wote kwa pamoja wamepotoka, wote wameharibika;*
hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja.

Mungu asema:*
"Je, wote watendao maovu hawana akili?

Huwakandamiza watu wangu ovyo,/
kama vile watu walavyo mkate;*
wala hawaniombi msaada."

Hapo watatetemeka kwa hofu,*
kwani Mungu awaunga mkono watu waadilifu.

Waovu hupotosha mipango ya mtu mnyonge,*
lakini Mungu ndiye kimbilio lake.

Laiti wokovu umfikie Israeli kutoka Sion!*
Mungu atakaporekebisha hali ya watu wake,

watu wa Yakobo watashangilia,*
naam, watu wa Israeli watafurahi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Mungu aliwafanya watu wote wafungwa wa ukaidi, ili awadhihirishie wote huruma yake.

MASOMO

Kabla ya Adhuhuri: Yer.17:7-8
Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.

K. Bwana hawanyimi chema cho chote wale wasio na hatia.
W. Bwana, Mungu wa majeshi, ana heri mtu anayekutumainia wewe.

SALA:
Tuombe: Mwenyezi Mungu wa milele, uliyewapelekea mitume Roho wako Mtakatifu saa hii, umtume kwetu Roho huyo huyo wa upendo, ili tuweze kukushuhudia kiaminifu mbele ya watu wote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Adhuhuri: Mit.3:13-15
Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi. Yeye ana thamani kuliko marijani, Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye.

K. Ee Bwana, waupenda unyofu wa moyo.
W. Umenifundisha hekima moyoni mwangu.

SALA:
Tuombe: Ee Mungu Mwenyezi, uliyemfumbulia Petro mpango wako wa kuwakomboa watu wote, twakuomba uzipokee kazi zetu ili, kwa neema yako, ziendeleze kusudi lako jema la ukombozi. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.
Hatima ya sala ya mchana tazama chini ya ukurasa huu

---
Baada ya Adhuhuri: Ayu.5:17-18
Tazama, yu heri mtu yule Mungu amwadhibuye; Kwa hiyo usidharau kurudiwa na huyo Mwenyezi. Kwani yeye huumiza, lakini tena huuguza; Yeye hutia jeraha, na mikono yake huponya.

K. Ee Bwana, mtendee mtumishi wako kwa upendo.
W. Unifundishe amri zako.

SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, tunakumbuka jinsi ulivyomtuma malaika wako kwa akida Kornelio kumwonesha nia ya wokovu. Ifungue mioyo yetu tupate kuushughulikia wokovu wa dunia kwa ari zaidi, ili Kanisa lako litufikishe mbele yako sisi na watu wote. Kwanjia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.