JUMANNE JUMA 13 LA MWAKA WA 2
MASOMO

SOMO: Am.3:1-8:11-12
Lisikieni neno hili alilolisema Bwana juu yenu, enyi wana wa Israeli, juu ya jamaa yote niliowapandisha kutoka nchi ya Misri, nikisema, Ni ninyi tu niliowajua katika jamaa zote zilizo duniani; kwa sababu hiyo nitawapatiliza ninyi maovu yenu yote. Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana? Je! Simba atanguruma mwituni, asipokuwa na mawindo? Mwanasimba atalia pangoni mwake, ikiwa hakupata kitu? Je! Ndege ataanguka mtegoni juu ya nchi, mahali asipotegewa tanzi? Mtego utafyatuka juu ya nchi, bila kunasa kitu chochote? Je! Tarumbeta itapigwa mjini, watu wasiogope? Mji utapatikana na hali mbaya, asiyoileta Bwana? Hakika Bwana Mungu hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake. Simba amekwisha kuunguruma, ni nani asiyeogopa? Bwana Mungu amenena, ni nani awezaye neno ila kutabiri? Baadhi yenu nimewaangamiza, kama hapo Mungu alipoiangamiza Sodoma na Gomora, nanyi mkawa kama kinga kilichonyakuliwa motoni; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana. Basi nitakutenda hivi, Ee Israeli; na kwa sababu nitakutenda hivi, ujiweke tayari kuonana na Mungu wako, Ee Israeli.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.5:4-7
1. Huwi Mungu apendezwaye na ubaya;
Mtu mwovu hatakaa kwako;
Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako.

(K) Bwana uniongoze kwa haki yako.

2. Unawachukia wote watendao ubatili.
Utawaharibu wasemao uongo;
Bwana humzira mwuaji na mwenye hila. (K)

3. Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako,
Nitaingia nyumbani mwako;
Na kusujudu kwa kicho,
Nikilielekea hekalu lako takatifu. (K)

SHANGILIO: Yn.15:15
Aleluya, aleluya!
Bwana anasema, Siwaiti tena watumwa, lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya!

INJILI: Mt.8:23-27
Yesu alipanda chomboni, wanafunzi wake wakamfuata. Kukawa msukosuko mkuu baharini, hata chombo kikafunikizwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?