Generic placeholder image

JUMANNE JUMA LA 15 LA MWAKA
MASIFU YA JIONI

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Ewe Nguvu na Tegemeo
La viumbe vyote po pote,
Unadumu milele yote
Bila hata kutikisika;
Lakini kwa utaratibu
Waongoza mabadiliko
Yote ya mwanga kila siku,
Na saa baada ya saa.

Kipe kitambo cha maisha
Mwisho mtulivu kabisa,
Jioni isiyofunikwa
Na vivuli vinavyonuka,
Utujalie tufe vema,
Tufe kitakatifu sana,
Ili tuvikwe utukufu
Wa asubuhi ya milele.

Utusikie, Ewe Baba
Mhisani mwenye huruma,
Kwa njia ya Yesu Kristo,
Neno wako hata milele,
Ambaye, pamoja na Roho,
Roho wako Mtakatifu,
Anaabudiwa milele
Na kila kilo na uhai.

ANT. I: Bwana anawazunguka watu wake.

Zab.125 Usalama wa watu wa Mungu
Amani... kwa Israeli Wateule wa Mungu (Gal.6:16)

Wale wanaomtumainia Mungu,/
ni kama mlima Sion,*
ambao hautikisiki bali uko imara daima.

Kama Yerusalemu inavyozungukwa na milima,/
ndivyo Mungu awazungukavyo watu wake,*
tangu sasa na hata milele.

Maana hatawaruhusu waovu watawale nchi ya waadilifu;*
wasije waadilifu nao wakafanya maovu.

Ee Mungu, uwe mwema kwa watu wema,*
kwa wale wanaozitii amri zako.

Adhabu unayowapa watu waovu*
uwape pia wanaokiuka miongozo yako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Bwana anawazunguka watu wake.

ANT. II: Msipokuwa kama watoto wadogo, hamwezi kuingia katika ufalme wa mbinguni.

Zab.131 Kumtumainia Mungu kwa utulivu
Jifunzeni kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo (Mt.11:29)

Ee Mungu, nimeachana na kiburi;*
naam, nimeacha majivuno.

Sijishughulishi na mambo makubwamakubwa,*
au mambo makuu yanayoshinda uwezo wangu.

Ila nimetulia tuli na kuwa na amani./
Kama mtoto mchanga alivyo mtulivu kifuani pa mamaye,*
ndivyo roho yangu ilivyo tulivu ndani yangu.

Ee Israeli, umtumainie Mungu,*
tangu sasa na hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Msipokuwa kama watoto wadogo, hamwezi kuingia katika ufalme wa mbinguni.

ANT. III: Bwana, ulitufanya tuwe ufalme na makuhani wako, ili tumtumikie Mungu wetu.

WIMBO: Ufu.4:11;5:9,10,12 Wimbo wa waliokombolewa

Wewe ni Bwana na Mungu wetu,*
unastahili utukufu na heshima na nguvu;

maana wewe uliumba vitu vyote,/
na kwa matakwa yako*
kila kitu kimepewa uhai na uzima.

Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu*
na kuivunja mihuri yake,

kwa sababu wewe umechinjwa,/
na kwa damu yako umemnunulia Mungu*
watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani/
wamtumikie Mungu wetu,*
nao watatawala duniani.

Mwanakondoo aliyechinjwa*
anastahili kupokea

uwezo, utajiri, hekima,*
nguvu, heshima, utukufu na sifa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Bwana, ulitufanya tuwe ufalme na makuhani wako, ili tumtumikie Mungu wetu.

SOMO: Rom.12:9-12
Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema. Pendaneni kidugu; kila mmoja amfikirie kwanza mwenzake kwa heshima. Msilegee katika bidii, muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana. Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida. Salini daima.

KIITIKIZANO
K. Neno lako, Ee Bwana, litadumu milele. (W. Warudie)
K. Na ukweli wako utadumu kizazi hata kizazi.'
W. Neno lako litadumu milele.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Neno...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Roho yangu imemfurahia Mungu, mwokozi wangu.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Roho yangu imemfurahia Mungu, mwokozi wangu.

MAOMBI
Mungu amewaweka imara watu wake katika matumaini. Hakuna kiwezacho kuyavunja matumaini ya wale wampendao. Basi, na tuseme:
W. Baba, wewe ndio tumaini letu.

Twakushukuru, Bwana Mungu,
- kwa kuwa umemjalia mwanadamu utajiri wa hekima na ufahamu. (W.)

Bwana Mungu, unaijua mioyo ya watawala wote:
- uwawezeshe kufanya kazi kwa manufaa ya watu walio chini yao. (W.)

Bwana, wamwezesha mwanadamu kuupamba ulimwengu kwa sanaa:
- uijalie kazi yetu ilete mwanga na tumaini la kweli. (W.)

Hutuachi tujaribiwe kupita nguvu zetu:
- uwaimarishe wanyonge, na uwainue walioanguka dhambini. (W.)

Baba, umewaahidi watu kuwa watashiriki ufufuko wa Mwanao siku ya mwisho:
- uwakumbuke marehemu waliotutangulia wakiwa na tumaini la kupata uzima wa milele. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Kufuatana na mafundisho ya Bwana wetu, kwa imani na matumaini tunasali: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Ee Bwana, twakuomba masifu haya ya jioni yafike mbele ya kiti chako cha huruma, na utujalie baraka na neema, ili zitusaidie kupata wokovu daima na milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.