Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 15 LA MWAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana ni mfalme mkuu; njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Ee Kristo, uliye Mwanga wa mbingu
Uliye Mwanga hasa wa ulimwengu,
Unakuja katika yote nuruyo
Kukata kata wa usiku utando.

Cho chote kisicho kweli ndani yetu
Mbele ya kweli yako na kitoweke,
Kusudi wenye mioyo mitulivu
Leo na tuishi bila usumbufu.

Imani thabiti itusaidie,
Na pia tumaini imara kwako;
E Mungu wa mapendo upya tutie
Pendo lako tulilofuja tutilie.

Utatu Mtakatifu twakusifu
Ndani yako itakoma njaa yetu;
Utuhifadhi ndani yako milele
Katika furaha na amani tele.

ANT. I: Bwana, uliibariki nchi yako; uliwasamehe watu wako dhambi zao.

Zab.85 Kuliombea fanaka taifa
Mkombozi wetu alipofika duniani, Mungu aliibariki nchi yake (Origen).

Ee Mungu, umeifadhili nchi yako;*
umemjalia Yakobo bahati njema tena.

Umewasamehe watu wako kosa lao;*
umezifuta dhambi zao zote.

Umezuia ghadhabu yako yote;*
umeacha kabisa kuwakasirikia.

Uturekebishe, Ee Mungu, mwokozi wetu;*
uiondoe chuki uliyo nayo juu yetu.

Je, utatukasirikia hata milele?*
Je, ghadhabu yako itadumu kwa vizazi vyote?

Je, hutatujalia tena maisha mapya,*
ili watu wako wakufurahie?

Utuoneshe, Ee Mungu, upendo wako mkuu;*
utujalie wokovu wako.

Nasikia anayosema Mungu aliye Mungu:/
anaahidi kuwapa watu wake waaminifu amani,*
ikiwa hawatarudia upumbavu wao.

Hakika yu tayari kuwaokoa wanaomheshimu,*
na utukufu wake utadumu nchini mwetu.

Upendo wake mkuu na uaminifu vitakutana;*
uadilifu na amani vitakumbatiana.

Uaminifu utachipuka katika nchi;*
uadilifu utashuka toka mbinguni.

Mungu atatuletea fanaka,*
nchi yetu itatoa mazao mengi.

Uadilifu utamtangulia Mungu,*
na kumtayarishia njia yake.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana, uliibariki nchi yako; uliwasamehe watu wako dhambi zao.

ANT. II: Roho yangu yakutamani wakati wa usiku; alfajiri nakutazamia.

WIMBO: Isa.26:1-4,7-9,12 Wimbo baada ya kumshinda adui
Kuta za mji huo zilikuwa zimejengwa juu ya Mawe ya msingi kumi na mawili (Ufu.21:14)

Sisi tunao mji ulio na nguvu;*
Ataamuru wokovu kuwa kuta na maboma.

Wekeni wazi malango yake,*
Taifa lenye haki, lishikalo kweli, liingie.

Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea*
Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.

Mtumainini BWANA sikuzote,*
Maana BWANA ni mwamba wa milele.

Njia yake mwenye haki ni unyofu;*
Wewe uliye mnyofu wainyoosha njia ya mwenye haki.

Naam, katika njia ya hukumu zako*
Sisi tumekungoja, Ee BWANA.

Shauku ya nafsi zetu inaelekea*
Jina lako na ukumbusho wako.

Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku;*
Naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema;

Maana hukumu zako zikiwapo duniani,*
Watu wakaao duniani hujifunza haki.

BWANA, utatuamuria amani,*
Maana ni wewe pia uliyetutendea kazi zetu zote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Roho yangu yakutamani wakati wa usiku; alfajiri nakutazamia.

ANT. III: Bwana, uso wako utuangaze.

Zab.67 Wimbo wa shukrani.
Jueni, basi, kwamba wokovu utokao kwa Mungu umepelekwa kwa watu wa mataifa (Mate.28:28)

Utuonee huruma, Ee Mungu, utubariki;*
utuelekezee uso wako kwa wema;

dunia yote itambue mwongozo wako,*
mataifa yote yajue nguvu yako ya kuokoa.

Watu wote wakutukuze, Ee Mungu;*
mataifa yote yakusifu.

Mataifa yote yafurahi na kushangilia;/
maana wawahukumu watu kwa haki,*
na kuyaongoza mataifa ya dunia.

Watu wote wakutukuze, Ee Mungu;*
mataifa yote yakusifu.

Nchi imetoa mazao yake;*
Mungu, Mungu wetu, ametubariki.

Mungu ametujalia baraka zake,*
watu wote duniani wamche.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana, uso wako utuangaze.

SOMO: 1Yoh.4:14-15
Sisi tumeona na kuwaambia wengine kwamba Baba alimtuma Mwanae awe Mkombozi wa ulimwengu. Kila mtu anayekiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu anaishi katika muungano na mtu huyo, naye anaishi katika muungano na Mungu.

KIITIKIZANO
K. Mungu ni msaidizi wangu; nitamtumainia yeye. (W. Warudie)
K. Yeye ni kimbilio langu, na wokovu wangu.
W. Nitamtumainia yeye.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mungu...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Bwana ametupatia Mwokozi shujaa, kama alivyoahidi kwa njia ya manabii wake watakatifu.

WIMBO WA ZAKARIA Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana ametupatia Mwokozi shujaa, kama alivyoahidi kwa njia ya manabii wake watakatifu.

MAOMBI
Kristo, kwa kumwaga damu yake kwa ajili yetu, alijifanyia taifa jipya la watu kutoka pande zote za dunia. Tumwombe:
W. Kristo, uwakumbuke watu wako.

Kristo, mfalme na mkombozi wetu;
- utusaidie tuweze kufahamu uwezo na upendo wako. (W.)

Kristo, tumaini na nguvu yetu:
- utuimarishe siku ya leo. (W.)

Kristo, kimbilio na nguvu yetu:
- utusaidie tuweze kupigana na udhaifu wetu. (W.)

Kristo, furaha na kitulizo chetu:
- uwe pamoja na maskini na walio pweke. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Bwana utukumbuke katika utawala wako, kwa kuwa kwa kufuata mafundisho yako tunasali: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Mungu Mwenyezi, dunia hii pamoja na wema na uzuri wake ni mali yako; utujalie neema ili, kwa jina lako tuanze kwa furaha siku hii, na tukaijaze matendo ya mapendo kwako na kwa jirani. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.